Ikisiri

UTAFITI

Ukisoma Swahili hub utaweza kupata maarifa mengi ya kazi za kifasihi na kiisimu zilizofanyiwa utafiti na mabingwa wa Kiswahili katika taaluma ya mashairi, tenzi, hadithi, nahau, nk. Kwa upande wa sarufi utafahamu kwa kina isimu ya Kiswahili kama muundo, maumbo, maana na matamshi fasaha ya Kiswahili.

Maana ya utafiti

Utafiti ni neno linalotumika katika nyanja za kisayansi na kijamii likiwa na maana ya uchunguzi wa kina wa jambo maalumu wenye lengo la kugundua na kupata maarifa mapya au kuongeza ufahamu.

Kwa upande wa lugha, ziko tafiti za fasihi na isimu ya Kiswahili zikilenga katika uchanganuzi wa jambo, utafiti elekezi, utafiti fafanuzi, utafiti ingizi, utafitimsingi, utafiti rasmishi, nk.

Taasisi za lugha na watu binafsi hufanya utafiti kwa lengo la kufafanua masuala ya lugha, ili kuongeza maarifa au kufafanua jambo fulani. Nitatoa mifano michache ya utafiti uliowahi kufanywa na pia ile ambayo itafanywa kwa faida ya wadau na wapenzi wa Kiswahili.

  • Mchango wa lahaja katika kukikuza Kiswahili sanifu: Iko mifano kutoka katika istilahi za Tiba na Uuguzi.” Na Zuhura Al Moh’d.

Lengo ni kuonesha namna lahaja zinavyoweza kuchangia katika kukuza Kiswahili. Msisitizo utakuwa katika kukuza tasnia ya tiba na uuguzi kwa kufuata msamiati na istilahi za Kiswahili. Mapendekezo yaliyowahi kutolewa ni kuunda istilahi kutoka katika lahaja za Kiswahili, lugha za Kibantu, lugha za Kiafrika na ikishindikana kutafuta maneno kutoka katika lugha nyingine nje ya Afrika. Njia ya utohozi hupendelewa lakini inatakiwa kutumika kama hatua ya mwisho.

  • Kilio cha Mwalimu J.K. NYerere Na Yasin S. Musa

Mwalimu J.K.Nyerere alipendelea Kiswahili kitumike katika siasa za Kiafrika badala ya lugha za kigeni kwani lugha za kigeni huuza utu wa Mwafrika (Bloommert, 1990). Lugha ya Mwalimu ilikuwa na mshawasha kwa wasomaji na wasikilizaji kila uchao hasa kuhusu walarushwa, mafisadi na wasiopenda amani.

  • Uchambuzi wa mashairi ya kisiasa ya Lamu

Na Rayya Timammy

Mashairi yamekuwa ni njia mojawapo ya kuwasilisha jumbe za kisiasa ambazo zinaweza kuwa nzuri au mbaya kwa makundi tofauti ya kisiasa

  • Sanaa kama kazi na biashara kueneza Kiswahili

Na Phibian Nancy Muthama

Multimedia Unversity of Kenya

Sanaa ni utanzu katika fasihi ambao ni kipengele pekee kinachoeneza Kiswahili. Sanaa na ushairi ndio iliyofanya Kiswahili kitambulike, Waswahili na mila zao, itikadi, desturi na dini kufahamika. Sasa lugha yeti inatambulika ulimwenguni kwa sababu ya sanaa.

  • Dhima ya Kiswahili katika uendelezaji wa Biashara ya kisasa.

Na Timothy Kinoti M’Ngaruthi

Maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi kwa kiasi kikubwa hutegemea maendeleo katika sekta ya biashara. Huhusisha wahusika wakuu wawili yaani mfanyabiashara na mteja wake. Kwa upande mwingine, sekta ya biashara haitegemei sekta ya mawasiliano ili kufikia malengo yake. Hii ni kwa sababu biashara hushirikisha wahusika wakuu wawili yaani mfanyabiashara na mteja wake.

  • Nafasi ya Kiswahili katika uhamasishaji na ushirikishwaji wa Umma kwa ujenzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Sangai Mohochi, Chuo Kikuu cha Rongo.

Malengo na mkakati ya maendeleo ni kuleta mabadiliko yanayoboresha hali ya maisha katika jamii. Kwa maana hiyo, fanaka ya mipango na mikakati hiyo hupimwa , hatimaye kutokana na athari yake katika maisha ya binadamu waliolengwa.

