HANYANYASI WANAWAKE

Mume aliye shujaa, mpole mwenye akili,
Jandoni aliyekaa, akafunzwa maadili,
Anayejuwa sawaa, halali nayo batili,
Katu hawezi diriki, kuwapiga wanawake.

Mume aliye farisi, mjua moja na mbili,
Mwenye mwingi ufanisi, katika lile na hili,
Ambaye kwake rahisi, hasira kuzihimili,
Katu hawezi diriki, kuwatusi wanawake,

Mume aliye mwerevu, anayejua asili,
Ambaye unyenyekevu, ni yake kuu adili,
Mjua changa na pevu, mume aliye kamili,
Katu hawezi diriki, kuonea wanawake.

Mume aliye timamu, atazamaye dalili,
Subira pia nidhamu, vema amezikabili,
Anayejua haramu, yamchukiza Jalali,
Katu hawezi diriki, kudhulumu wanawake,

Hapa naacha kutunga, sasa nazima kandili,
Mume ambaye si bunga, maarifa si kalili,
Miko anayeichunga, na mambo kuyajadili,
Katu hawezi diriki, kusimanga wanawake,

Mshairi Machinga,
mfaumehamisi@gmail.com,
+255716541703/752795964,
Dar es salaam, Kariakoo.

Author: Gadi Solomon