Hadithi ya Nyangeche

Na Wilbert Maridadi

Eric alianza kutweta kwa kijasho chembamba na kufanikiwa kuongea: “Nyangache … hapa ni nyumbani.  Pia kumbuka heshima na upendo wetu kwa Mungu.” Alitulia. Nilimtazama na kumshika mkono wake wa kulia na kumketisha katika kiti nami niliketi katika kiti kingine.Tulitazamana. Nilianza kuvunja ukimya na kusema: ”Najua nitakufa! Najua nitakufa! …Kifo ni nini? Nilitulia. Eric aliyekuwa ameketi kitini alikurupuka macho yake akanitazama. Maisha ni uchaguzi. Wako wachaguao vyema kama wewe na tupo tuchagua vibaya tukisubiri kifo. Tena kifo cha aibu. Eric. Nilichangua vibaya tangu kuzaliwa kwangu. Kutokana na uchaguzi mbaya, hata marafiki zangu na kikundi kilichopo ni kibaya. Rafiki yangu aliniamulia kesho yangu. …nastahili kifo. Nimewapoteza mabinti wengi. Kifo ni chipukizi nililolipanda mwenyewe. Ni kazi ya mikono yangu mwenyewe nastahili kifo Eric. Kuliko mama yangu kufa heri niondoke mimi. Kuliko baba yangu kufa kabla ya wakati ni bora nikaondoka mimi. Tazama sina mtoto wala mume  acha nife. Alitweta Nyangeche mbele ya Eric ambaye alikuwa kimya asofahamu kisichoendelea.  Taratibu taratibu aliamka na kusogelea Eric na kumbana  pumzi zake  kwa ukaribu. Yote niliyoyaongea leo sikuwahi kukueleza lakini leo nigali kijana, kigori na moyo wenye  upendo usiopimika juu yako. Amini kuwa kuishi na mimi  Etic unataka kuuvaa ugane mapema. Hakika nimeamini ule usemi usemao kuwa cha mbahili huliwa na wadudu. Amini Eric wadudu ndio wauguao. Nyangeche aliketi  kitini kuku akimtazama Eric ambaye wakati wote alikuwa  kimya.Tumaini ambalo lilianza kupenyeza  katika maisha ya Eric sasa aliliona likiyeyuka mithili ya barafu  katika jua. Alitafuta cha kuzungumza alibaki akivuta pumzi nzito. Alitafakari na kisha akasema:

“Hakika kujifunza si kazi rahisi.” Alimtazama Nyangeche ambaye kuwa ameketi akimtazama Eric aliyekuwa ameketi kitini. Alimsemesha:

“Huwezi kufa kirahisi. Kufa…huwezi kuniacha na hisi za kuvunja moyo muhibu.” Nakuahidi kuwa katika machweo sote tutakufa  na katika mapambazuko sote tutafufuliwa.” Alitulia kimya Nyangache alimfuata na kumnong’oneza  sikioni Eric.

“Hapana lisilokuwa na kiwango katika maisha Eric. Alimsogeza Eric kwa mikono yake.

“Ndiyo najua kuwa hakuna lisilokuwa na kiwango katika maisha, ila kwa nini ufe mapema namna hii! Aliuliza Eric huku akimtazama Nyangeche. Ilikuwa ni usiku na   Nyangeche alikuwa amelala. Eric naye akiwa na maswali mengi kichwani.  Swali lililokuwa likimsumbua ni kwa nini  Nyangeche  alikuwa  katika kuzima kiufahamu. Clara alikuwa Songea mjini tayari. Kichwa chake kilikuwa kizito katika kufikiri. Mawazo pekee yaliyomsumbua kuanzia Dar es Salaam ni kwa nini awe yeye  wa kwanza kuitekeleza kafara ile. Kwa nini mama yake afe. Nini faida ya kuua? Kuna uhusiano gani kati ya kuua na mali? Clara   akiwa katika mawazo yaliyomchanganya aliamua kuelekea mghahawani ili kupata chakula cha jioni. Aliketi na kuagiza chakula. Mhudumu alipokuwa akielekea  kutimiza matakwa yake alimwita. Mhidumu alimsikiliza akamwambia:

“Naomba kimywaji ambacho hakina kilevi sana. Mhudumu aliondoka. Clara akiwa mezani ghafla masikio yake yalivamiwa na sauti ndani yake.”

“Daima wafao ni wale ambao hawana watoto.” Alishtuka. Alitazama huko na huko asione kitu. Alianza kujiuliza hivyo hata nikimuua mama yangu haina shida? Mbona sielewi sauti hii?

