Bakita yapongeza Ubalozi wa Marekani kuadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani

Summary: Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (Unesco) lilitangaza Julai 7 kila mwaka kuwa siku ya Kiswahili Duniani, mwaka huu ni mara ya pili maadhimisho hayo kufanyika duniani kote.

Gadi Solomon, Mwananchi

[email protected]

Dar es Salaam. Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) limeupongeza ubalozi wa Marekani nchini Tanzania kwa juhudi kuhamasisha matumizi ya Kiswahili duniani, huku wakifanya maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani kwa mara ya pili mwaka huu katika ofisi za ubalozi huo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika maadhimisho hayo ya siku ya Kiswahili yaliyofanyika leo Juni 27, 2023, Katibu Mtendaji wa BAKITA, Consolata Mushi amesema lugha ya Kiswahili imetandawaa zaidi duniani na hivi sasa wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili wamefikia  milioni 500.

“Serikali imefanya juhudi mbalimbali kuhakikisha tunawatumia diaspora katika kusaidia kufundisha Kiswahili duniani,” amesema Mushi ambaye pia ni mtaalamu wa lugha ya Kiswahili.

Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Robert Raines amesema Kiswahili sasa siyo tu lugha ya Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki bali imekuwa lugha ya dunia.

Amesema Marekani imekuwa ikiweka mkazo katika kujifunza lugha ya Kiswahili ili kuendana na mabadiliko ya utamaduni duniani.

Mkuu wa Utawala Ubalozi wa Marekani nchini,  Shan Kennedy ambaye pia ni mwanafunzi aliyejifunza Kiswahili, amesema zaidi ya Wamarekani 100,000 wanazungumza lugha ya Kiswahili katika nchi hiyo.

“Tangu lugha ya Kiswahili itangazwe kuwa lugha ya kimataifa, zaidi vyuo zaidi 100 vinafundisha lugha ya Kiswahili,” ameeleza.

Amesema katika vitu vingi ambavyo wanapenda kujifunza Kiswahili ni kutokana kuwa na semi nyingi ambazo zinawasaidia kufahamu stadi mbalimbali za maisha.

Amesema wapo Wamarekani wengine hapa nchini wanasoma Kiswahili kwa ajili ya kuwawezesha kushiriki miradi mbalimbali ya maendeleo.

Vilevile amesema kwamba sababu nyingine inayowafanya wapende kujifunza Kiswahili ni kuonyesha upendo kwa Watanzania na wafanyakazi wengine wanaofanya kazi katika ubalozi huo.

Akizungumza katika mdahalo huo, Joramu Mkumbi amesema Marekani ina mchango mkubwa katika kukuza Kiswahili duniani kutokana kutumika katika Nyanja mbalimbali za sanaa kama vile filamu na muziki.

Mwanafunzi nwingine wa Kiswahili wa Marekani kutoka Jimbo la Calfonia, Christa Andeson amewaacha washiriki wa kongamano wakiangua kicheko baada ya kueleza ugumu aliowahi kukutana na akitumia neno ‘choo’ badala ya kusema neno ‘chuo’.

Christa amesema mipango yake aliyoanza mwaka huu kwa kuanza kusoma Riwaya ya Vuta N’kuvute.

Washiriki wa mdahalo huo walikuwa ni Kituo cha Mafunzo cha MS TCDC Arusha, wafanyakazi, wanafunzi wa Kiswahili wa Ubalozi wa Marekani, Shirika la Wamarekani wa Kujitolea (Peace Corps).

Pia, maadhimisho hayo yaliwashirikisha wanaharakati wa lugha ya Kiswahili, Abdul Fumau ambaye ni mshairi chipukizi pamoja na Seko Shamte anayejishughulisha na kutayarisha filamu.

Author: Gadi Solomon