  • Nafasi ya Kiswahili katika elimu Tanzania

Na Musa Hans

Chuo Kikuu cha D’Salaam.

Lugha ni kitu muhimu sana katika mwasiliano ya sekta mbalimbali kama elimu, afya, sanaa. Mara baada ya Tanganyika kupata uhuru, lugha ya Kiswahili iliendelea kutumika katika sekta mbalimbali ingawa kwa viwango tofauti tofauti. Mathalan katika sekta ya elimu, Kiswahili liliendelea kutumika na sasa kinatumika kama njia ya mawasiliano katika ufundishaji wa masomo ya shule za msingi na vyuo vya ualimu ngazi ya cheti.Adha, Kiswahili ni somo la lazima kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne. Kwa upande wa elimu ya sekondari hadi vyuo vikuu, lugha ya mawasiliano ni Kiingereza na Kiswahili kinaendelea kufundishwa kama somo.

Kwa maelezo zaidi kuhusu utafiti uliofanywa kufanywa na mabingwa wa lugha asiliana na Taasisi ya Taaluma ya Kiswahili (TATAKI), Chuo Kikuu cha D’Salaam au Shule ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Serikali (SUZA), Zanzibar.

*********************

IKISIRI

Hili ni neno jipya ambalo halijafahamika sana kwani linatumika katika masuala ya kitaaluma hususan masuala ya utafiti. Kwa kawaida watafiti wanapoandika maelezo kuhusu maudhui wa mada waliotayarisha, hupenda kutoa maelezo mafupi kwa wale wasomaji ambao hawana muda wa kusoma ripoti yote.

Hivyo huandika maelezo mafupi ya kuweka jambo bayana. Huu ni ufupisho wa ripoti husika au ikisiri.

Katika programu ya kongamano la Kimataifa lililotayarishwa na Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki, Mada Kuu ilikuwa “Kuleta mabadiliko katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kutumia Kiswahili.

Mada zifuatazo ni matokea ya ikisiri zilizotayarishwa:

  1. Kiswahili kwa uimarishaji wa Ushirikiano na Utangamano wa kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Na Anna M. Kishe wa Teofilo Kisanji University,

Dar es Salaam.

Maelezo yafuatayo yanakusudia kujadili dhima ya lugha ya Kiswahili katika kuimarisha ushirikiano na utangamano wa ukanda wa Afrika Mashariki. Utangamano wa Afrika Mashariki kupitia Kiswahili si jambo geni kabisa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kiswahili kilikuwapo na kilikuwa sehemu muhimu ya kijenga ushirikiano wa kikanda. Jumuiya ya kwanza ya Afrika Mashariki iliundwa na nchi za Kenya, Tanganyika, Uganda na Zanzibar. Jumuiya ya sasa iliundwa mwaka 1967 na kuvunjika mwaka 1977.

Lugha ya Kiswahili ilionekana kuwa ni nyenzo madhubuti ya kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizi hasa kwenye masuala ya elimu, uchumi, ustawi wa jamii, sayansi, teknolojia, utamaduni na lugha Jumuiya mpya imeleta mabadiliko katika utendaji na mipango ya kazi.

Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa Kamisheni ya Kiswahili, Prof Kenneth Inyani Simala, Jumuiya mpya inaashiria utangamano wa kikanda unaoendana na mwelekeo wa sasa wa dunia ambapo lugha inachukuliwa kama taasisi muhimu inayostahili kuzingatiwa kwa makini.

Hivyo lugha ya Kiswahili inaagaliwa kama nyenzo muhimu katika kuimarisha ushirikiano na utangamano wa kikanda kwa maendeleo endelevu.

Na Antoney Owino Oloo

Chuo Kikuu cha Kababtii Lugha ya Kiswahili ambayo ndiyo inayoongoza kwa ukubwa na umaarufu miongoni mwa lugha kuu za asili za Afrika imezidi kushuhudia mwamko mpya. Kadiri inavyozidi kubadilika na kuashiria dalili za kutumiwa na watu wengi duniani kote, ndivyo inavyozidi kukumbatia na kutumika kwenye majukwaa mbalimbali ya utandawazi.