“Kuzaa ndiyo mwanzo wa kufa.” Sauti ilinena tena ndani yake. Hakika sauti ilichachafya  vya kutosha. Clara alijiona yu sawa na viwavi. Alifikiri juu ya maisha yake . Aliutazama upendo wa mama kwa mtoto. Alikumbuka utoto ambao alikuwa akimtaabisha mama yake. Mawazo mfano wa tope zito kichwani  mwa Clara yalielemea mwili. Alishindwa kutafakari  hata mhudumu alipomletea chakula na kinywaji hakuwa na utambuzi. Clara alivuta chupa ya kinywaji na kuvuta fundo za mfululizo baada ya dakika kadhaa kama mzoefu wa pombe.  Alivuta chupa mbili na kuwa hoi. Akiwa katika meza yake, pembeni mwake alikuwa amekaa kijana mmoja ambaye alikuwa akimtazama. Kijana yule alijua fika kuwa msichana mzuri aliye pembeni mwake alikuwa hayupo sawa. Aliinuka na kumfuata mezani. Walikutanisha macho yao wakaketi chini. Kijana alimwagizia Clara kinywaji kingine. Waliendelea kunywa hadi saa nne na nusu na kijana akamuaga Clara.

“Dada nashukuru.”

“Unashukuru nini?” Alijibu kwa sauti ya pombe. Aliinua mkono wake wa kushoto na kumshika mkono na wakainuka wote. Alfajiri ilipotimu, Clara alijua kuwa alikuwa na mtu pembeni mwake. Alitazama huko na huko aliishia kuinamisha kichwa. Harufu ya kifo aliisikia katika masikio yake. Macho yalitazama kaburi lililokuwa  mbele yake. Ubongoni mwake alisimama Jong. Ghafla aliingia maliwatoni na kuanza kulia. Kilio hakikuleta maana kamili kuwa alilia utajiri au uhai. Alilitafakari kufu la furaha la utajiri aliloishi kwa miaka minane  sasa. Alilia kwa uchungu. Alishindwa kung’amua ni nani wa kumlaumu. Huzuni ilimea  katika moyo wake. Alijiona kuwa wambili havai moja katika maisha. Sura yake ilishuka ghafla  kwa huzuni. Huzuni ambayo iliharibu kabisa  tabia yake na katika sura yake. Huzuni ilichimba  uso wake. Kijana alokuwa ameachwa kitandani na Clara aliamka. Alitazama huko na huko asimwone Clara. Clara alikuwa mgeni wake wa neema. Aliinuka kitandani na kuelekea maliwatoni. Alipoufikia mlango aligonga, gonga ambayo ilimzindua Clara  kutoka kisima cha mawazo asubuhi ile. Kwake ile kauli siku njema huonekana asubuhi  ilikuwa kinyume. Aliinuka na  kuufuata mlango. Alipufungua tu nyuso zao ziligongana ana kwa ana. Clara alikuwa wa kwanza kuinamisha kichwa chini. Clara alitoka maliwatoni  na kijana akaingia kama mfano wa nyuki kupishana kwenye mzinga. Clara alijiuliza kijana huyu ametoka wapi? Ilikuwaje? Tangu lini mimi nakunywa pombe? Kumbukumbu za jana zilimjia  lakini kufikia katikati zilifutika. Alihisi zimetoweka  mfano wa analoji katika  ulimwengu wa watu ambao hawana rupia za kuingia katika digiti. Alijilaumu mno mara sauti katika mtima wake kukazusha mabishano:

Daima kivuli cha fimbo hakiwezi kumficha mtu jua.”

“Ama kweli wewe ni debe tupu” sauti ilijibu sauti nyingine ndani.

“Kelele ndio kiimo cha uhai.”

“Mweye kelele hana neno.”

“Acha niende  maana ninayo safari ndefu ya maisha.”

“Mkate mkavu wa nyumbani ni bora kuliko  nyuma ya shuwa.  Kila jambo lina mwanzo na mwisho wake. Mwanzo na mwisho huitwa safari. Sauti ilinyamaza na baadaye ikaendelea:
“ Mambo katika maisha ya mwanadamu huanza kama mambo ya ukwe. Huanza kama utani.” Sauti zilitoweka  na kijana aliingia chumbani akiwa amejifunga taulo alimtazama Clara aliyekuwa ameketi kitandani  kwa macho ya kutaka kuuliza. Clara alipoona  dalili hizo alilala kitandani na kugeukia ukutani. Kijana alivaa na kuonekana akitafakari  kitu. Alijiuliza ilikuwaje mtu ambaye walikutana naye jana na wameamka pamoja lakini hakuna hata neno. Alionekana kuzunguka huko na huko mfano wa mtu atafutaye  kitu  asikione. Aliuendea mlango na kutokomea. Clara akiwa katika kisima cha  woga wa kifo hakuweza kujua kilichoendelea. Punde mlango ulilalamika kwa ishara ya mtu kuingia ndani. Alikuwa kijana yule ambaye alikuwa mfano wa jehenamu kwa Clara. Mkono wake wa kulia ulikuwa umeshika kikaratasi na kukiweka juu ya meza. Aliamua kutokomea kusikojulikana . Baada ya usumbufu wa ufahamu wake , Clara aliinuka na kuelekea maliwatoni. Sehemu ambayo ilikuwa ni sehemu sahihi tafakari kwake. Alijiweka sawa kimwili. Alipomaliza alitupia macho katika meza ndogo na kuona  kikaratasi. Alipeleka mkono wake  katika ile meza  na kuinua kikaratasi  na kusoma:

