
Assalam allaykum, naisalim jamii,
Nasalim binadam, viongozi wa dunia,
Salam ya isilam, salama iliyo dua,
Kutibu tibu mgonjwa, huwezi tibu maiti.
Maneno ya aghalabu, na akili za kitume,
Sineni yalo ghadhabu, vibaya msiniseme,
Kinywa cha kistaarabu, mekuja kutoa shime,
Kutibu tibu mgonjwa, huwezi tibu maiti.
Mwana mwenda mmwele, pitia huku chukule,
Mwana wewe mvimbele, kaulilo waambile,
Hayafi yalo yalele, ukufi utuzingatile,
Kutibu tibu mgonjwa, huwezi tibu maiti.
Vipi tuchimbe kaburi, maiti tuzifukue?
Na tena watanabahari, eti tiba upatie,
Maiti haiwi nzuri, ukweli tuupokee,
Kutibu tibu mgonjwa, huwezi tibu maiti.
Kufa wamekufa wengi, tena wakafa kibudu,
Jambo liliso msingi, hawakuwa waabudu,
ugonjwa wao shilingi, lakini hawakusujudu,
Kutibu tibu mgonjwa, huwezi tibu maiti.
Wagonjwa watazameni, walivyolala wodini,
Kama nyanya kirobani, jinsi walivyosheheni,
Hawa hata hamuoni, tiba muwapatieni,
Kutibu tibu mgonjwa, huwezi tibu maiti.
Mnasubiri wafe wote, tuchangishe rambirambi,
Wapo hai waokote, wodini kapige kambi,
Muwape amri wafate, matabibu wa vitambi,
Kutibu tibu mgonjwa, huwezi tibu maiti.
Wanasema bora kinga, kinga kuliko ya tiba,
kulia lia ujinga, wakishapata dhoruba,
Pelekeni waganga, na wakunga wa akiba,
Kutibu tibu mgonjwa, huwezi tibu maiti.
Tusifukue makaburi, kuwasaka marehemu,
Jambo lililo la kheri, tutafute mtaalamu,
Ugonjwa apige kufuri, usije shika hatamu,
Kutibu tibu mgonjwa, huwezi tibu maiti.
Ikifa imeshakufa, katu haitofufuka,
Tena taacha maafa, na pengo lisozibika,
Tutumie maarifa, madhira kuyaepuka,
Kutibu tibu mgonjwa, huwezi tibu maiti.
Jina la Mtunzi: Shaaban Maulidi
Lakabu: Nguo Ya Kuazima
Maoni Mapya