Mfalme wa Kinanda -2

Mwandishi Grey Solver

KWA WASOMAJI WAPYA

UTANGULIZI…

Simulizi ya “Mfalme wa kinanda” ni simulizi ya kihistoria ambayo inaelezea namna mfumo wa siasa ya vyama vingi ulivyoingia kwenye nchi za kiafrika na kuratibiwa huku ukiua uzalendo wa viongozi wa kiafrika na kuzorotesha uchumi na afya za wananchi.

Riwaya hii inaeleza kuwa kabla ya mfumo wa uchaguzi wa viongozi wanasiasa kuingizwa Afrika, nchi za kiafrika zilikuwa na mfumo wake wa kiutawala. Nchi za magharibi zikaanza kuwarubuni wanasiasa wa kiafrika ili waige mfumo wao wa siasa na kuwaahidi kuwapa fedha za msaada kwa ajili ya kufanyia uchaguzi na kutatulia shida zingine. Ndipo na wanasiasa wa nchi ya Ntale walipoanza kumshinikiza Mfalme wao ili waingie kwenye mfumo wan chi za magharibi.

SASA ENDELEA…

Kapteni Ngongonile alikuwa mpiga KINANDA maarufu sana jeshini na hata mitaani. Popote alipopiga kinanda, watu walikaa kimya wakisikiliza ala nzuri za muziki zilizotoka kwenye kinanda chake. Kutokana na umahiri wake wa kupiga kinanda, mfalme wa nchi ya Ntale alimpa jina la MFALME WA KINANDA kama heshima, na wengi walimwita jina hili.
Kila sherehe za kijeshi na kitaifa kapteni Ngongonile alipewa nafasi ya kupiga kinanda ili kusherehesha, na alipokuwa akienda nje ya nchi vitani, sherehe zilipofika alikuwa akipewa amri na mfalme arudi nchini Ntale kwa ajili ya kupiga kinanda.
Mara nyingi Mfalme alipoalikwa kwenda nchi za nje kusuluhisha migogoro baina ya nchi na nchi, alikuwa akiambatana na kapteni Ngongonile kwa ajili ya kwenda kupiga kinanda. Ala za kinanda cha Ngongonile zililainisha mioyo ya wale viongozi ambao mfalme alienda kuwapatanisha na kufanya shughuli ya usuluhishi kuwa nyepesi kwake. Kutokana na umahiri wake, alisaidia kutatua matatizo mengi sana ya kimataifa.
Wanawake walimlilia kila kukicha majukwaani, na wengine walidiriki kuomba ridhaa ya kuzaa nae ili mradi tu watimize adhma ya mioyo yao, lakini Ngongonile aliwakataa.
Siku moja walipokwenda kusuluhisha mgogoro wa kisiasa nchi za ughaibuni, mfalme mmoja wa nchi za ughaibuni alimzawadia kinanda kikubwa aina ya YAMAHA kapteni Ngongonile. Kinanda kile kilikuwa toleo jipya, kilipigwa kwa mikono na miguu na kiliuzwa bei ghali dukani.
Akiwa nje ya nchi vitani, alikutana na binti mmoja mrembo sana aliyejulikana kwa jina Anna, na alikuwa mkimbizi. Anna alikuwa na ngozi ya rangi ya maji ya kunde, mrefu wa wastani, mwenye makalio makubwa na alikuwa na umbo la wastani. Alijaaliwa na tabia njema na staha mbele za watu. Wengi walimfahamu kama “Miss wa vitani”
Anna alikuwa na taaluma ya uuguzi na aliwasaidia majeruhi wengi sana wanajeshi na wakimbizi wenzake. Kapteni Ngongonile alivutiwa sana na Anna, na aliamua kumchumbia ili waanzishe mahusiano ya kimapenzi.
Kwani kulikuwa na mwanamke wa kumkatalia kapteni Ngongonile! Subutu! Licha ya kuwa na mwonekane wa mvuto kwa wanawake, kuwa na cheo kikubwa katika jeshi na kiongozi wa kambi ya mapigano, kapteni Ngongonile alijaaliwa pia vipaji vingi vya sanaa ambavyo vilimfanya afahamike na kupendwa na watu wengi. Kutokana na umahiri wake kwenye sanaa, sio wanawake tu waliompenda, bali hata wanaume na viongozi mbalimbali wa kisiasa wa ndani na nje ya nchi ya Ntale.
Walipokubaliana, kapteni Ngongonile na Anna wakawa wanaishi kama mme na mke ndani ya kambi ya vita.
Kuna minong’ono ya chinichini ilisikika kulekule ndani ya kambi ya vita kuwa Anna alikuwa mchumba wa mkuu wa kundi la waasi ambalo akina kapteni Ngongonile walipigana nalo vita usiku na mchana. Na pia ilisemekana kuwa Anna alitoroka kwenye kambi ya waasi akiwa na ujauzito usiozidi wiki mbili baada ya kutofautiana na huyo mpenzi wake. Na sababu ya kutoroka ilikuwa alimtaka mpenzi wake huyo asipigane vita na badala yake asaini mkataba wa amani na kiongozi wa nchi yake. Mpenzi wake alikataa na kuendeleza vita.
