CHANZO NI WEWE

Mwandishi, Ismaily Himu

Chanzo ni wewe ni tamthiliya inayozungumzia athari za watoto wa mitaani na changamoto zinazowakumba hasa katika nchi zinazoendelea. Mtunzi ameonesha jinsi jamii nzima inavyohusika kwa namna moja au nyingine kuongezeka kwa watoto hawa pamoja na namna ya kutatua tatizo hili, lengo likiwa ni kuifanya jamii nzima iwajibike katika hili. Tatizo la watoto wa mitaaani limekuwa ni tatizo la kidunia, limekuwa ni tatizo kubwa hasa katika nchi zinazoendelea hasa za bara la Afrika na Asia ambako jamii kubwa ni masikini. Tatizo hili haliwezi kutatuliwa na mtu mmoja mmoja au kikundi fulani cha watu bali kwa jamii nzima kujumuika na kuona kuwa kuna haja ya kutatua tatizo hili.

ALFAJIRI

Sijali na baba Baraka wanarudi kutoka kazini Sijali anamshawishi Baba Baraka wakanywe pombe.

BABA BARAKA:    Vipi rafiki yangu ule mpango wako wa kujenga 

nyumba umeishia wapi? Jitahidi uanze kujenga  

                                    mapema rafiki yangu kwani hela ni maua leo 

                            yamechanua kesho yamenyauka. (Anaongea huku anabonyeza bonyeza simu yake ya mkononi)

SIJALI:                      Hela zipo tu bwana, ngoja nifanye kwanza matumizi baa.

BABA BARAKA:    Ufanye matumizi? (Anakodoa macho na kusikitika)

SIJALI:                      Unashangaa nini, lazima niweke heshima baa!

                                    Lazima watu wajue mimi ni nani hapa mtaani…

BABA BARAKA:    Heshima haitafutwi baa ndugu yangu wewe jenga nyumba nzuri watu watakuheshimu tu, na pia lazima tufanye maandalizi mapema maana hizi nyumba za kupanga zinatupumbaza.

SIJALI:                      Mimi najipanga sitaki kujenga kibanda, nataka nikianza kujenga nijenge kasri kweli kweli!

BABA BARAKA:    Haya bwana, ngoja ngoja huumiza matumbo…

SIJALI:                      Pia usisahau kuwa haraka haraka haina Baraka…

                                    (Wote wanacheka, hahaaaaaaa)

SIJALI:                      Tupitie kidogo hapa baa uone wanaume wanavyojua kutumia hela zao! Ni nyama choma na bia, si unaniona nilivyonawiri!

BABA BARAKA:    Acha masihara yako bwana, uliona wapi pombe ikamfanya mtu anawiri! Mimi sioni faida yake na katu sitojaribu.

SIJALI:                      Ngoja nikupe faida ya baa, moja nirahisi kupata wasichana warembo, mbili inatusaidia kupunguza msongo wa mawazo, tatu inatukutanisha na marafiki wapya kila kukicha nne.

BABA BARAKA:    Tena ishia hapo hapo, mimi nimeoa hao wasichana wanisaidie nini katika maisha yangu zaidi ya magonjwa! Na aliyekwambia pombe inapunguza msongo wa mawazo ni nani? Hizo dhana potofu, mimi siendi huko kabisa.

SIJALI:                      Hapa hatugombani tunaeleweshana tu (Anamshika mabega na kumtuliza)

BABA BARAKA:     Tunaeleweshana au tunapotoshana! Mimi ninamuheshimu sana mke wangu kama ni hivyo basi hiyo baa inawafaa nyie makapera sio watu wenye familia na majukumu kama mimi.

SIJALI:                      Kweli bado uko usingizini ndugu yangu mwanaume gani usiyetumia pombe! Yaani Unashindwa hata na wasichana!

BABA BARAKA:    Naomba tuheshimiane bwana! Mimi sio mtoto, unanilaghai nishiriki kwenye mambo ya kipuuzi kama haya, tena kama umekosa mada za kuongea ni bora unyamaze.

