Bakita yawataka wakalimani kutumia Tehama kujitangaza

Gadi Solomon, Mwananchi

Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) limewataka wataalamu wa fani za Kiswahili nchini kutumia vyema Teknolojia ya Habarai na Mawasiliano kujitangaza taaluma zao na kuacha kuweka vitu visivyo na tija kwenye sehemu za kuweka taarifa mpya za kila wakati (status).
Bakita limetoa wito huo leo wakati wa kufunga mafunzo ya msasa ya kuwanoa wakalimani yaliyofanyika kwa wiki tatu katika Ukumbi wa Ukalimani wa baraza hilo Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kabla ya kuwatunuku vyeti vya kuhitimu, Katibu Mtendaji wa BAKITA, Consolota Mushi amesema baraza hilo litashirikiana na wakalimani waliopata mafunzo pindi zitakapotokea fursa za ukalimani kwa kuwapa kipaumbele lakini akiwataka kutumia kwa manufaa mitandao ya kijamii hususani kujitangaza taaluma zao.
“Siyo jambo baya kuweka picha zenu au ‘kumposti’ mtu lakini wapo wenzenu wamefanikiwa kwa kujitangaza kupitia sehemu hizo za kuweka picha na wamepata fedha za kujikimu kimaisha,” amesema Mushi.
Katibu huyo Mtendaji amesema wakalimani ambao wamepata mafunzo wamejengewa uwezo na kuweza kufanya ukalimani. Hivyo ni jukumu lao kuendelea kufanya mazoezi mara kwa mara.
“Hii ni azma ya kitaifa katika kutaka kuimarisha fani zote za Kiswahili hususani ukalimani. Hii ndio sababu serikali iliamua kununua vifaa vya ukalimani ili kuwezesha wakalimani mbalimbali kujifunza kwa vitendo,” amesisitiza Mushi.
Mkuu wa Sehemu ya Ukalimani na Tafsiri, Vida Mutasa amewapongeza wanafunzi wa ukalimani kujitokea kwa wingi ili kupata mafunzo hayo ya ukalimani.
Amesema mafunzo hayo ya wiki tatu yamekuwa na manufaa kwa sababu baada ya kuwapatia mafunzo hayo watahini wamejiridhisha kuwa yamewajenga na kuwa mahiri tofauti na walivyoanza.

Mwalimu wa Ukalimani wa Baraza hilo, Rajabu Kiswagala amesema ni muhimu wanafunzi waliohitimu mafunzo ya msasa kuendelea na mazoezi ya ukalimani mara kwa mara hata baada ya kuhitimu.
Amewataka wakalimani hao kuongeza ujuzi wa lugha za Kiarabu, Kiingereza ili waweze kuendana na mahitaji ya ukalimani katika Nyanja za kimataifa.
Mkalimani kutoka lugha ya Kiswahili kwenda Kiingereza, Mohamed Kambangwa amesema huu ndio wakati watumiaji wa lugha ya Kiswahili kujitokeza kuitumia lugha hiyo ili kuchangamkia fursa za Kiswahili duniani.
Amesema amenufaika na mafunzo hayo namna ya kutumia kizimba cha ukalimani jambo ambalo awali hakuwa anafahamu.
“Nimejifunza kutumia Kiswahili sanifu pamoja na nyenzo kama kamusi ya toleo jipya ya Baraza la Kiswahili,” amesema Kambangwa.
Mwanafunzi mwingine aliyehitimu mafunzo ya msasa, Ally Jambia ambaye anakalimani Kiarabu kwenda Kiswahili amesema amejifunza kutumia vifaa vya ukalimani na matumizi ya maneno ya Kiswahili kwa ufasaha kwenda lugha zingine.

Ametoa wito kwa watu wengine kuyatumia mafunzo ya BAKITA ili waweze kuwa bora zaidi miongoni mwa wakalimani wengi waliopo mtaani.
Mkalimani Halima Zakaria anasema amejifunza kwa vitendo zaidi kuliko na ilivyokuwa awali. Hivyo ameweza kutumia vifaa vya kisasa vinavyopatikana katika chumba cha ukalimani Bakita.
Mwanafunzi huyo anayefanya ukalimani wa Kiswahili Kifaransa na Kiswahili Kiingereza, amesema analishukuru Baraza la Kiswahili kuandaa mafunzo hayo ambayo yamemuwezesha kuwa mkalimali mahiri.

Author: Gadi Solomon