 “Kwako Malaika…”

Hakika umekuwa malaika kweli kwangu. Hunenwa kuwa kicheko kikiwamo mdomoni  shukurani hutoka. Nami leo nasema, “Ewe binti  ulojaliwa uso wa fikra kwa sura isokuwa nyeupe wala nyeusi, macho ya kung’ara, meno ya mwanya yaliyokuwa sawa  na safu mbili za lulu katika mdomo na nywele za kushuka juu ya kichwa chako  cha umbo zuri vilivyoshikana sawia ili kuonyesha sawia upeo wa uzuri wako. Clara mwenye zuri mfano wako. Dahari hunenwa kuwa apendaye huwa kama mvuvi  aliyemezwa katika kisiwa kilichozungukwa na maji  na asijue la kufanya . Hivyo ndivyo ulivyo kwangu. Ingawa ni usiku mmoja tu umejaa mtimani kwangu. Hebu lazimisha mbonizo katika mshaololo huu:

“ U muhibu johari   almasi yako sitahiki.

Nakupenda.”

Alimalizia kijana kwa kuwasilisha mawazo yake kwa lugha ya maandishi. Kama nyoya za ndege  katika mkoba , Clara alijikuta amejibweteka sakafuni kama ishara ya kuzidiwa na maandiko ya kijana aliyomwandikia. Hakika ukitaka kujua harufu ya mtu kuwa naye karibu. Clara alishindwa kung’amua. Alikiona mkosa. Tena aliyestahili kifo. Kifo ambacho kilikuwa adhabu tosha. Aliitaabisha nafsi yake Kwa kuiuliza nafsi yake,” Kwa nini hakumsemesha japo kidogo kijana yule?” Taratibu alijiinua sakafuni na kujilaza kitandani. Clara alijihisi ameibeba dunia. Ulimi wake uliongea pesa ni nini? Pesa ziko wapi Jong? Mbona hazinisaidii kutatua hili? Alilia kwa uchungu. Uchungu ambao ulimlaza kitandani moja kwa moja. Eric na Nyangeche  walikuwa wakipata kifungua kinywa  mezani.  Macho ya  Nyangeche yalimwona mama Eric  na Joyce. Aliustaajabia uwezo wa Mungu katika uumbaji maana Joyce alikuwa halisi kama mama yake, kitendo ambacho kilimfanya Nyangeche atokwe na maneno:

“Ama kweli Joyce alikuwa kioo.” Baada ya kufungua kinywa walinyanyuka na kuiendea   sebule.  Hapa ni mahali ambapo Nyangeche aliwakuta wazee wa Eric  wakiwa wanatazama  runinga. Walimkaribisha Nyangeche ambaye aliitika kwa kuketi kitini. Mama Eric alikuwa  alikusanya mate yake  vyema ili kusafisha koo lake. Alikohoa kidogo  na kuzungumza.

“ Mama tunaomba utueleze  kwa kifupi historia yako.” Alizungumza huku akimtazama baba Eric ambaye naye alitingisha kichwa  kwa ishara ya kukubaliana na kauli ya mama Eric. Nyangeche  alijiweka sawa  na kuanza kueleza  historia yake  mbele ya kadamnasi ile. Akiwa katika pumziko  aongee kuhusu Duara la Utajiri simu yake iliita.  Aliitazama. Aliwatupia macho  hadhira yake ambayo ilimtazama  kwa mtazamo wa kumruhusu kuipokea.

“Haloo wewe ni Nyangeche? Unamjua Clara? Tumia namba hizo ujue  nini kinaendelea.” Sauti ambayo ilifululiza na isiache  nafasi kwa Clara ya kuongea. Ilikatika simu. Hakika Nyangeche  alikuwa akitoa na neno.

“Halooo! Halooo! Huku akitoa macho kwa Eric. Eric alimfuata alipokuwa amesimama alimuongoza na kumketisha chini. (Itaendelea)

Author: admin