Congo kuingia EAC kutaongeza matumizi ya Kiswahili duniani

Gadi Solomon

Unakumbuka ile dhana Kiswahili  asili yake ni Kikongo? Hivi karibuni wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wameidhinisha kuingizwa kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika umoja huo.

Kwa sasa Kiingereza na Kiswahili ndizo lugha rasmi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, ingawa kumekuwa na mazungumzo kuhusu kuanzisha Kifaransa, ambacho kinazungumzwa nchini Rwanda na Burundi.

Lugha rasmi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni Kiswahili, Kifaransa, Kilingala, Kituba (Kikongo) na Tshiluba. Wataalamu wanasema asili ya lugha nyingi katika eneo hili inapaswa kuangaliwa kama fursa na sio kizuizi.

Wasanii wengi wa Congo tumeona wakiishi Ufaransa au nchi zinazozungumza lugha hiyo. Kwa namna  nyingine lugha ya Kiswahili itaendelea kusambaa barani Ulaya.

Kumekuwa na msukumo wa kukuza matumizi makubwa ya Kiswahili, hasa baada ya Umoja wa Afrika kukipitisha kama lugha rasmi ya kazi mwezi Februari 2022. Hata hivyo, baadhi ya mikoa kama vile Magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na sehemu za mataifa mengine ya EAC haizungumzi Kiswahili. Lakini kutokana na mwingiliano baina ya nchi zinazozungumza lugha ya Kiswahili kutaleta athari chanya ya uenezaji wa lugha hiyo.

Kusonga mbele katika ukuaji wa Kiswahili, tunatarajia EAC ambayo ni ya lugha nyingi, ambayo inaweza kusababisha mwingiliano zaidi kati ya raia wa EAC na nchi zinazozungumza lugha ya Kifaransa katika Afrika ya Kati.

Pengine ni wakati muafaka wa  kuondoka kutoka katika lugha ya mkoloni. Afrika inapaswa kuwa na kitu ambacho ni chetu na kwa ajili yetu. Historia na ukuaji wa Kiswahili katika kitovu chake, Kiswahili na lahaja zake huenea kutoka sehemu za Somalia hadi Msumbiji na kuvuka hadi sehemu za magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Umbali huo ungeweza kuonekana kama kipimo cha kuenea kwa lugha na mvuto wake unaokua.

Baada ya Shirika la Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco) kuteua tarehe 7 Julai kuwa siku ya lugha hiyo duniani, imeongeza hamasa dunia kujifunza lugha hii adhimu. Kiswahili, ambacho kinachukua takriban  asilimia 40 ya msamiati wake moja kwa moja kutoka Kiarabu, awali kilienezwa na wafanyabiashara wa Kiarabu katika pwani ya Afrika Mashariki.

Kisha ilirasimishwa chini ya tawala za kikoloni za Wajerumani na Waingereza katika eneo hilo mwishoni mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa Karne ya 20, kama lugha ya utawala na elimu.

Na ingawa imezungumzwa hapo awali kama njia mbadala katika bara la Afrika, Kiingereza, Kifaransa au Kireno kama lingua franca, au kama lugha inayoeleweka na watu wengi, sasa kuna msukumo mpya.

Katika mkutano  wa hivi karibuni wa wakuu wa nchi, Umoja wa Afrika (AU), ulipitisha Kiswahili kama lugha rasmi ya kazi.

Pia ni lugha rasmi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambayo DR Congo tayari imejiunga.

Mnamo 2019, Kiswahili kilikua lugha pekee ya Kiafrika kutambuliwa na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

Muda mfupi baadaye, ilianzishwa katika madarasa kote Afrika Kusini na Botswana.

Pia hivi karibuni, Chuo Kikuu cha Addis Ababa cha Ethiopia kilitangaza kuanza kufundisha Kiswahili. Baadhi ya wanaisimu wanatabiri kwamba ufikiaji wa Kiswahili barani Afrika utaendelea kupanuka. Hii ni kutokana na uongezekaji wa watumiaji wa lugha hiyo.

Wazo la Kiswahili kuwa lugha ya Afrika nzima lilisukumwa miaka ya 1960 na Rais wa Kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere, ambaye alitumia Kiswahili kuunganisha taifa hili baada ya uhuru.

Afrika Mashariki  iwapo itaongeza  juhudi zaidi kukuza ujifunzaji wa Kiswahili katika maeneo mengine, tunaweza kufikia haraka mawazo ya Nyerere Kiswahili kuwa lugha ya bara zima.Kuna umuhimu pia wa kukipa nguvu Kiswahili kwa kuwa na wataalamu tunao wa kutosha.

Changamoto iliyopo katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Kiswahili kinazungumzwa katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo tu. Tofauti na nchi nyingine zinazounda umoja wa EAC.

Kwa hivyo upo umuhimu kwa Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuweka msukumo baraza la Kiswahili lianzishwe hara kchini humo ili kuleta usawazishi wa matamshi kwa Wakongo na kuwasaidia kupata majarida na machapisho ambayo yanatumiwa na watangalizi wao kwenye Jumuiya kama vile kamusi za Kiswahili.

Mwandishi anapatikana kwa namba 0712127912

Author: Gadi Solomon