Haki yangu


Kuno kubaki sukuti, si kwamba nimepumbaa,
Nausubiri wakati, nifanya lenye kufaa,
Hata naiwe katiti, ama iliyo fakaa,
Iwavyo nitaitwaa, haki yangu siiwati,

Tena sitopiga goti, matozi ni mwae mwaa,
Sitishwi kwa kalimati, zilizo pambwa hadaa,
Viwavyo tajizatiti, nitwae kwa ushujaa,
Iwavyo nitaitwaa. haki yangu siiwati,

Na viwekwe vizingiti, wala sishikwi fadhaa,
Tapambana kama Nyati, kilomfika kichaa,
Sitochezeshwa foliti, nibaki nimezubaa,
Iwavyo nitaitwaa, haki yangu siiwati,

Nahari na lailati, kimya siwezi kukaa,
Uoga haunipati, nibaki nimenyamaa,
Namuhofu Jabaruti, dhuluma alokataa,
Iwavyo nitaitwaa, haki yangu siiwati.

Hayano si utondoti, mkamba sina kilaa,
Ndiyo yangu ithibati, moyoni niloivaa,
Na iyoyome sanati, sio ukomo wa baa,
Iwavyo nitaitwaa, haki yangu siiwati.

Mdhulumuo wanati, kisiki mme kikwaa,
Kuwata ni usaliti, unitiao kinyaa,
Nitakuja kitikiti, hata lizuke balaa,
Iwavyo nitaitwaa, haki yangu siiwati.

Kwa hapa kaditamati, twaeni beti sabaa,
Siongezi abiyati, naenda itibu njaa,
Kudai haki shuruti, hata naiwe bakaa,
Iwavyo nitaitwaa, haki yangu siiwatu.
MKANYAJI
HAMISI A.S KISSAMVU
📞 0715311590

Author: Gadi Solomon