Kasoro ya mkia

Msambe nimechukia, kwa huno wangu uneni,
Zanitatiza tabia, walo nazo ikhiwani
Za utu kuwakimbia, na chuki kuwa moyoni,
Kumbe nao hayawani, kasoro yao mkia

Wanafanana hisia, na akili za kichwani,
Sio wa kufikiria, wakaweka akilini,
Hata kiwasaidia, hawakumbuki hisani,
Kumbe nao hayawani, kasoro yao mkia.

Wako ladhi nawambia, wote mungie tabuni,
Lengo likose timia, ndipo huwa furahani,
Si watu walo timia, wana fanana na Nyani,
Kumbe nao hayawani, kasoro yao mkia.

Si wandama njema ndia, hila zimewasheheni,
Chini chini hupitia, Kusaka wako undani,
Walivyo kama shazia, ipenyavyo mkekeni,
Kumbe nao hayawani, kasoro yao mkia.

Pamoja mtatumia, kiwanacho mfukoni,
Sana watakusifia, wana yao mtimani,
Kwa ndani wanaumia, ghiliba ipo surani,
Kumbe nao hayawani, kasoro yao mkia.

Nyamayo wanajilia, peke wakiwa pembeni,
Kutuzi watakutia, wakuteme mtaani,
Sahau imewangia, jana uliwaauni,
Kumbe nao hayawani, kasoro yao mkia.

Tamati na tamatia, nahao tuwe makini,
Wala hawakutimia, japo wazuri machoni,
Kilio watakwachia, kitegemea aini,
Kumbe nao hayawani, kasoro yao mkia.

                    MKANYAJI 
            HAMIS A.S. KISAMVU
                  0715311590
         [email protected]
           Baitu shi'ri- Mabibo
         Dar es salaam - Tanzania
               04-january-2023

Author: Gadi Solomon