Baraza la Kiswahili la Taifa lawatunuku vyeti washereheshaji 50 Dar

Gadi Solomon na Pelagia Daniel, Mwanachi

Dar es Salaam. Baraza la Kiswahili la Taifa(BAKITA), limewatunu vyeti washereheshaji takribani 50 baada ya kupatiwa mafunzo ya siku tatu kwenye Ukumbi wa Utamaduni, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam jana.

Akizungumza wakati wa kuwatunuku vyeti vya mafunzo hayo ya siku tatu, Kaimu Katibu Mtendaji wa BAKITA, Consolata Mushi amesema washereheshaji ni kundi muhimu kwa sababu katika sherehe zao wanawahudumia watu zaidi ya 1,000 kwa wiki.
Alisema baraza litaendelea kupanua wigo ili mafunzo hayo yaweze kuwafikia washereheshaji wote nchi nzima.
“Bakita itaendelea kushirikiana na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) katika kuwadhibiti washereheshaji wasio na sifa wanaofanya kazi hizo,” amesema Kaimu Mtendaji huyo.

Aidha, Serikali imepongeza juhudi za ukuzaji na kueneza lugha ya Kiswahili kimataifa ikiwa ni pamoja na hatua ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco) kutenga Siku ya Kiswahili duniani.
Naibu Waziri wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Pauline Gekul amesema hayo Jumatano Novemba 24, 2021 na kusisitiza kwamba hatua hiyo ni muhimu pia matumizi ya Kiswahili yazingatie utamaduni husika.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya washereheshaji kuhusu matumizi ya Kiswahili sanifu yaliyofanyika Ukumbi wa Utamaduni katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, amesema ni sifa kubwa kwa taifa letu kutokana na Unesco kukitambua Kiswahili ambacho ni lugha ya kwanza Afrika kwa kuadhimishwa kila Julai 7.


Naibu Waziri Gekul amesema hayo ni mafanikio makubwa na matokeo ya jitihada za viongozi watangulizi, pamoja na Rais Samia Hassan Suluhu kwa juhudi zake kuhimiza matumizi ya lugha ya Kiswahili nchini na kimataifa.
Pia amesema tayari kuna mipango imeandaliwa kila kwenye ubalozi wa Tanzania, kuwepo na dawati la Kiswahili ambalo litaratibu na kuwasaidia wageni wanaotaka kujifunza Kiswahili kabla ya kuja nchini.


“Rais Samia amekuwa mstari wa mbele kukinadi Kiswahili, na kutafuta fursa za Kiswahili kila anapokwenda,” amesema Naibu Waziri Gekul.
Amesema Watanzania wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuzungumza Kiswahili kwani Unesco kama tayari wamekitambua, hivyo nao washereheshaji wanapaswa kukitumia bila uoga.
“Tusiogope kutumia lugha ya Kiswahili mbele ya wageni kwa sababu tunapokipa nafasi, tutapanua wigo kwa wakalimani kupata ajira,” alisema Naibu Waziri.
Mwenyekiti wa Chama cha Washereheshaji Tanzania, Steven Mwakajumba amesema ni wakati mwafaka sasa jamii kuwatumia washereheshaji ambao wamepatiwa mafunzo kutoka Bakita.
Amesema kutokana na mafunzo ambayo Bakita imeanza kuyatoa itawapa wigo wa kufanya kazi katika maeneo mbalimbali kutokana na kutambuliwa.
“ Mafunzo haya ya siku ya tatu, yametuwezesha kutambua istilahi na misamiati ya Kiswahili ambayo awali tulizoea kutumia maneno ya Kiingereza,” alisema Mwakajumba ambaye pia ni mshereheshaji mkongwe.

Author: Gadi Solomon