Baraza la Kiswahili lafungua mafunzo ya ukalimani awamu mpya

Gadi Solomon, Mwananchi

Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) limeendeleza utekelezaji wa mpango mkakati  wa miaka kumi wa ubidhaishaji lugha ya Kiswahili kwa kutoa mafunzo ya kuwapiga msasa wakalimani wenye sifa lakini wamekosa uzoefu wa kazi hiyo.

Akizungumza leo Jumatatu kwenye Ukumbi wa Ukalimali uliopo kwenye ofisi ya baraza hilo, Katibu Mtendaji wa Bakita, Consolata Mushi amesema serikali kupitia baraza hilo imeanza kuwanoa wakalimani wa Kiswahili kwenda lugha mbalimbali ikiwamo Kispaniola, Kireno, Kichina, Kifaransa, Kiingereza.

Mushi amesema baraza hilo limeamua kumtumia mwalimu mwenye uzoefu kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Petro Basil  ambaye amebobea kwenye lugha mbalimbali za kigeni ikiwamo Kifaransa.

” Kiswahili sasa ni lugha ya kimataifa na yeyote ambaye atapingana na hilo, sababu zipo wazi. Tumeona sasa inatumika katika nyanja mbalimbali hata vyombo vya kikanda  na Umoja wa Mataifa vinakitumia,” amesema Mushi ambaye ni mtaalamu wa lugha ya Kiswahili.

Amesema baraza limeweka mpango huo wa kuwanoa wakalimani kwa sababu wengi wao wamepata mafunzo ya ukalimani kwa nadharia.

Amesema ili kutatua changamoto hiyo, Serikali iliamua kununua vifaa vya ukalimani ili kuwawezesha kuwaandaa wakalimani kuingia kwenye ushindani katika maeneo mbalimbali wanakoenda kufanya kazi.

Katibu huyo Mtendaji amesisitiza kuwa ni muhimu wakalimani wazoefu kuwashika mkono wenzao wanaopatiwa mafunzo ili waweze kuwa na uzoefu pia ni vyema wapewe nafasi katika shughuli ambazo wanazifanya.

“Wapo baadhi ya wakalimani kutokana na kutokuwa na uzoefu wa matumizi ya vifaa vya ukalimani wanajikuta wanashindwa hata kuwasha na kuvitumia vifaa jambo ambalo serikali imelipatia ufumbuzi,” amesema Mushi.

Amesema kutokana na ushindani uliopo kimataifa, baraza litahakikisha linawanoa wakalimani wa lugha mbalimbali ili kuwa na watu wanaoweza kufanya kazi katika vyombo vya kikanda na kimataifa.

“Serikali inapowapa fursa kama hii, ni matarajio mtakapohitajika kutoa huduma katika maeneo mbalimbali, ninyi ndiyo mtatumika kwa kazi hiyo,” alisisitiza Mushi.

Katibu huyo mtendaji wa baraza ametoa wito kwa wakalimani waliopo mtaani kuwasiliana na baraza ili waweze kupatiwa mafunzo hayo kisha kuwasajili kwenye kanzi data yao. Pia, watapata fursa ya kupewa vyeti vya utambuzi wa kazi yao.

Mwalimu wa Ukalimani, Basil  amesema tangu aanze kutoa mafunzo ya msasa takribani wakalimani 600 wameshahitimu mafunzo hayo.

Amesema kwa kuwa wanafunzi hao wa ukalimani wameshaonyesha nia wataendelea kuwanoa huku wakitakiwa kujiamini kuwa wao ni wakalimani.

Mkuu wa Idara ya Ukalimani, wa Bakita, Vida Mutasa amesema mafunzo hayo ni endelevu baraza litaendelea kuwanoa wakalimani kila wakati kulingana na mahitaji.

Katika Mpango Mkakati wa Taifa wa Ubidhaishaji wa Kiswahili uliozinduliwa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani, Julai saba mwaka huu,  mojawapo ya malengo kwenye mkakati huo kuanzisha kanzidata ya wakalimani wa lugha Kiswahili kwenda lugha mbalimbali baada ya kuwapiga msasa.

Mwisho

Author: Gadi Solomon