Miongoni mwa majukwaa hayo ni Swahili Hub ambao ni mradi mahususi wa kukikuza, kukiendeleza na kukiimarisha Kiswahili. Tafsiri ya Swahili Hub ni kitovu cha Kiswahili. Kitovu hiki kina tovuti yake inayohifadhi, kukuza na kuendeleza taaluma ya Kiswahili mtandaoni.

Ni mojawapo ya majukwaa yanayohimiza matumizi ya lugha ya Kiswahili mtandaoni. Kiswahili pia inatumika vilivyo katika tovuti ya kupeana, kupeleka na kutafuta taarifa.

Tovuti za Kiswahili zimezagaa duniani na nyingi ziko Marekani na Ulaya na hata Afrika zimeanza tovuti zenye kufundisha Kiswahili, kusoma na kusikia kupita kompyuta.

Zipo kamusi za Kiswahili, makala na maelazo ya kitaaluma kuhusu Kiswahili. Ziko injini za (search engines) zenye kutumia Kiswahili (mfano Google). Juhudi mmbalimbali zimekuwa zikifanywa katika kukienzi Kiswahili katika naja za sayansi na teknolojia. Miongoni mwa juhudi hizo ni kutekeleza Mradi wa Swahili Language Manager (SALAMA) kwa ushirikiano na TATAKI na Kikuu cha Helniski unaokusanya maneno na matini za lugha ya Kiswahili, kuwa na kusanyo la data za Kiswahili na kisha kuchanganua kiisimu, kupatia tafsiri za Kiingereza na kuhifadhi kwa ajili ya watumiaji.

3. Kiswahili nchini Rwanda: Ufunguo wa maendeleo endelevu katika Afrika Mashariki

Na Cypren Nyomugabo

Chuo Kikuu cha Rwanda, Koleji ya Elimu

(UR-CE)

Kijiografia na kihistoria Rwanda ni nchi ambayo haina budi kuhusiana na lugha ya Kiswahili. Jamii hii inapakana na nchi zinazotumia Kiswahili . Kwa upande wa kihistoria ni koloni wa Kijerumani tangu mwaka 1892 hadi 1914. Waliwezesha Kiswahili kuingia Rwanda, nchi ambayo wakati huo ilikuwa katika ukoloni wa Kijerumani.

Huu ulikwa ukanda uliokuwa na Kiswahili kama lugha rasmi.

Watu wengu hutaka kujua nani allyekuwa wa kwanza kuleta iswahili nchini Rwanda. Watawala wa Kijerumani, walifanya biashara wa Kiarabu, dini ya Kiislamu au wamisionari wa kizungu.

Inaaminika kwamba lugha ya Kiswahili iliingia Rwanda na utawala wa Kijerumani mwishoni mwa karne ya 19. Ndiyo sababu Kiswahili Rwanda kilipitia mihula mitatu muhimu. Kiswahili kama lugha ilizungumzwa Rwanda mwaka 1900-1929. Katika muhula huu ambao ni kipindi cha utawala wa Kijerumani kinachukuliwa kama muhula wa staha wa Kiswahili. Maadam Mjerumani alikiteua Kiswahili kuwa lugha dhadi ya Kidachi na Kinyarwanda.

Muhula uliofuata ulikuwa kipindi cha Kiswahili usingizini (1929-1979). Mnamo mwaka 1929 Wabelgiji walipiga marufuku Kiswahili kwa nia ya kufuta mabaki ya athari za utawala wa Kijerumani hadhi. Kifaransa kikachukua nafasi ya Kiswahili.

Hali hii ya kutopata thamani na hadhi lugha ya Kiswahili iliendelea hadi mwaka 1979. Kipindi kilichofuata ni muhula wa tatu kuanzia mwaka 1979 hadi sasa ambapo kumekwa na mwamko mpya wa lugha ya Kiswahili.

Tarehe 2 Machi, 1979 Serikali ya Rwanda na Tanzania zilitiliana saini mkataba wa ushirikino katika nyanja za elimu na utamaduni. Tanzania iliipatia Rwanda walimu na wataalamu wengine wa Kiswahili

Tarehe 17 Oktoba, 2017 Rwanda iliteua lugha ya Kiswahili kuwa lugha rasmi pamoja na Kinyarwanda, Kiingereza na Kifaransa. Hii ni hatua muhimu kwa lugha ya Kiswahili na wadau wa Kiswahili hasa walimu na wachapishaji vitabu waanze kuichangamkia fursa hii.

Mifano Ya Ikisiri