Bakita kutembelea vituo vya kufundisha Kiswahili kwa wageni

Gadi Solomon, Mwananchi

Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) limeanzisha mkakati wa kuwaunganisha watoa huduma ya ufundishaji lugha ya Kiswahili kwa wageni kwa kuwaweka pamoja kupitia mtandao wa Whatsapp.

Lengo la Baraza hilo ni kuwawezesha watoa huduma hao kushirikiana na kupata mrejesho kutokana na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo.

Aidha, Baraza hilo limetangaza kuanzia mwezi Agosti mwaka huu litavitembelea na kukagua vituo vyote ambavyo vimeomba kitambuliwa kuvipa vyeti vya utambuzi.

Bakita imeomba ushirikiano wa kila kituo katika kufanikisha zoezi hili muhimu kwa lengo la kuwatambua na kufahamiana katika utendaji kazi wetu wa kubidhaisha lugha ya Kiswahili.

Taarifa iliyotolewa jana na Baraza hilo mtandaoni ilieleza ilisema, “Lengo la kufungua kundi hili ni kuwaunganisha pamoja na kupeana taarifa muhimu zinazohusiana na maendeleo na ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni.”

“Baraza linawapongeza wadau wetu muhimu ambao mnafanya kazi kubwa ya kubidhaisha Kiswahili tuendelea kushirikiana.”

“Hapa tumeunganika BAKITA na vituo vya Kiswahili kwa wageni ambavyo BAKITA lishavitambua,  kuvipa vyeti vya utambuzi na kuvitembelea na vingine bado hatujavipa vyeti  vya utambuzi wala kuvitembelea,” ilieleza taarifa hiyo ya mtandaoni.

 Bakita ndilo balaza lenye jukumu kuratibu na kusimamia vituo vyote vinavyofundisha Kiswahili kwa wageni.

Author: Gadi Solomon