Kaulimbiu za Simba zilizowafikisha hatua ya robo fainali

Dkt. Ahmad Sovu

Ndugu zangu, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania-Kazi iendelee. Kwa wale wapenzi wa makala zetu ambao wengi wamezoea makala zetu zilizo nyingi huwa zikichambua masuala anuwai yahusuyo hotuba za viongozi wetu, lugha yetu adhimu ya Kiswahili na siasa.

Uchambuzi wetu wa leo umejikita katika suala la michezo, lakini kwa muktadha wa namna matumizi ya lugha za hamasa (kaulimbiu au misemo) zinavyosaidia kuchagiza mafanikio ya timu fulani au chama au asasi nyingine yoyote ile ya kijamii.

Kaulimbiu kama tulivyowahi kufafanua katika makala zetu huko nyuma. Ni misemo rahisi inayotumiwa zaidi na wanasiasa au asasi fulani kwa lengo la kujenga hamasa yenye madhumuni ya kufikia malengo fulani.

Makala haya maarubu yake makuu, ni kutaka kuonesha namna Timu ya Simba ya Kariakoo, Dar es salaam -Tanzania ilivyoweza kufikia hatua ya juu ya mashindano ya Klabu bingwa barani Afrika pamoja na mambo mengine lakini kwa umuhimu wa misemo au kaulimbiu mbalimbali.

Pamoja na kujizatiti kwa maandalizi mengine ya kuimarisha kikosi kama klabu ya mpira wa miguu, Simba pia walitumia kaulimbiu mbalimbali kwa lengo la kujenga morali na kutia shime wachezaji, viongozi na mashabiki ili kufikia malengo yao.

Hivyo basi, msingi wa makala haya mwega wake upo kwenye kaulimbiu naweza kuiita kaulimbiu kuu ya ‘Kwa Mkapa Hatoki Mtu’.

Uwanja wetu mkuu wa michezo umepewa jina la aliyekuwa Rais wa awamu ya 3, hayati Mzee Benjamin William Mkapa. Kwa hivyo kaulimbiu ya Simba ililenga kuonesha kuwa mechi zote zitakazochezwa kwenye uwanja wa nyumbani hakuna timu itakayoshinda mchezo ndani ya dimba hilo. Yaani kwa Mkapa hatoki mtu. Wakimaanisha katika uwanja wa nyumbani Tanzania hatutafungwa na timu yoyote ile katika uwanja huo.

Ilianza kama mzaha, lakini hadi jana imethibitika kuwa kwa Mkapa hakutoka mtu.

Timu ya Simba ilitolewa kwenye mashindano hayo na timu ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini kwa ushindi mwembamba wa goli 1. Yaani 4 kwa 3.

Ufuatao ni baadhi ya uchambuzi wa kaulimbiu au misemo 7 maarufu ya Simba zilivyoichagiza kaulimbiu kuu ya kwa Mkapa hatoki mtu.

Ingawa misemo hii iliyo mingi imebuniwa katika lugha ya Kingereza rahisi. Kiingereza ambacho Watanzania wengi wanakifahamu maana yake.
Misemo hii ilichagizwa na mbwembwe, madoido, ukabobo, kujishongondoa, kujitanibu na hata kujifaragua kwa mnenaji wa timu hiyo Ndugu Haji Manara. Uwasilishaji wa Manara kwa misemo na kaulimbiu hizi ulisaidia sana kutamalaki kwake.

Ukiachilia mazonge au ukayeye wetu wa Usimba na Uyanga Manara naweza kusema aliifanya kazi yake vilivyo.

Sasa hebu tuidurusu misemo au kaulimbiu hizo hapa chini:

