Kakama kuadhimisha siku ya Kiswahili Duniani

na Pelagia Daniel

Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika mashariki Kakama ambayo katika kuadhimisha siku ya Kiswahili Duniani, imeandaa kongamano la kuadhimisha siku ya Kiswahili Duniani litakalofanyika tarehe 6-7 Julai Golden Tulip Hotel, mjini Zanzibar mada kuu ikiwa “Kiswahili kwa Amani, Ustawi na Utangamano wa Kikanda”.

Katika kongamano hilo kuna mada ndogo ambazo zinatarajiwa kutolewa na wataalamu mbalimbali kutoka nchi za Afrika Mashariki. Ambapo mada hizo ni “Kiswahili na vyombo vya habari” inayotarajiwa kutolewa na Bw Jacob Riziki kutoka nchi ya Burundi katika mada hio italenga kueleza namna lugha ya Kiswahili inavyotumika kuuhabarisha umma kupitia vyombo vya habari

Pia jamii katika kujipatia mahitaji yake huitaji lugha ambayo itawarahisishia mawasiliano kutokana na changamoto mbalimbali ambazo wanajamii wanazipata hasa katika baadhi ya maeneo wanapohitaji huduma za kijamii kama afya hasa maeneo ambayo lugha inayotawala sio Kiswahili sanifu. Kamisheni imeandaa mada muhimu itakayotolewa na Prof. Clara Momanyi kutoka Kenya mada “Kiswahili na huduma za jamii”

Sekta ya biashara imekuwa ikikuza uchumi wa nchi katika kulichukulia uzito suala hilo Kiswahili ikiwa miongoni mwa bidhaa. Kamisheni imeandaa mada ya “Nafasi ya Kiswahili katika Biashara na uchumi wa Kikanda” itakayotolewa na Prof. Cyprian Niyomugabo kutoka Sudani Kusini.

Katika sekta ya elimu Kiswahili imekuwa lugha inayotumika kutolea elimu katika ngazi mbalimbali ikiwemo vyuoni imekuwa programu inayojitegemea. Katika hilo Kamisheni imeandaa mada “Kiswahili na Elimu, Sayansi na Ubunifu kwa maendeleo ya Kikanda” itakayotolewa na Bw. John Atem kutoka Uganda.

Kiswahili kimepewa nafasi kubwa kama lugha rasmi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, hii ni kutokana na harakati mbalimbali zinazofanywa na viongozi wa serikali katika kukithaminisha Kiswahili. Kamisheni pia imeandaa mada “Kiswahili kama Lugha rasmi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki: Changamoto na Mustabali” itakayotolewa na Austin Bukenya kutoka Uganda.

Katika kutambua mchango na nafasi mbalimbali za wataalamu na waasisi wa lugha ya Kiswahili Tanzania imeandaa mada maalumu “Shabaan Robert: Makavazi na Urithi wa Kiswahili” mada hiyo itatolewa na Prof. M. M. Mulokozi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaamu.

Mbali na mada hizo kongamano litaambatana na maonyeho ya vitabu, usiku wa Mswahili ambao utajumuisha mavazi, vyakula na burudani za Waswahili.

Author: Gadi Solomon