SIJALI:                      Haya bwana ngoja mimi nikaonyeshe umwamba wangu. Tutaonana kesho kazini. (Anacheka na kuondoka)

BABABARAKA:     Haya, lakini tambua kuwa pombe sio nzuri rafiki yangu itakuumbua, wewe cheka tu. (Baba Baraka  anaagana na Sijali na kuwahi kurudi nyumbani na zawadi mkononi kama kawaida yake.

BABA BARAKA:   Ngo! Ngo! Ngoo… Hodiii! Nifungulie mlango

                                    mke wangu.

MAMA BARAKA: Ooooh! Karibu! Karibu mume wangu lete mzigo nikupokee…

BABA BARAKA:    Habari za hapa?

MAMA BARAKA:  Nzuri, pole sana mume wangu.

BABA BARAKA:   Aaaah! Usijali nimeshapoa… Vipi mbona

                                    pamepooza sana hawa watoto wako wapi niwape zawadi zao?

MAMA BARAKA: Ndio wamerudi toka shule muda huu! Subiri

niwaite, Aishaa! Barakaa! Tojoo! Njoeni mnaitwa naBaba   yenu (Aisha na Tojo walikuja mbio mpaka mapajani mwa Baba yao na walisalimia kwapamoja) “Shikamoo Baba”

BABA BARAKA:    Marahaba, hamjambo?  (Aisha na Tojo wanaitika tena wote kwa pamoja) “Hatujambo”

BABA BARAKA:    Baraka yuko wapi?

AISHA:                      Amemsindikiza rafiki yake kwao…

BABA BARAKA:    Mimi nilisema usiku ukishaingia ni marufuku mtoto yeyote kutoka humu ndani au mpaka nitumie viboko ndio mtanielewa enhee!   

TOJO:                        Mimi nilimwambia Baba hapendi utembee usiku akasema hafiki mbali.

BABA BARAKA:    Haya basi inatosha, nimewaletea viatu lakini niambieni kwanza leo mmefundishwa nini   shuleni?

TOJO:                        Sisi leo tumejifunza Hisabati, Kiingereza, na Kiswahili…

AISHA:                      Sisi tumefundishwa Kemia, Baiolojia, na Kiingereza.

BABA BARAKA:    Mitihani iliyopita hamkufanya vizuri sana ila leo nawaahidi atakayeshika nafasi ya kwanza, ya pili au ya tatu katika mitihani ijayo nitampa zawadii nzuri sana.

TOJO:                        Zawadi gani hiyo?

BABA BARAKA:    Aaah! ni siri yangu ila mtaifurahia sana…          

                                (Ghafla anaingia Mama Baraka huku jasho  

                                 jembamba likimtiririka)  

MAMA BARAKA:   Mume wangu, maji ya kuoga tayari na chakula pia tayari, chagua mwenyewe utaanza na kipi?

BABA BARAKA:    Mimi nashauri tule kwanza kwa sababu njaa inaniuma sana, kula lazima, kuoga hiyari au umesahau huu msemo mke wangu? (Wote wanacheka na kuelekea mezani) 

Asubuhi imeingia, anga bado ni nyeupe pee.  Sijali anampitia Baba Baraka na kuelekea kazini kwao, wakiwa njiani Sijali anagundua njia nyingine ya kumshawishi Baba Baraka anywe pombe.

SIJALI:                      Rafiki yangu, kuna jambo naomba msaada wako

BABA BARAKA:    Jambo gani hilo?

SIJALI:                      Jioni kuna wageni watanitembelea, ni mpenzi wangu anaitwa Malungo ila amesema hataweza kuja mwenyewe atakuja na rafiki zake

BABA BARAKA:    Sasa mimi nikusaidie nini?

SIJALI:                      Subiri bado sijamaliza, sasa mimi naomba tujumuike kwa pamoja kwenye chakula chajioni pale ‘SAVANA HOTEL’

BABA BARAKA:    Mmmh, huko hakuna vilevi! si unajua mimi situmii pombe?

SIJALI:                      Haa! Haa! haaaa! (Anacheka kwa kejeli) Ile ni hoteli tu na sio baa, na hata kama wewe hautatumia pombekutakuwa na vinywaji vingine vingi tu kama maji, juisi na soda ushindwe wewe tu.

BABA BARAKA:    Sawa kama ni hivyo tu ondoa shaka ndugu yangu, nitakuunga mkono usijali.

