Bakita yampa tuzo mwanafunzi bora Kiswahili Chuo Kikuu Tumaini

Na Nasra Abdallah

Dar es Salaam. Baraza la Kiswahili Taifa (Bakita), limeanza utaratibu wa kuwatunuku tuzo wanafunzi wanaofanya vizuri somo la Kiswahili katika vyuo vikuu mbalimbali nchini.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Kiswahili wa Bakita, Vida Mutasa alipokuwa akikabidhi tuzo hiyo kwa mwanafunzi aliyefanya vizuri katika somo hilo Chuo Kikuu cha Tumaini, Mary Daudi.

Vida amesema awali walikuwa wakitoa tuzo hizo kwa wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne na cha sita, lakini sasa wameona watoe na kwa vyuo vikuu kama moja ya njia ya kuwahimiza kupenda kusoma lugha hiyo kwa kuwa sasa imekuwa bidhaa ambayo wanaweza kuitumia kujiajiri mara wamalizapo masomo yao.

Katika utoaji wa tuzo hiyo, Bakita wametoa cheti cha utambuzi, Kamusi Kuu ya Kiswahili na Sh300,000 taslimu kwa mshindi.

“Awali tulikuwa tukitoa tuzo hii  kwa kidato cha nne na cha sita lakini sasa hivi kutokana na kuwa bidhaa na kinahitajika kutolewa kwa wageni tumeona tuanze kutoa na vyuoni kwa kuwa kutahitajika walimu wa lugha hii,” amesema Vida.

Mkurugenzi huyo amewataka wanafunzi wanaosoma Kiswahili wajue kwamba sasa hivi Kiswahili ni bidhaa tangu ilipotangazwa kuwa lugha ya kimataifa ambapo watu wengi kutoka mataifa mbalimbali wamekuwa wakitaka kujifunza.

Kuhusu wanaoenda nje ya nchi kufundisha Kiswahili, amesema bado wanaenda kwa kuomba mmojammoja lakini fursa anayoiona bado ipo hapa nchini kwani kuna baadhi tayari wamefungua vituo Tanga, Mwanza, Iringa na wanaingiza kipato.

Kuhusu agizo la Makamu wa Rais, Dk Philip Mipango alilotoa katika siku ya kuadhimisha siku ya Kiswahili Julai 7, mwaka huu kwa kuwataka Bakita kuwaweka walimu wa lugha hiyo kwenye kanzidata, Vida amesema kazi hiyo bado inaendelea na mpaka sasa kuna walimu 1000 wameshawasajili katika mfumo huo.

Ametumia nafasi hiyo kuwasihi wanafunzi wanaomaliza mwaka huu waende kujiandikisha ofisini kwao au kujisajili walipo kwa kutumia mfumo wao uliopo mtandaoni.

Author: Gadi Solomon