Bora nimpe mama

Najaribu ku’dekeza,
Japo niwekwe moyoni,
Nakupa nisivyoweza,
Bado huna shukurani,
Huwezi hata kwigiza,
Kudhibiti kisirani,
Jama jama nimekoma,
Kumjali hayawani,
Ni heri nimpe mama,
Kidogo akithamini.

Huishi jibaraguza,
Nikupe za benkini,
Hukauki Ki’ngereza,
“Ai lavi yuu hani,”
Pesa ukizimaliza,
Huoni yangu thamani,
Jama jama nimekoma,
Kumjali hayawani,
Ni heri nimpe mama,
Kidogo akithamini.

Yani nikikupa laki,
Unataka milioni,
Hapo utanidhihaki,
Na matusi ya nguoni,
“Huwezi kunimiliki,
Heri nende kwa fulani,”
Jama jama nimekoma,
Kumjali hayawani,
Ni heri nimpe mama,
Kidogo akithamini.

Mama’ngu hataki laki,
Sikwambii milioni,
Baraka hadi zabaki,
Nikimpa ishirini,
Dua zinatamalaki,
“Uishi vyema mjini”,
Jama jama nimekoma,
Kumjali hayawani,
Ni heri nimpe mama,
Kidogo akithamini.

Author: Gadi Solomon