Gazeti la Mwananchi lapata tuzo matumizi ya Kiswahili sanifu

Gadi Solomon, Swahili Hub

Dodoma. Gazeti la Mwananchi limetunukiwa Tuzo ya gazeti bora linalotumia lugha ya Kiswahili kwa usanifu na ufasaha nchini Tanzania kwa vyombo vya habari binafsi.

Tuzo hiyo imetolewa leo Jumatano Januari 20, 2021 na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Tabia Maulid Mwita na kupokewa na Mwakilishi wa Gazeti hilo mkoani Dodoma.

Gazeti la Mwananchi linachapishwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) inayochapisha pia magezeti ya The Citizen, Mwanaspoti.

Gazeti hilo ndilo gazeti pekee kwa makampuni binafsi lililopata tuzo hiyo, magazeti mengine yaliyopata tuzo ni ya Serikali, Habari Leo na Zanzibar Leo.

Pia, upande wa vyombo vya televisheni waliopata tuzo ni TBC, ITV na Channel Ten na kwa upande wa redio ni Radio One, Kiss FM, Wapo Radio, BBC Swahili na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa.

Akizungumzia utoaji wa tuzo hizo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdallah amewapongeza washindi na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kukienzi Kiswahili.

Amesema Watanzania wanapaswa kujisikia fahari kutumia lugha ya Kiswahili kutokana na kushika kasi katika matumizi ndani na nje ya Tanzania jambo ambalo limeifanya lugha hiyo kuwa bidhaa.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa MCL, Noor Shija amesema wameipokea tuzo huku wakitambua jukumu kubwa lililopo mbele yao ya kuimarisha Kiswahili kupitia gazeti la Mwananchi na mitandao ya kampuni hiyo.

 “Tunashukuru kwa wadau wa Kiswahili kutambua mchango wa gazeti letu katika kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya Tanzania,” amesema Shija.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere, Ahmed Sovu akizungumzia tuzo ya Mwananchi amelishukuru  kwa kutoa habari zilizomsaidia kwenye utafiti wake.

Amesema alipokuwa akisoma shahada ya uzamivu gazeti la Mwananchi lilikuwa msaada kwake kwa kuwa alilitumia kwenye tafiti alizokuwa akizifanya.

“Nawapongeza Mwananchi kwa kuthamini Kiswahili, na kutenga kurasa maalumu kwa ajili ya kuzungumzia masuala ya Kiswahili,” amesema Sovu ambaye pia ni mshititi wa lugha ya Kiswahili.

Mshairi maarufu wa Kiswahili, Ngatuma Ngatuma amesema gazeti la Mwananchi limeendelea kuwa bora kwa sababu limekuwa likigusa masuala muhimu yanayohusu jamii ya Watanzania.

Author: Gadi Solomon