Wanafika kazini na kuanza kufanya kazi kama kawaida yao na jioni ilipofika Sijali na Baba Baraka waliondoka na kupitia ‘SAVANA HOTEL’ kama walivyopanga; na Malungo na rafiki zake pia walikuwa wameshafikawamekaa kwenye viti virefu vya baa huku wakiagiza vinywaji mbalimbali.

SIJALI:                      Jamani karibuni sana, kabla ya yote napenda kutumia fursa hii ya pekeekumtambulisharafiki yangu kwenu (Wote wanatega masikio yao kusikiliza vizuri) huyu hapa ni Baba Baraka, ni mfanyakazi mwenzangu huwa popote utakapomkutahuyu bwana na mimi nipo, popote utakaponikuta mimi na huyu bwana hutomkosa (Wote wanacheka)

(Malungo na rafiki zake wanashukuru kwa pamoja) “Tunafurahi kumfahamu” (Sijali anaendelea kuwatambulisha Malungo na rafiki zake kwa baba Baraka)

SIJALI:                      Na huyu hapa ni Malungo kipenzi changu, yule pale ni Tina pembeni yake ni Kurusumu wote ni rafiki wa Malungo.

BABA BARAKA:    Nimefurahi sana kuwafahamu (Wananyanyuka

                                    na kupeana mikono wakiwa wenye nyuso za

                                    furaha)

SIJALI:                      Jamani karibuni sana… Agizeni chochote

                                    mnachohitaji

BABA BARAKA:    Una hela? (Anamtania na kucheka)

SIJALI:                      Hapa ndio Benki ya Taifa, kuhusu hilo ondoeni shaka kabisa tena mkiweza bebeni mpeleke nyumbani kwenu (Kwa mzaha)

MALUNGO:             Hee heee heeee, halooo! Hawa ndio wanaume wa shoka sio wababaishaji (Malungo na rafiki zake wanaagiza pombe kali za aina mbalimbali na baba Baraka anaagiza juisi ya embe huku akionekana mwenye aibu tele)

SIJALI:                      Muhudumuu! Lete kilo ya nyama choma iliyokauka vizuri.

MALUNGO:             Samahani Sijali! naomba tuongee pembeni kidogo

KURUSUMU:           Mmmh! yaani mmeshaanza kuitana pembeni!

MALUNGO:             Aah kawaida tu jamani mniwie radhi.

                                (Wanashikana mikono na kusogea pembeni)

TINA:                         Usijali shoga, utamuweza huyu Kurusumu? Huwa haishiwi maneno (Malungo na Sijali wanasogea pembeni kidogo na kuanza kuongea)

MALUNGO:             Vipi mbona huyu rafiki yako ananiaibisha, yaani mtu mkubwa vile anywe juisi ya Embe! Au ndio umeamua uniletee vioja (Wananong’onezana taratibu)

SIJALI:                      Yule ni kweli hatumii pombe ila uwepo wenu hapa leo mnaweza mkamshawishi anywe hata kidogo, najua mwanamke ni shujaa hashindwi na kitu (Wanarudi mezani na kujumuika na wenzao, baada ya saa mbili kupita wote wanaanza kumshambulia Baba Baraka kama nyuki)

MALUNGO:             Vipi shemeji mbona sikuelewi! Yaani sisi wasichana tunakunywa pombe wewe mwanaume unakunywa juisi, au una matatizo?

BABA BARAKA:    Mimi huwa situmii kilevi cha aina yeyote na hata Sijali analitambua hilo.

KURUSUMU:           Heee unanishangaza!

MALUNGO:             Au upo kwenye dozi?

BABA BARAKA:    Hapana shemeji, huo ni msimamo wangu nimejiwekea katika maisha.

TINA:                         Msimamo? Hee makubwa!

SIJALI:                      Acha misimamo ya ajabu… hii sio sumu bwana kunywa hata nusu tu ili tuwe sawa, teremshia na nyama choma.

