Hili la Kiswahili Rais katukumbusha tulilolisahau, tumuunge mkono

Amani Njoka, Swahili Hub

Hakuna shaka yoyote kwamba Rais Magufuli ni mkereketwa na kinara wa kukipigania Kiswahili. Moja ya juhudi zake za hivi karibuni ni kusisitiza matumizi ya Kiswahili katika Jumuiya za kimataifa kama SADC, EAC na nyinginezo. Alifanikiwa kupenyeza ushawishi wake hata kwa nchi za kusini mwa Afrika mathalani Namibia kufundisha Kiswahili, yapo mengi.

Hata alichokisema pale Dodoma si kigeni, ni mwendelezo wake wa kuonesha uzalendo na mapenzi ya dhati kwa lugha hii adhimu bila kujali vikwazo na maneno ya watu. Magufuli alipoeleza namna alivyosemwa na kukejeliwa kwamba hajui Kiingereza na wala siwashangai waliofanya hivyo, kwa sababu tupo siku za mwisho, siku ambazo kila mtu anafikiri tofauti na uhalisia, siku ambazo tunadhani vyetu si bora kuliko vya watu.

Sishangai kwa sababu hata mimi mwenyewe nimewashuhudia vijana wa Baba wa Taifa wakiwacheka ndugu zao Waswahili wakikosea kuzungumza Kiingereza halafu watampongeza Mwingereza kwa kukosea Kiswahili, kwamba amejitahidi, inasikitisha sana.

Kiswahili ni lugha ya taifa yenye misingi iliyowekwa tangu uhuru, lugha ambayo ilisaidia kuwaunganisha wapigania uhuru mpaka ikafanikiwa kuyaleta pamoja zaidi ya makabila 120. Watanzania wengi wana umilisi na lugha hii na wengi Kiswahili lugha yao ya kwanza. Ni kwanini hadi leo tunang’ang’ania lugha za watu tena tunajisifu na kujipiga kifua?

Mpaka sasa tunavyoongea kuna Watanzania wanafahamu zaidi lugha za kigeni kuliko lugha yao wenyewe tena wanaona fahari na kujipiga kifua kuwa wao ni wasomi na mioyo yao haiwasuti. Inashangaza Mtanzania asilia, mzawa anatembea barabarani hawezi kuongea hata sentensi moja ikaisha bila kuweka neno la lugha nyingine, sio kwa kupenda, ni kwa sababu ama hajui Kiswahili au. lugha aliyochomeka neno.

Kasumba walionayo wengi kwamba Kiswahili ni lugha ya watu wasiosoma au washamba na kwamba akiongea lugha ya kigeni ataonekana mjanja nio kujitapeli mwenyewe na kuuikana lugha yako ili ujifurahisha na lugha ya watu. Sipingi watu kuzungumza lugha nyingine la hasha! Isipokuwa hatupaswi kukitupa Kiswahili chetu na kukidharau kwa sababu ya lugha nyingine.

Wapo wanaohalalisha mawazo yao kwa hoja kwamba Kiswahili hakina msamiati wa kutosha, Rais alitoa jibu la kitaalamu kabisa kwamba hakuna lugha yenye msamiati wa kutosha. Ni ukweli mtupu, hakuna lugha inayojitosheleza, lugha zote duniani zimeathiriwa na lugha nyingine, lugha nyingi zimekopa msamiati.

Jambo ambalo wengi hawalifahamu na wanahitaji kuelezwa ni kwamba lugha zipo vile zilivyo kutokana na mahitaji ya watumiaji wake. Mfano, kama hakuna neno la Kiswahili lenye maana ya neno fulani la Kiingereza, si kosa la Kiswahili kukosa msamiati huo isipokuwa kwa Waswahili neno hilo halikuwa na matumizi tangu awali.

Pia, hakuna ubishi kwamba lugha inakua, kwahiyo hata msamiati unaokosekana leo unaweza kupatikana kesho. Kwahiyo hakuna haja ya kubeba mzigo mzito kwenye bongo zetu kwamba hatuwezi kukitumia Kiswahili kwa sababu hakina msamiati wa kutosha.

Lugha zote zimekopa msamiati au maneno kutoka lugha nyingine, hata lugha inayoonekana ni maana ya Kiingereza ina msamiati mwingi tu kutoka lugha za Kigiriki, Kijerumani na nyinginezo. Na ieleweke kwamba si kosa lugha moja ikitoa msamiati fulani kwenye lugha nyingine, ni jambo la kawaida kabisa la kimchakato katika kuathiriana kwa lugha kama ambavyo tamaduni za binadamu zinavyioathiriana.

Tuache woga na kukosa utashi, sisi ni Watanzania, ni watu wenye utamaduni wetu, asili yetu kama taifa na lugha yetu ni Kiswahili, Rais Magufuli ameona nini mpaka asisite matumizi ya Kiswahili kwa kiasi hiki? Umefika wakati wa kujipapambanua kwa lugha yetu na utamaduni wetu.

Tufahamu wazi kwamba lugha zote duniani zina watu wake, yaani Kiingereza, Kichina, Kifaransa au Kiitaliano kina watu wake. Hizi ni lugha zenye utamaduni wake kwa wake, kudhani kuwa ukizifahamu hizo lugha na kukipuuza Kiswahili utakuwa wa maana sana au kuonekana msomi ni kujidanyanya ingawa ni muhimu kuzifahamu.

Pongezi nyingi kwa Mh. Jaji Galeba, ataandikwa kwenye vitabu vya historia ikiwa kwamba alifanikiwa kuandika hukumu kwa Kiswahili na kumfurahisha Rais pamoja na wadau wa Kiswahili, tulipaswa tuwe tunefika huku muda mrefu sana. Bila shaka Mh. Jaji ametuonesha njia, amethibitisha kwamba Kiswahili kinaweza kutumika kwenye uga wa sheria na kila kitu kikaeleweka. Italeta ahueni kubwa Mtanzania anapewa nyaraka zilizoandikwa kwa Kiingereza, inawezekana hili limewaumiza wengi sana ingawa linaonekana kama suala dogo.

Shime tuamke, ukweli ni kwamba Kiswahili ndio lugha yetu, lugha nyingine ni za watu na haibadiliki. Ni wakati sahihi wa kubadilisha mambo, Kiswahili kitumike kufundishia, kitumike katika tafiti, afya, bidhaa kama ambavyo lugha zingine zinavyotumika. Kukumbatia lugha za watu na huku sisi ni Watanzania tena Waswahili ni utumwa wa karne ya 21, kujua sana na kuzikumbatia lugha za watu hakuondoi vinasaba vya Utanzania wetu.

Ufike Wakati kila Mtanzania aone fahari kukitumia Kiswahili, zile kasumba zinazokididimiza tuachane nazo. Rais Magufuli kaonesha njia, Mh. Jaji Galeba kaonesha kwamba inawezakana, tuinuke tuwafuate.

Mwandishi ni mdau wa Kiswahili na mwandishi wa Swahili Hub. Maoni na ushauri: 0672395558

Author: Gadi Solomon