 1. Simba Next Level
  Msemo huu ambao una maana ya TIMU ya Simba ni ya kiwango kingine cha juu. Msemo huu ulilenga kuwajenga kisaikolojia wachezaji, viongozi wa Simba na hata mashabiki kuwa timu yao ni ya kiwango cha juu ukilinganisha pengine na timu nyingine za Tanzania. Haya tuliyashuhudia hata pale ambapo mashabiki wa Simba wakihojiwa walikuwa wakitamba na kujimwambafai kuwa wao ni wa kiwango cha juu. Saikolojia katika msemo huu ulisaidia sana kuifanya timu ya Simba kujiamini na kusonga mbele katika kila hatua. Wachezaji walijiona wao ni timu kubwa na wanastahiki kuchukua ubingwa.
 2. Do or Die
  Kaulimbiu au msemo mwingine ulikuwa ni huu wa ‘Do or Die’ ukiwa na maana ya kufa au kupona. Kama kumbukumbu zangu ziko sawa msemo huu ulichagizwa wakati wa mechi ya marudio baina ya Simba na timu ya AS Vita ya Congo. Kufa au kupona unaweza ukaona ni maneno machache na mepesi? Lakini yalisaidia kuijenga saikolojia ya wachezaji wa Simba. Kufa au kupona, yaani liwalo na liwe ushindi lazima. Hii ni kauli inayoongeza ari ya kujituma kwa hali zote kuhakikisha ushindi unapatikana. Kaulimbiu hii ilizaa matunda na kuifanya Simba kuendelea kujizolea alama Katika hatua za makundi. Msemo huu pia ulisikika ukitolewa na mashabiki wa Simba kuwa na wao walikuwa wakisema tu ni kufa au kupona leo.
 3. War in Dar (WIDAR)
  Msemo au kaulimbiu hii ambayo ina maana ya vita ndani ya Dar es Salaam. Kama asemavyo Mtangazaji wa Azam, Baraka Mpenja. Msemo huu haukumaanisha vita ya vifaru, bunduki za SMG au AK 47 wala mabomu na kuuuwa watu la hasha. Ni vita ya kisoka, ni vita pira biriani, pira sambusa. Msemo huu ulihanikiza mechi ya marudio kati ya Simba na Platinum. Nakumbuka Simba aliibuka na ushindi wa bao nne katika uwanja wa Mkapa. Ilikuwa vita kweli, wachezaji walijituma wakapambana vilivyo na kuishinda vita ya kisoka. Msemo ‘war in Dar’ unaifanya Simba kubakia kileleni mwa kundi lake.
 4. Total war Point of no return
  Kaulimbiu au msemo mwingine ulikuwa ni huu, msemo huu ulimaanisha vita kamili kwa hatua hii hakuna kurudi nyuma .

Ama kwa hakika misemo hii ni muhimu sana kwani huongeza siha na afya kwa wachezaji na wadau wote wa timu inayohusika. Kuwaambia wachezaji sasa ni vita kamili na hakuna kurudi nyuma ni jambo linalowapa ukakamavu, uimara na linalotia nguvu kukabiliana na timu pinzani. Katika hali hiyohiyo tulishuhudia vita kamili na Simba kuendelea kujinyakulia alama muhimu dhidi ya Al Ahly na kuzidi kusogea mbele zaidi katika mashindano hayo. Ambapo Simba ilimaliza Michezo yake katika hatua za makundi. Simba iliibuka ikiwa kinara katika kundi lake kwa alama 13 dhidi ya wababe kama Al Ahly ya Misri. Vita kamili waliyoinadi iliwafanya Simba wasirudi nyuma.

 1. Visit Tanzania
  Msemo mwingine ni huu wa Visit Tanzania, ukimaanisha tembelea Tanzania. Simba baada ya kusogea katika hatua zaidi katika mashindano hayo, walianza kuiona fursa ya kuitangaza nchi yetu ya Tanzania. Wakaona pia hatuwezi kuitangaza nchi tu hivihivi wakaamua kubuni msemo wa Tembelea Tanzania huku usawiriwa na picha za Mlima Kilimanjaro. Ingawa kwa maoni yangu ingekuwa tembelea Tanzania hakuna matata. Msemo huu ulihanikizwa katika fulana zao, mabegi, barakoa na vifaa vyao mbalimbali. Mawaziri wenye dhamana nao kwa wakati huo waliiunga Simba mkono. Kwani msemo huo ulichagiza uchumi katika kukuza utalii wetu. Simba walisafiri Congo, Sudan, Misri na Afrika Kusini. wakiwahamasisha kila wanayekutana naye kutembelea Tanzania. Maana waliwahimiza wageni kuja kutembelea nchini mwetu. Tembelea Tanzania Simba Sports Club.
 2. Pira Biriani
  Msemo mwingine ni huu wa pira biriani. Msemo huu ulikuwa na maana ya Mpira wa Biriani. Biriani ni aina upishi wa wali ambao kwa siku za hivi karibuni chakula hiki kimepata umaarufu sana hasa katika majiji ya Dar es salaam, Mwanza, Tanga, Unguja, Dodoma na kwenye miji mbalimbali. Chakula cha biriani kimetengewa siku mahsusi ambayo huliwa kwa wingi. Mathalan, kwa Dar es salaam watu wengi hutoka katika ofisi zao siku za Ijumaa na kwenda kwenye vijiwe, nyumba, migahawa, hoteli mbalimbali kwenda kula Biriani kwa lengo la kukidhi haja ya mioyo na mitima yao.😄😄 mambo ya Dar na Biriani 🍝.