MALUNGO:             Juisi wanakunywa watoto wa shule…

SIJALI:                      Mwanaume lazima uwe ngangari. (Wote wanamshambulia kwa maneno na kumshangaa, ananyanyua chupa na kuipeleka mdomoni kwa woga huku akiwa amekunja sura)

BABA BARAKA:     Mmmh! Chungu sana! Mnapata raha gani kunywa vitu vichungu hivi? (Anakunja sura zaidi na kutema pembeni)

TINA:                         Taratibu tu utazoea na utainywa kama maji…

BABA BARAKA:    Hapana, haizoeleki hii (Anaendelea kunywa mpaka anaanza kulewa)

KURUSUMU:           Kweli Malungo umepata mume anayejua matumizi, usimwache huyu.

MALUNGO:             Huyu ni wa kufa na kuzikana… wenye wivu

                                    wajinyonge!

(Wote wanaitikia) Wenye vivu wajinyongeeee

(Baada ya saa tatu kupita Baba Baraka amekwishalewa na kuanza kulia kama mtoto mdogo)

BABA BARAKA:    Jamani nipelekeni nyumbani eee… namtaka mke wangu ooooooh! Ghooo!  Khaaaa!

                                    (Anatapika na kujilaza chini)

SIJALI:                      Tulia wewe unatutia aibu… ona watu wote wanatuangalia sisi, jikaze bwana.

BABA BARAKA:    Toka tokaa! Kwanini mnataka kuniua? Nyie watu wabaya sana.

MALUNGO:             Utauliwa na nani wewe… utajiua mwenyewe na hizo pombe zako.

KURUSUMU:           Mpelekeni kwake asituharibie starehe zetu…

TINA:                         Mmmh! Pombe kidogo tu mtu kalewa kama amekunywa pipa zima!

MALUNGO:             Jamani watu kama hawa msije nao sehemu kama hizi siku nyingine.

SIJALI:                      Lakini atazoea tu.

TINA:                         Ni kweli lakini hapa sio sehemu ya kujifunzia, akajifunzie huko huko vichochoroni.

MALUNGO:             Kweli kabisa mafunzo vichochoroni hapa ni starehe tu sio kubebana kama watoto.

SIJALI:                      Jamani tutaonana siku nyingine mimi nampeleka kwake asije akazidiwa hapa… (Anaaga na kushikana na Baba Baraka wakijikongoja kurudi nyumbani.)

                                    (Wakiwa nyumbani kwa Baba Baraka…)

BABA BARAKA:    Tuko wapi hapaa?

SIJALI:                      Hapa tumefika kwako, bisha hodi ufunguliwe mlango, mimi naondoka kwani shemeji akinikuta hapa itakuwa balaa (Sijali anaondoka huku akiyumba yumba na  

                                    kumwacha Baba Baraka mlangoni)

BABA BARAKA:    Haya wewe nenda tutaonana kesho. (Anatema mate pembeni)

SIJALI:                      Bisha hodi usije ukalala nje. (Anamsisitiza huku akizidi kutokomea gizani)

BABA BARAKA:    Mke wangu nifungulie mlango… fungua mlango wewe mwanamke (Anaongea huku akiwa ameegemea mlango, mkewe anafungua mlango na wote wakaanguka chini)

MAMA BARAKA:  Umekumbwa na masahibu gani mume wangu… jikaze ukae!

BABA BARAKA:    Ghoooo! Ghaaaa!  Niachee (Anaanza kutapika

                                    pombe alizokunywa)

MAMA BARAKA:   Mume wangu haya ni matapishi ya pombe… umeanza lini tabia ya kunywa pombe?

BABA BARAKA:    Nipe chakula usiniulize maswali kama bwana jela.

MAMA BARAKA:  Hembu ona ulivyojitapikia… huyu Sijali atakuwa amempa pombe mume wangu na asubuhi akija hapa atanikoma (Mama Baraka anamvua viatu na kumbadilisha nguo mumewe na kumbeba mpaka kitandani. Asubuhi na mapema Sijali anampitia Baba Baraka kama kwaida yao ili waende kazini, anamkuta Mama Baraka nje anafagia uwanja akiwa amefura kama puto.

SIJALI:                      Shemeji habari za asubuhi?

MAMA BARAKA:  (Kimya kidogo) Sina shida na hiyo salamu yakokama salamu ni mali ichukuwe mwenyewe. (Anaendelea kufagia uwanja)

SIJALI:                      Kwani vipi shemeji! Kuna tatizo gani?

