Jafo apigia chapuo Kiswahili tovuti ya Taasisi Bonde Mto Nile

Jafo akipigia chapuo Kiswahili akizindua tovuti ya Taasisi ya Bonde la Mto Nile  wakati wa  mkutano wa Baraza la Mawaziri wa maji wanaopitiwa na bonde hilo

Elizabeth Edward, Mwananchi

eedward@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira,  Suleiman Jafo amezindua tovuti Taasisi ya Bonde la Mto Nile (NBI).

Uzinduzi huo umefanyika wakati wa mkutano wa baraza la mawaziri wa nchi wanachama wanaopitiwa na bonde hilo uliofanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa NBI, Sylvester Matemu amesema tovuti hiyo imeanzishwa kwa lengo la kukusanya na kuhifadhi taarifa zinazohusu rasilimali za maji kwa nchi wanachama wa bonde hilo.

Amesema, “Katika jumuiya yetu takwimu na taarifa sahihi imekuwa tatizo ndiyo maana tumetengeneza tovuti hii ili kupata taarifa za uhakika zinazohusu maji katika bonde hili.

“Tunayo machapisho na taarifa nyingi lakini hayachapishwi na kuwafikia walengwa hivyo ujio wa tovuti hii unasaidia kuziweka pamoja taarifa na machapisho hayo na hata wadau wa maendeleo wataona huko,” anasema Matemu.

Akizungumza kwa niaba ya Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, Waziri Jafo amewataka wanachama wa jumuiya hiyo inayopitiwa na Bonde la Mto Nile kufanya kila linalowezekana kutunza chanzo hicho muhimu cha maji.

“Ajenda ya kupambana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi iwe endelevu kwetu sote maana wote tunafahamu umuhimu wa maji, hivyo tuna kila sababu ya kukilinda chombo hiki.”

Aidha Jafo amesisitiza matumizi ya Kiswahili kuwa lugha ya kazi akiitaka jumuiya hiyo kuona umuhimu ya kuiweka lugha hiyo kwenye lugha zake za kazi na mawasiliano kama ilivyo kwa Kiingereza na Kifaransa.

Author: Gadi Solomon