Kaacha Mwiko


Kisamvu nayoyaona, kimenishika kicheko,
Mfano wa kufanana, kwa hili wala hauko,
Alojitia mapana, limemfika anguko,
Mpishi kaacha mwiko, pishi vipi litafana?

Pishi vipi litafana, wale wa huku na huko,
Mpishi ulojivuna, upishi ni kazi yako,
Kumbe lolote hauna, watulisha bokoboko,
Mpishi kaacha mwiko, vipi pishi litafana?

Unahaha kila kona, jikoni ni kokokoko,
Kinachopikwa hakuna, zaidi manung’uniko,
Jikoni pamekazana, mpika waacha piko,
Mpishi kaacha mwiko, vipi pishi litafana?

Ugani tumejazana, twangoja madikodiko,
Maswali tunauzana, kunani kunako jiko,
Sifa zile kumbe hana, lilikuwa hamaniko,
Mpishi kaacha mwiko, vipi pishi litafana?

Inanishangaza sana, wajihi na sifa zako,
Viungo kila namna, vilijazwa kwenye meko,
Umeshindwa muungwana, kuonyesha sifa yako,
Mpishi kaacha mwiko, vipi pishi litafana?

Ungatwambia bayana, hapa tusinge kuwako,
Umesha vukwa mchana, kuchutama si kituko,
Ona umechamba sana, umetwachia mnuko,
Mpishi kaacha mwiko, vipi pishi litafana?

Ndimi wa vito msana, kaditama hino mbeko,
Vina hulipwa kwa vina, ja pipa na mfuniko,
Ushakuwa huna mana, kutushindisha wenzeko,
Mpishi kaacha mwiko, vipi pishi litafana?.
MKANYAJI
HAMIS AS. KISAMVU
kissamvujr@gmail.com

     0715311490/0784311590
          BAITU SHI RI
          MABIBI- DSM
           TANZANIA
          

Author: Gadi Solomon