Asimulia jela ilivyomwandalia mazingira mazuri ya kutunga mashairi

NA BITUGI MATUNDURA, TAIFALEO

KWENYE makala yake ‘Abdilatif Abdalla’s Book Translated to English’ yaliyochapishwa katika Saturday Nation mapema mwaka 2024, alieleza kwamba msomi Ken Walibora alikuwa angali ‘anaandika akiwa kaburini’, zaidi ya miaka mitatu tangu aagane na ulimwengu.

Taswira hiyo ya ukwelikinzani (paradox) iliibuka tena  kwenye Kongamano la 36 la Kiswahili lililofanyika Bayreuth, Ujerumani Kusini, Mei 17 -19, 2024, ambapo tafsiri  ya Kiingereza ya Sauti ya Dhiki (OUP,1973) ilizinduliwa rasmi. Tafsiri hiyo   – The Imaginative Vision of Abdilatif Abdalla’s Voice of Agony huenda ilikuwa mojawapo ya miradi ya mwisho ya Prof Walibora, aliyeaga dunia kufuatia ajali ya barabarani iliyotokea jijini Nairobi mnamo 2020.

Kazi hiyo iliyohaririwa na Prof Annmarie Drurry ina makala za wasomi kama Meg Arenberg, Ngugi wa Thiong’o, Kai Kresse, Ann Biersteker na Abdilatif Abdalla.

Akihutubia katika hafla hiyo, ‘mshairi na mfungwa’, Ustadh Abdilatif Abdalla alisema: “Kitabu hiki si changu, ni chetu. Changu mimi kilikuwa ni ‘Sauti ya Dhiki’ kwa Kiswahili.”

Ustadh Abdalla alibubujikwa na ‘machozi ya dhiki’ na huzuni alipovuta nyuma taswira ya safari yake, katika uanaharakati, iliyomtia matatani serikalini, alipothubutu kuuliza mkondo Kenya ilikuwa imeuchukua, chini ya uongozi wa Mzee Jomo Kenyatta.

Alishangaza hadhira alipomshukuru mtesi wake, Mzee Jomo Kenyatta kwa kumtumbukiza gerezani.

“Mtu wa kwanza ambaye ningependa kumshukuru, na ambaye ndiye sababu hata nikaweza kutunga mashairi haya ni rais wetu wa kwanza wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta. Maanake, kama asingenifunga, huenda ‘Sauti ya Dhiki’ isingaliandikwa. Kwa hiyo, namshukuru sana huko aliko,” anasema Ustadh Abdalla.

Author: Gadi Solomon