Askofu Gwajima akomaa na Kiswahili bungeni, serikali kuanzisha madarasa balozini

Amani Njoka, Swahili hub

Dodoma: Mbunge wa Jimbo la Kawe, Askofu Josephat Gwajima (CCM) amehoji nafasi ya serikali katika kukitangaza Kiswahili duniani kutokana na kukua na kuenea kwake katika bara la Afrika na dunia kwa ujumla. Aliyasema hayo katika mkutano wa pili na kikao cha 4 cha Bunge la 12 jijini Dodoma.

Alilielekeza swali lake kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, pia alitaka kufahamu namna serikali inavyochukua hatua kukibidhaisha Kiswahili katika diplomasia na kuwa fursa ya kiuchumi kwa Watanzania.

“Kwa kuwa Kiswahili ni miongoni mwa lugha 10 zinazozungumzwa zaidi ulimwenguni na lugha ya pili kwa kuzungumzwa barani Afrika, serikali ina mkakati gani kuhahakiki Kiswahili kinakuwa bidhaa hasa wakati wa kuchangia diplomasia ya uchumi na kuwa fursa ya ajira kwa Watanzania?”

Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema, kutokana na Kiswahili kuzungumzwa katika mataifa makubwa mathalani Ujerumani, Marekani, Uingereza na mataifa mengine makubwa, serikali imewaagiza mabalozi kuanzisha vituo vya kufundishia Kiswahili katika balozi zilizopo katika nchi hizo. Kwahiyo, Watanzania watapata fursa ya kuwa walimu katika vituo hivyo na kukuza uchumi wa Watanzania na taifa kwa ujumla.

Vilevile amekiri kwamba ni kweli Kiswahili kinalitangaza taifa nje ya mipaka hasa vyombo mbalimbali, vyombo vya habari vya kimataifa vinakitumia kurusha matangazo yake, ndio maana wanaendeleza juhudi za kukikuza.

Kadhalika, ameeleza namna Rais Magufuli anavyochukua hatua za dhati kukisambaza Kiswahili katika nchi za ukanda wa SADC, kuwahamasisha viongozi wa nchi hizo na hatimaye Kiswahili kuanza kufundishwa katika nchi zao.

Author: Gadi Solomon