Baraza la Kiswahili lahimiza kutumia istilahi za Kiswahili

Subira Kawaga, SwahiliHub

Dar es Salaam. Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita), Consolata Mushi amewataka Watanzania kutumia istilahi za Kiswahili zinazoandaliwa na baraza hilo.

Mushi aliyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza kwenye kipindi kinachorushwa na Channel Ten.

Alisema Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita), liliundwa kwa Sheria ya Bunge namba 27 kama chombo cha kusimamia ukuzaji na maendeleo ya lugha ya Kiswahili.

  “Jukumu kubwa la Bakita ni kusimamia vyema yale matumizi na maendeleo yake, ukuaji wake. Lugha inapigaje hatua nje ya mipaka yake,” alifafanua Mushi.

Alisema Kiswahili kimekua na kuendelea kwani hadi sasa ni miongoni mwa lugha kuu kumi ulimwenguni.

Miongoni mwa mafanikio ya baraza hilo ni kukuza msamiati na istilahi zake. Mfano uviko 19 (kiambukuzi, kivukizi, kitakasa).

Mushi alisema, “Kila istlahi hutumika katika uga maalumu, kwa mfano ukienda katika uga wa teknolojia (kompyuta) ukiambiawa maneno kama;-kipanya, kilambaza, maobonye, kicharazio.”

“Maneno hayo sio lazima uyakute katika uga mwingine. Ndio maana tunaposema, kiambukuzi/kipukusi wengine husema kitakasa, yote huhusika katika mazingira haya ya umviko-19.”

Katika jamii, maneno mbalimbali yanaibuka katika jamii na mengine ni kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Kaimu huyo mtendaji ambaye pia ni mtaalamu wa Kiswahili alisema, “Kwa mfano, baada ya janga hili la corona kuanza, yaliibuka maneno mengi, kama vile;-sanitizer baada ya kuyakusanya maneno hayo na kuyatafiti  kwamba yanahusu nini katika jamii, tulifanya jopo la usanifishaji wa maneno hayo na hatimaye tukatengeneza istlahi za Umviko-19 kama kazi ya Baraza.

“Natulitengeneza istlahi za  nyanja zote kuhusu uviko-19,kama vile za kimazingira,hali ya hewa pia tunakitabu cha Istilahi za nyanja zote (historia,baiolojia n.k).”

Hivyo alisisitiza kuwa isitokee mtu aseme nataka neno fulani la Kiswahili lakini sipati maana zake. Nawakati mwingine mtu husema hivyo kutokana na uvivu wa kusoma,kwani lugha hukua kila siku.

Pia, jukumu jingine, ni kutoa tafsiri rasmi. Nimoja ya huduma itolewayo katika Baraza hili, hivyo unapopata maandishi aidha kutoka lugha ya Kihispania au Kiingereza kwenda lugha ya Kiswahili, unapaswa kufika Bakita ili kupata mhuri unaothibitisha kwamba tafsiri hiyo ni rasmi.

Kuna kanuni na taratibu maalumu katika uhamishaji wa ujumbe kutoka lugha moja kwenda nyingine(tafsiri), hivyo ni vyema kupata tafsiri ya kisemantiki na sio sisisi (neno kwa neno) ili kuweza kueleweka vyema.

Baraza hilo lina kanzidata za wakalimani wa lugha zote kwa sababu wanaweza kukalimani. Pia lina vyombo vya ukalimani ili kuweza kumudu kufanya ukalimani.

Vilevile inajukumu la kushughulikia usawazisho wa matumizi ya Kiswahili katika nchi za Afrika Mashariki.

Author: Gadi Solomon