Bakita yawapa mbinu Watanzania kunogesha lugha

Gadi Solomon, Mwananchi

Dar es Salaam. Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) limewataka Watanzania kuongeza umahiri katika kutumia Kiswahili ili wajitofautishe na watu wanaojifunza lugha hiyo kwa kutumia vinogesho katika mazungumzo, uandishi wa vitabu, mawasilisho, hotuba na tafrija mbalimbali.

BAKITA imesema imeweka mkakati ili kuhakikisha Watanzania wanaacha kutumia lugha ya Kiswahili kwa mazoea na maneno yaleyale kila siku.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Kubidhaishaji Kiswahili kuanzia  mwaka 2021-2031, ikiwa ni pamoja na kusambaza msamiati mpya mara kwa mara.

Akizungumza wakati wa kikao cha kumpongeza mdau wa Kiswahili Joramu Nkumbi, Katibu Mtendaji wa BAKITA, Consolata Mushi amesema watumiaji wengi wa lugha ya Kiswahili wamekuwa wavivu kutumia msamiati mpya wa Kiswahili.

Pia amesema wameamua kumtambua na kumwalika Nkumbi kutokana na umahiri alioonyesha wa kutumia msamiati kwa namna ya kipekee.

“Kijana huyu amekuwa maarufu kwenye mitandao ya kijamii kwa namna anavyoitumia misamiati isiyozoeleka akitumia mbinu mbalimbali ili jamii ihamasike kuitumia,” amesema Katibu Mtendaji huyo ambaye ni mtaalamu wa lugha ya Kiswahili.

Ameongeza kuwa, “Watu wengi wanazungumza kama watoto wanavyojifunza, wamekuwa wavivu kutumia msamiati mpya.”

“Mtu anazungumza anashindwa kutumia methali, nahau, misemo ili kuipamba lugha yake. Hii ndiyo sababu inayowatofautisha kizazi cha sasa na watu kama kina Shaaban Robert, turudi kwenye lugha yetu ya Kiswahili kwa namna ilivyotumiwa na wazee wetu,” amesema Mushi.

Amesema ni wakati sasa kutumia semi mbalimbali kama misemo, nahau, methali na zinginezo ambazo zitamshawishi msikilizaji kuendelea kusikiliza hata kama amechoka.

Mdau wa Kiswahili, Nkumbi amesema amefanya utafiti katika jamii na kubaini kwamba vijana kuanzia miaka 1980 wamekuwa wakitumia Kiswahili kwa mazoea na kutozingatia ufundi wa lugha.

Amesema ukilinganisha na wazee wa zamani walikuwa wakizungumza lugha mufti (yenye kuvutia na maridadi).

Mdau wa Kiswahili, Joramu Nkumbi akijadili jambo na Ofisa Habari wa BAKITA, Jovina Bujulu.

Amesema ipo haja kwa sasa kuhamasisha jamii kuacha kutumia Kiswahili shelabela (shaghala baghala).

“Mimi ninatumia njia mbalimbali ya kuwafanya watu watumie lugha ya Kiswahili. Ninazungumza kwa kujiamini na kutumia misamiati migumu na kuitolea ufafanuzi katikati ya mazungumzo,” amesema Nkumbi ambaye ameandika vitabu vitano vya Kiswahili na kimoja kwa lugha ya Kiingereza.

“Ninapenda watu waachane kuzungumza Kiswahili rahisi kama watoto, waanze kutumia lugha ambayo ilitumiwa na wazee wetu kwa kuzingatia tamathali mbalimbali za semi, methali na misemo,” alifafanua Nkumbi ambaye kwa taaluma amesomea Shahada ya Sayansi katika Hisabati.

Licha ya melengo makubwa ya baraza hilo, pia limejipanga kuhakikisha Kiswahili kinatumika katika nyanja za kimataifa na kinaongezeka katika matumizi ya msamiati hapa nchini.

Miongoni mwa vijana wanaotajwa kutumia ufundi katika lugha ya Kiswahili ni msanii wa maigizo, Madebe Lidai maarufu kama Nabii Mswahili.

Author: Gadi Solomon