MAMA BARAKA:  Wewe jana usiku ulimpa nini mume wangu? Kama ni hizo pombe zako kunywa mwenyewesio mpaka uniharibie familia yangu.

SIJALI:                      Mumeo sio mtoto, anajua baya na zuri mimisijamshauri anywe pombe ni akili yake

                                    mwenyewe naomba tusivunjiane heshima shemeji.

MAMA BARAKA: Heshima umeivunja wewe na sio mimi, looh! huna hata haya (ghafla baba Baraka anatoka na kukuta mtafaruku unaendelea)

BABA BARAKA:   Habari yako Sijali, vipi mbona nasikia kelele 

                                    kuna nini tena?

SIJALI:                      Hakuna tatizo, tunawekana sawa tu na shemeji hapa.

BABA BARAKA:    “Ok” sawa! naona umewahi kama kawaida yako.

SIJALI:                      Kweli si unajua foleni za magari siku hizi? Bila kuwahi tutakuwa tunashinda njiani tu.

BABA BARAKA:   Kwaheri mke wangu…

MAMA BARAKA: Sawa ila nakuomba uachane na hizo pombe mume wangu. (Amekunja uso huku akiwa ameshika kiono)

BABA BARAKA:    Usijali mke wangu.

Baba Baraka na Sijali wanaondoka huku wakiwa wameongozana kama mapacha kuelekea kazini wakiwa hoi kwa pombe za usiku. Wakiwa njiani wanajadiliana jinsi ya kuondoa uchovu.

SIJALI:                      Unajua mimi pombe bado zipo kichwani… naona kichwa kizito sana sijui leo huko kazini itakuwaje

BABA BARAKA:    Hata mimi ila najikaza kiume tu, yaani utadhani usiku nilibebeshwa magunia ya misumari kichwani.

SIJALI:                      Sasa unajua dawa yake ni nini?

BABA BARAKA:    Hapana… ni nini?

SIJALI:                      Dawa ya moto ni moto na sio maji….

BABA BARAKA:    Unamaana gani?

SIJALI:                      Lazima tukazimue… inatakiwa tupate hata chupa moja moja ili vichwa na akili zetu zirudi sawa, na hii ndio sheria ya pombe.

BABA BARAKA:    Hee! Wewe una wazimu, yaani kichwa bado kina pombe halafu tuongeze tena pombe?

SIJALI:                      Hiyo ndio sheria ya pombe rafiki yangu… lazima tuzimue lasivyo tukifika kazini hatutaweza kufanya kazi kwa ufanisi.

BABA BARAKA:    Najuta kunywa pombe sijui ni shetani gani aliyenipitia.

SIJALI:                      Usijute, mbona ni hali ya kawaida tu… utazoea siku si nyingi. Leo piga chupa moja, na kesho moja ila usilewe.

BABA BARAKA:    Eti nini? Tena acha kabisa hiyo kauli yako.

SIJALI:                      Mimi nilianza kama wewe lakini sasa hivi niko sawa kabisa, kwa sababu umeshaanza haitakiwi uache ghafla, lasivyo utaumwa sana?

BABA BARAKA:    Sawa mimi nakusikiliza wewe mzoefu… shida

yangu mimi nirudi katika hali yangu ya kawaida yaani najiona tofauti sana.

SIJALI:                      Sawa kuhusu hilo usijali rafiki yangu, upo na mimi mtaalamu wa ‘alcohol’

Wanapitia baa wakanywa, wakanywa, wakanywa mpaka wakalewa ndipo safari yakuelekea kazini inaendelea. Wanafika kazini wakiwa wamelewa chakari na kuanza kuwatukana wafanyakazi wenzao.

SIJALI:                      Nyie manamba fanyeni kazi kama nilivyowaagiza, mshahara wenu si mnapata!

