
Kuelekea maadhimisho ya siku ya Kiswahili duniani (Masikidu) ambayo kilele chake ni Julai 7 2023, na kitaifa yataadhimishwa Zanzibar, kwa kuwajumuisha wadau mbalimbali wa Kiswahili. Katika kusherehekea siku hii adhimu, ni muhimu kutambua vipo vyombo ambavyo vimechangia pakubwa kukua na kuenea kwa lugha ya Kiswahili.
Miongoni mwa vyombo hivyo ni “Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”. Bunge la Tanzania ni chombo cha uwakilishi wa wananchi, hii ni kwa mujibu wa ibara ya 62 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977), kwani haiwezekani wananchi wote kukusanyika mahali pamoja na kufanya maamuzi muhimu katika uendeshaji wa nchi hivyo, uwakilishi unapaswa kuwepo.
Wabunge wanapokuwa bungeni hutekeleza majukumu yao kwa niaba ya wananchi. Bunge katika utekelezaji wa majukumu yake huongozwa na “Kanuni za Kudumu za Bunge” ambao ni mwongozo wa shughuli zote za bunge. Mwongozo huu unabainisha wazi Kiswahili kitatumika katika shughuli za uendeshaji wa Bunge sambamba na Kiingereza, kwa kurejelea kanuni ya 168 (1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge:Toleo la 2020.“Shughuli za Bunge zitaendeshwa katika lugha ya Kiswahili au Kiingereza, bila tafsiri ya lugha hizo kutolewa.
”Kanuni za kudumu za Bunge hujumuisha masuala anuwai ikiwemo: Uendeshaji wa shughuli za kila siku za bunge, utaratibu wa uchaguzi wa viongozi wa Bunge, utaratibu wa mikutano na vikao vya Bunge.
Matumizi ya Kiswahili yanajidhihirisha kupitia maeneo yafuatayo bungeni:Kiswahili kutumika katika Taarifa rasmi za Bunge (Hansard), hizi ni taarifa rasmi za majadiliano yote ya mikutano ya bunge au vikao vya kamati ambapo inahusisha uwekaji wa kumbukumbu wa neno kwa neno (verbatim) wa kila kinachosemwa na kufanyika ndani ya bunge au kwenye kamati za bunge. Hansard hutekelezwa kupitia kanuni za kudumu za bunge, katika kanuni ya 169 (1), (2), (3): 2020.
Kanuni zinaelekeza Hansard kuandikwa katika lugha iliyotumiwa na msemaji na yakiwa ni maneno halisi aliyoyatamka, pia atapewa nakala ya alichozungumza ili asahihishe makosa ya kiuchapaji sio kubadili maana halisi ya maneno aliyoyatamka bungeni. Hansard hutolewa kwa mfumo wa maandishi kwa nakala ngumu na laini zote kwa lugha ya Kiswahili ikiwa lugha rasmi ya matumizi bungeni.
Matumizi ya Kiswahili kwenye mikutano na vikao vya Bunge. Uendeshaji wa mikutano na vikao vya Bunge umeanishwa wazi kupitia kanuni za kudumu za Bunge kuanzia kanuni ya 28 (1). Mikutano na vikao huendeshwa kwa Kiswahili ikiwa ni lugha rasmi ya matumizi bungeni, suala hili limeendelea kukipa thamani Kiswahili, kwa kutumika katika muktadha wenye dhamana ya kutunga sheria za nchi na kuishauri serikali kwenye utekelezaji wa majukumu yake.
Mchango huu unaofanywa na Bunge, unapaswa kuigwa na vyombo vingine ndani na nje ya Serikali hii itaendelea kukipa thamani Kiswahili na kukikuza. Mamlaka za Kiswahili zihakikishe zinatoa ushirikiano mujarabu pindi unapohitajika na kuhakikisha kuna utumizi wa lugha sanifu na fasaha, pasiwe na Kiswahili kibovu ndani ya vyombo hivi kutokana na umahususi wake kwa taifa.
Maoni Mapya