Anna alipoulizwa kuhusu minong’ono ile alikataa kuwa hajui lolote kuhusu uvumi ule na hakuwa mjamzito. Hata kapteni Ngongonile naye alijihakikishia kuwa Anna aliongea ukweli kulingana na jinsi alivyokuwa akiishi nae.
Baada ya muda wakiwa kulekule vitani, walizaa mtoto mwenye jinsi ya kiume, na Kapteni Ngongonile alimpa mtoto yule jina LUPALA likiwa na maana ya shukrani kwa lugha ya kwao.
Vita vilipoisha walirudi Ntale kuendelea na shughuli zingine za kijeshi.
Waliporudi nchini, Kapteni Ngongonile alipandishwa vyeo viwili na kuwa Luteni kanali.
Lupala alipofikisha miaka kumi na moja, mama yake alibahatika kushika ujauzito na kujifungua mtoto wa kike aliyejulikana kwa jina la Bahati. Jina hili alipewa baada ya mama yake kukaa miaka mingi bila kushika ujauzito.
Bahati alipofikisha miaka tisa, na kaka yake Lupala miaka ishirini, baba yao alipandishwa cheo na kuwa kanali na miezi michache baadae alikuwa Brigedia Jenerali. Wakati huo nchi ya Ntale ilikuwa inaongozwa kifalme na mfalme aliyejulikana kama “Mfalme Hawanga VI” ambaye alimteua Brigedia Jenerali Nyalimo Ngongonile kuwa kamishna wa kupambana na madawa ya kulevya akiwa na miaka arobaini na tisa.
Katika kutekeleza majukumu yake, Kamishna Ngongonile alidhani kuwa anapigana vita na wauzaji wa madawa ya kulevya pekee, kumbe alikuwa anapigana pia na wanasiasa na wafanyabiashara wakubwa wa nchi ya Ntale. Alikosa ushirikiano kwa viongozi wa serikali na wadau mbalimbali wa vyombo vya habari.
Alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kusambaratisha mtandao wa madawa ya kulevya mpaka nchi za jirani walifika Ntale ili kujifunza mbinu za kupambana na maharamia wa madawa ya kulevya.
Miaka sita alidumu kwenye cheo cha ukamishna, lakini vita ilibadili uelekeo na kuegemea upande wake. Mapambano yalipokuwa magumu zaidi Rais aliamua kumtoa madarakani Kamishna Ngongonile ili apumzike na kumteua mtu mwingine.
Kitendo cha kumvua ukamishna kiliwarahisishia mapigano adui zake kwani hakuwa na ulinzi tena wala kinga kutoka serikalini. Brigedia Jenerali Ngongonile hakupigana vita ya madawa ya kulevya kwa sababu ya cheo tu, bali alikuwa na nia thabiti ya kuyaondoa kabisa Ntale.
Maadui zake hawakukoma kuendeleza mapigano licha ya kutokuwa na madaraka ya kupambana nao.
“Baba Lupala punguza mwendo bhana, unaendeshaje hivyo gari?” aliongea Anna maarufu kama mama Lupala.
“Mama Lupala kuna watu wanatufatilia na gari nyeusi”
“Acha uongo, we umejuaje kama wanatufatilia”
“Angalia kupitia kioo, kuna gari linakuja kwa kasi sana. Sio mara ya kwanza leo kuliona gari hili likinifatilia” brigedia jenerali Ngongonile alipunguza mwendo wa gari.
Mara gari lililokuwa likiwafatilia likawapita kwa mwendo na kubana breki ghafla ili lizibe njia. Lakini walichelewa, tayari Ngongonile aliongeza mwendo na kuwapita kabla hawajaziba barabara.
Wakati gari ya maharamia ilipofunga breki ghafla na kusimama, mama Lipala aliweza kumtambua mtu mmoja kati ya maharamia waliokuwa ndani ya gari nyeusi.
Alikuwa mpenzi wake wa zamani, kiongozi wa waasi ambaye aliendesha vita wakati Ngongonile akiwa kapteni. Alijulikana kwa jina la KALIKWECHE.
Kalikweche alikuwa mtu katili sana, na alikuwa msambazaji mkubwa wa madawa ya kulevya nchini Ntale na nchi za jirani. Aliifanya kazi hii kwa siri sana na mara nyingi aliwatumia watu wengine kufanya kazi zake haramu.
Mama Lupala alianza kujiuliza maswali kadhaa bila ya kupata majibu;
“Inamaana Kalikweche nae anauza madawa ya kulevya? Au anataka kulipiza kisasi cha kumsaliti? Na kama anataka kulipiza kisasi miaka yote hii alikuwa wapi?”
Hakutaka kumshirikisha mme wake kwa maana alishawai kusema kuwa hakuwahi kuwa na mahusiano ya kimapenzi na kiongozi wa waasi tangu walipokuwa vitani. Kumwambia mme wake historia ya Kalikweche ni kama kuamsha vita baina ya mashujaa wawili, Ngongonile na Kalikweche.

Itaendelea kesho Ijumaa….

Kwa maoni: +255756926416/+255713880861, Barua pepe: mbwilagreyson@gmail.com

Author: Gadi Solomon