(Wafanyakazi wenzake wanabaki wanamshangaa tu)

BABA BARAKA:    Na huyo mnayemuita Bosi wenu mwambieni kama kazi imemshinda hapa aje afanye kazi ya kufua nguo za wanangu (Anaendelea kutoa lugha chafu kwa Bosi wao na kuwaacha watu wote wakiwa wamepigwa na bumbuwazi)

SIJALI:                      Jamani tumechoka kuonewa hapa kazini mwambieni na huyo Bosi sitaki tena kufanya kazi kwake, mshahara mdogo hautoshi hata kununua chupa mbili za bia. (Anayumba yumba na chupa yake ya bia mkononi)

Baada ya siku tatu kupita habari zinamfikia Bosi na anawaita Sijali na Baba Baraka ofisini kwake

BOSI:                         Nimewaita hapa kwa jambo moja… nataka mtambue kuwa hiki ni kiwanda cha nguo na sio kiwanda cha pombe, juzi nilipata habari zenu kuwa siku hizi mnalewa sana, kazi hamfanyi na mnawatukana wenzenu! Lakini hiyo mmeona haitoshi mnanitukana hata na mimi! Kwanini 

                                    mmebadilika kiasi hiki?

SIJALI:                      Mimi ni kweli nakunywa pombe lakini katu siwezikukutukana Bosi wangu wala kuwatukana wafanyakazi wenzangu.

BOSI:                         Kwahiyo wamekusingizia? Watu wote wawasingizie nyie tu!

BABA BARAKA:    Samahani sana Bosi msema kweli ni mpenzi wa Mungu, mimi kweli sijawahi kutumia kilevi chochote tangu nizaliwe ila juzi na jana shetani alinipitia nikanywa pombe ila sikumbuki kama unayoniambia niliyatenda lakini nilitumia busara   nikawaomba radhi wafanyakazi wenzangu na pia naomba na msamaha wako bosi wangu.

BOSI:                          Unachekesha sana, yaani Baba Baraka umefanya kazi miaka yote hiyo ukiwa mfano wa kuigwa hapa kiwandani leo umebadilika hivi! Kweli umdhaniaye ndiye kumbe siye.

SIJALI:                      Lakini hatukudhamiria kufanya hivyo Bosi.

BOSI:                         Tena wewe nyamaza kabisa! Nisikilizeni, mkipata kazi fanyeni kazi kwasababu mkichezea kazi ni Kazi sana kupata kazi hapa mjini. (Wote wanaitikia wakiamini wamesamehewa) “Sawa bosi”

BOSI:                         Hivyo basi sihitaji wafanyakazi walevi, wazembe na wasiojitambua hapa ofisini kwangu leo mmefanya hivi kesho mtafanya makubwa zaidi ya haya, sasa chukuweni hii ndio zawadi yenu (Anamaliza na kuwapa barua ya kuwaachisha kazi na kuwaamuru watoke nje)

BABA BARAKA:    ‘Sory Boss, please…’ ninafamilia inanitegemea nilipitiwa bahati mbaya ‘boss’ naomba unisamehe nitajirekebisha.

BOSI:                          Tokeni nje lazima niwawajibishe ili iwe mfano

                                    kwa wenzenu na mtambue hii ni ofisi wala sio 

                                    genge la wahuni kama mnavyofikiria.

SIJALI:                      Kutenda kosa sio kosa bali.

BOSI:                         Sihitaji uswahili wako hapa, pombe mmekunywa kwa kujitakia halafu mniambie eti bahati mbaya! Kwani hamkujua kuwa pombe ni mbaya?

BABA BARAKA:    Bosiii…. Bosii tuhurumie.

BOSI:                         Hivi hamnisikii au hamnielewi nasema tokeni, tokeni nje au niwaitie askari? (Ananyanyuka toka kwenye kiti chake na kuanza kuwasukuma nje ya ofisi)

SIJALI:                      Twende zetu bwana unaomba kazi kama unaomba kuingia peponi! kama ni kazi zipo nyingi tu, asitubabaishe bwana (Anamvuta Baba Baraka mkono kwa nguvu na kutoka naye nje kwa jazba).

Wanaondoka na kurudi baa, wanaagiza pombe tena na kuanza kunywa kwa fujo huku wakijadili kilichotokea ofisini.

BABA BARAKA:    Hivi imekuwaje rafiki yangu mbona ghafla sana!

Au kuna mtu ametufanyia fitna tufukuzwe kazi?

SIJALI:                      Wewe kunywa pombe uondoe hayo mawazo, kesho pakikucha kila mtu atakuwa ana mawazo mapya.

