CHAPASI MRUMBA


Siipotezi risasi, kwa ndovu ama kwa simba,
Nikimlenga sikosi, huisha wao umwamba,
Hupinduka sarakasi, mauti yesha wakumba,
Ndimi chapasi mrumba, korofindo si pepesi.

Jicho moja nikifumba, korofindo si pepesi,
Nyati hawezi kutamba, kidole changu chepesi,
Awapo nitamtimba, haimkosi risasi
Korofindo si pepesi, ndimi chapasi mrumba.

Wajua yangu nemsi, uzani wenu wajomba,
Walio wakinitusi, zama zile za ugumba,
Wao walikula nyasi, nyama kwangu ilitamba,
Ndimi chapasi mrumba, korofindo si pepesi.

Hayano ninayo amba, mbishi aseme basi,
Maozi pasi kufumba, nimuondoshe ubishi,
Nikitungue kilemba, pasipo kugusa rasi,
Ndimi chapasi mrumba, korofindo si pepesi,

Nachunga wangu unasi, simi mgonga usumba,
Kinyama chenye mkosi, shaba sitaki kiramba,
Shabaha na yangu kasi, si hangaiki na Komba.
Ndimi chapasi mrumba, korofindo si pepesi.

Kipite kwa kujikomba, wala bunduki sigusi,
Si wazi kwake kutamba, niseme kina ni ghasi,
Afyaye isha mgomba, kitenda liwa na fisi,
Korofindo sipepesi, ndimi chapasi mrumba.

Si mrumba wasiwasi, msitu kwangu ja nyumba,
Nikishindia nuhasi, pori lote ninatamba,
Hazinivuki kugesi, nikimbie ja manamba,
Ndimi chapasi mrumba, korofindo si pepesi

Tama nasega lebasi, ya Mungu si ya Mkumba,
Akili kama fanusi, ikizima umeyumba,
Katu si yangu ramisi, visonona kuperemba,
Ndimi chapasi mrumba, korofindo si pepesi.
MKANYAJI
HAMIS A.S. KISAMVU
0715311590
kissamvujr@gmail.com
Baitu shi’ri- Mabibo
Dar es salaam – Tanzania
20-Nov-2022

Author: Gadi Solomon