
Ufupisho. Lugha ya Kiswahili inafundishwa katika vyuo vikuu viwili ambavyo ni Chuo Kikuu cha Serikali cha Moscow (Moscow State University) na Chuo Kikuu cha Mahusiano ya Kimataifa (Moscow State University of International Relations). Hata hivyo walimu wanaofundisha somo hilo wameunda umoja wao wa Chama cha Kiswahili Moscow.
Gadi Solomon, Mwananchi
Dar es Salaam. Kasi ya maendeleo ya lugha ya Kiswahili duniani imelisukuma Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) kutoa jumla ya nakala 27 za vitabu kwa Balozi wa Tanzania nchini Urusi, Fredrick Kibuta.
Miongoni mwa vitabu vilivyogawiwa ni Furahia Kiswahili nakala 20, Mwongozo wa Taifa wa Ufundishaji wa Kiswahili kwa Wageni (5) na Kamusi Kuu ya Kiswahili Toleo la 3 nakala (2).
Bakita imechukua hatua hiyo ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango wakati maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani Julai 7 mwaka huu, kuhakikisha wanaendelea juhudi za kukuza Kiswahili nje ya mipaka ya Tanzania kwa vitendo.
Akizungumza leo Jumatano, wakati wa makabidhiano ya vitabu hivyo kwenye Ukumbi wa Mikutano wa baraza hilo, Kijitonyama jijini Dar es Salaam, Mwakilishi wa Balozi wa Tanzania, aliyekabidhiwa vitabu hivyo, Kanali Mohamed Adam amesema vitabu hivyo vitatumika katika kufundishia lugha ya Kiswahili katika vyuo vikuu mbalimbali nchini Urusi.

“Kwa maelezo ya balozi wetu nchini Urusi (Fredrick Kibuta), vitabu hivyo vitagawiwa katika vyuo na taasisi mbalimbali ambazo wanafundisha lugha ya Kiswahili nchini Urusi,” amesema Kanali Adam.
Amesema huo ni utekelaji wa sera ya Serikali katika kuhakikisha Tanzania kupitia ofisi za ubalozi wake inaendelea kuwa chachu ya maendeleo ya Kiswahili duniani.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa BAKITA, Vida Mutasa ambaye ni Mkuu wa Sehemu ya Ukalimani na Tafsiri amesema, hatua hiyo ni ishara namna ambavyo Kiswahili kimeendelea kukubalika kwa kasi duniani.
Mutasa amesema hitaji la watu kujifunza lugha ya Kiswahili limeendelea kwa kasi tangu Shirika la Sayansi, Elimu na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) litangaze tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuadhimisha siku hiyo duniani.
Amesema Baraza hilo litaendelea kushirikiana na ofisi mbalimbali za ubalozi wa Tanzania ili kuhakikisha azma ya Serikali ya kukifanya Kiswahili kuwa nyezo ya ukuzaji uchumi inafanikiwa.
Ameongeza kuwa hii ni faraja kuona Kiswahili kinaendelea kufundishwa katika taasisi na vyuo vikuu mbalimbali nchini Urusi.

Ubalozi wa Tanzania nchini humo uliadhimisha siku ya Kiswahili duniani tarehe 7 Julai 2022. Ambapo maadhimisho hayo yalihudhuriwa na mabalozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Chama cha Kiswahili Moscow (Chakimo), diaspora na wanafunzi wa elimu ya juu.
Maoni Mapya