BABA BARAKA:  Hapo umeongea hoja ya msingi rafiki yangu… (Ananyanyua chupa ya pombe na kuielekeza mdomoni kama tarumbeta)

SIJALI:                      Lakini rafiki yangu mchunguze sana mkeo ana mdomo mbaya sana kwani juzi ulivyotukuta pale nje alikuwa ananifokea kama mtoto mdogo, eti ooh mwache mumewangu… Eti mimi nakuharibu wewe, nikajua tu lazima mambo mabaya yatatokea na kweli yametokea haya. Yule mwanamke sio mtu mzuri hata kidogo.

BABA BARAKA:    Eti enheee! Basi atanitambua mimi ni nani, kama ni mchawi akawaloge hao hao ndugu zake sio mimi.

SIJALI:                      Mimi sijawahi kuona mwanamke anaongea kiasi kile, anatoa lugha chafu, anaongea kama chiriku! haijulikani Baba nani, Mama nani ndani ya nyumba! Inabidi umnyooshe…

BABA BARAKA:    Haswaa, hiyo ndio dawa yake, enzi za Babu zetu wanawake hawakuwa na mdomo hivi kwa waume zao lakini siku hizi kitu kidogo tu atakwambia anataka haki sawa (Wanamaliza kunywa pombe, wanainuka na kila mmoja anarudi nyumbani kwake huku wakitoa lugha za matusi mtaani)

Nyumbani kwa Mama Baraka watoto wamelala, mama Baraka amekaa kwenye kiti akimsubiri mumewe ghafla mumewe anaingia bila kubisha hodi.

BABA BARAKA:    Mama Baraka kuja hapa (Anamuita mkewe kwa ukali kama simba mwenye njaa hali iliyomshtua mkewe).

MAMA BARAKA:  Abee mume wangu (Anakuja mbio na kabla hajakaa vizuri anapewa kofi zito linalomuangusha chini puuu mpaka watoto wanaamka toka usingizini) uiii unaniuaaa! Unanionea buree jamani mume wangu

AISHA:                      Baba acha kumpiga Mamamwache mamaaaa (Aisha naye anashindwa kuvumilia na kuanza kulia huku akiwa amejificha nyuma ya mlango kwa woga)

Anaendelea na tabia ya kumpiga mkewe kila siku bila sababu za msingi mpaka Mzee Nyambo na Mzee Mtua wakaamua wamuite ili waongee naye juu ya tabia yake hiyo, wakiwa wamekaa chini ya mfenesi mkubwa uliyotengeneza kivuli cha kuvutia sana, wanamuagiza Baraka akamuite Baba yake ili wamuonye. Muda si mrefu Baba Baraka anaingia.

MZEE NYAMBO:    Karibu jirani.

BABA BARAKA:    Asanteni sana wazee wangu.

MZEE MTUA:          Baba Baraka sisi tumekuita hapa kama mtoto wetu, kama jirani yetu na pia kama wazee wa mtaa… tumekuita kwa ajili ya hiyo tabia yako uliyoianzisha ya ulevi na kumpiga mkeo, hakika haujengi bali unabomoa mwanangu… 

MZEE NYAMBO:    Swadakta mzee mwenzangu! Uliona wapi mke

                                    anapigwa ngumi na mateke? Je mama yako

                          angekuwa anapigwa na baba yako kiasi hiki wewe ungekuwa hivyo?

MZEE MTUA:          Haya hiyo haitoshi, je na matusi unayeyatoa mtaani uanawafundisha nini watoto?

 MZEE NYAMBO:   Pombe sio nzuri mwanagu, pombe ni adui wa maendeleo… pombe ililaaniwa hata na wazee wetu waliotutangulia.

MZEE MTUA:          Inabidi ujiheshimu na uiheshimu jamii inayokuzunguka… wewe unaona raha unavyowajaza majirani kwenye ugomvi usiokuwa na kichwa wala miguu!

BABA BARAKA:    Hapana wazee wangu ni shetani tu alinipitia

MZEE NYAMBO:    Shetani ni nani bwana, shetani ni wewe mwenyewe! kwani ni nani anamjua shetani, nani aliwahi kumuona shetani? hizo ni lugha za kujitetea tu na wala hazina mantiki (Wanaendelea kumshambulia kwa maneno kama mpira wa kona)

MZEE MTUA:          Mbona ulikuja hapa mtaani ukiwa kijana mzuri tu! nini kimekusibu? Jaribu kuepuka rafiki walevi uijenge familiya yako.

MZEE NYAMBO:    Sisi tumeishi hapa toka enzi za uhuru lakini hatujawahi kuona vituko kama hivi unavyovifanya wewe hapa mtaani, tunaomba ujirekebishe bwana.

BABA BARAKA:    Nimewaelewa wazee wangu, nanawaomba radhi na ninaahidi nitajirekebisha.

MZEE MTUA:          Sisi pia tulikuwa vijana kama wewe, tunajua ujana ulivyo kuliko hata wewe, sisi tumemaliza wewe ndio unaanza.

MZEE NYAMBO:      Tena afadhali hata na enzi zetu… sasa hivi dunia   

                                    imebadilika, watu wanasema wanaingia kwenye  

                          ulimwengu wa digitali sasa mbona wewe bado uko kwenye analojia? (Wote wanacheka)

MZEE MTUA:          Sisi ndio wazee wa mjini ukikaidi haya tunayokueleza yatakukuta mambo makubwa sana (Anaongea kwa lugha ya vitisho huku akikunja msuli wake vizuri)

BABA BARAKA:    Naapa kwa jina la mama yangu alioko kaburini… sitorudia tena pia mimi naumia sana kuwa hivi.

MZEE NYAMBO:    Haya bwana sisi yetu ni hayo tu… unaweza

ukaendelea na shughuli zako. (Wote wanamaliza na kutawanyika huku wakishikana mikono).

Usiku wa manane Baba Baraka anatoka baa na kusahau nyumba yake na kwenda kubisha hodi kwa fujo nyumbani kwa Mzee Nyambo huku kukiwa na giza totoro akijua ni kwake.

BABA BARAKA:    Hodii, hodii wewe mwanamke fungua mlango… au umenisahau eeh! Toka nje haraka nitavunja mlango.

MZEE NYAMBO:    Nani wewe saa hizi…

BABA BARAKA:    Fungua mlango mbwa wewe… unamuuliza nani maswali yako ya ajabu! Huna adabu mimi ndio Baba mwenye nyumba.

MZEE NYAMBO:    Mmh! Huyu nani saa hizi… anatukana kama yuko kwake au ni jambazi!

(Anajiuliza maswali na kwenda kuchungulia kwa dirishani na kukuta ni Baba Baraka)

BABA BARAKA:    Fungua nitavunja mlango.

MZEE NYAMBO:    Nini! Utavunja mlango? Jaribu uone, nitakufunga Jela… Alifungua mlango na kuanza kumfokea.

BABA BARAKA:    Samahani mzee wangu… nimepotea njia nilijua hapa ni nyumbani kwangu.

MZEE NYAMBO:    Toka hapa nenda kafie huko, yaani leo tu tumetoka kukuhusia lakini umetudharau sio? Haya toka, toka usinitafutie kesi mwana haramu mkubwa wewe.

BABA BARAKA:    Usinibabaishe wewe mzee haunitishi kwa lolote, unaringia nyumba wakiambiwa wenye nyumba watoke na wewe utatoka! Hii ni nyumba au kibanda.

MZEE NYAMBO:    Ondoka katapike huko kwako, umeshindwa

kutusikiliza sisi, ulimwengu utakufundisha.

BABA BARAKA:    Usinitishe bwana mimi pia naitwa Ulimwengu… Hii pombe nimekunywa kwa ajili yenu nyie ndio wachawi wa mtaa… sasa nilogeni mniue… nyie wazee wachawi sana ila hapa ndio mmegonga mwamba.

MZEE NYAMBO:    Eti nini? Sisi wachawi! Sasa wewe naona unavuka mipaka, dawa yako iko jikoni inachemka na utainywa tu.

BABA BARAKA:    Kama kuinywa utaanza wewe, tena usinitishe kabisa. Mwambie na huyo mchawi mwenzako kuwa hamtaniweza.

Kupata uhondo wote pata nakala ya kitabu hiki, wasiliana na mwandishi kwa mawasiliano Simu: +255756736348 au +255712631303

Author: Gadi Solomon

1 thought on “CHANZO NI WEWE

Comments are closed.