Katika hali kama hiyo timu ya Simba inataka kuonesha aina ya mchezo wanaoucheza. Wanatafuta msemo rahisi wa kuwaelewesha mashabiki wao na wanaamua kubuni msemo pira biriani kwa mujibu wa mchambuzi wa masuala ya Michezo ndugu Ali Kamwe katika makala yake ya “mambo 10 niliyoyaona Simba Vs Kaizer Chiefs” anaelezea namna pira Biriani lilivyotamalaki pale kwa Mkapa Simba walipocheza na klabu ya Kaizer Chiefs anaposema,
Simba wamepiga mashuti 32 na on target 10, Chama aliutembeza mpira hakuna na mambo mengi, Boko kaweka kamba 2 muhimu, sub ya Muzamir na Morisson na Asante kwa Thabalala aliyekuwa akitoa superb sana kwenye kuipandisha timu na kuidumbukia vyema katikati muda ambao viuongo wake walivamia zone ya Kaizer…

uchambuzi huu wa Alikamwe unaonesha namna msemo wa Pira Biriani ulivyooneshwa na timu ya Simba katika dimba la kwa Mkapa.

 1. Ama zetu ama zao Do or Die season 2
  Msemo mwingine ambao unaweza kuuita wa mwisho katika mashindano haya, ni huu msemo wa ama zetu ama zao, kufa au kupona msimu wa 2. Msemo huu umekuwa muhimu sana na umedhihirisha kuwa kwa Mkapa hatoki mtu. Kila shabiki wa michezo ambaye anajua namna ambavyo mchezo wa marudio kati ya Simba na Kaizer Chiefs ulikuwa mchezo mgumu na wenye presha na msisimko wa aina yake. Basi anaweza kubaini ni kwa namna gani Simba walipambana hadi kushinda mchezo huo.

Simba walipoteza mchezo wao wa awali wa robo fainali dhidi ya timu hii Kaizer Chiefs kwa kufungwa bao 4 kwa nunge.

Kama ilivyo ada yao Simba wanasema pamoja na kipigo hicho waliiendeleza kaulimbiu yao kuwa kwa Mkapa hatoki mtu na wakahanikiza kwa kaulimbiu ya ama zetu ama zao kufa au kupona msimu wa pili. Simba wanapambana vilivyo kuonesha kuwa ni ama zetu au ama zao, jasho la mapambano linawavuja.
Kwa Mkapa hatoki mtu Simba wanaibuka na Ushidi wa GOLI 3 kwa nunge. Ingawa wanatolewa kutoka Robo Fainali ya 2020/21 kila shabiki wa Simba anaondoka Kwa Mkapa, akijipiga kifuani kwake na kusema HATUWADAI CHOCHOTE.

Huku wachambuzi, wadau wa soka wakitoa sifa kedekede kuwa Simba imepiga hatua kubwa sana. Nikakumbuka msemo wa Next level Hivi ndivyo Simba walivyoiishi kaulimbiu ya ama zetu ama zao kwa Mkapa hatoki mtu.

Simba anaondolewa kwenye mashindano akiwa kwenye hatua ya robo fainali. Katika robo fainali hii akiwa ameiingia kibabe kwa kuongoza kundi na akikutana na miamba mingine ya soka kama vile Mamelodi Sundawns ya Afrika Kusini, Al Ahly ya Misri, Waydad Casablanca ya Moroko, Esperance de Tunis ya Tunisia na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

Hivi ndivyo ambayo kaulimbiu kuu ya kwa Mkapa hatoki mtu na misemo mbalimbali ilivyochagiza mafanikio makubwa ya soka kwa timu ya Simba.

Kaulimbiu na misemo hiyo imetuacha na hadithi ya vipigo kwa timu kama Plateau United, Platnum FC, AS Vita, Al Merrikh na Al Ahly.

Simba anafikia mwisho wa mashindano haya akiwa amecheza michezo 12, akishinda mechi 7, akipoteza 3 akitoka sare mechi 2, akiwa na magoli ya kufunga 17 na kufungwa 9 na akipata hati/mkeka safi (clean sheet) katika mechi 8.

Kongole sana Mohammed Dewji (Mo) mwekezaji thabiti maana tija na rajua imepatikana.

Pia, Mwandada Barbara Gonzalez, mwanamke wa shoka na mtendaji Mkuu wa klabu kwa ubunifu na usimamizi mahiri bila kuwasahau Mwalimu Didier Gomes Da Rosa na Msaidizi wake Seleman Matola (Veron) mtoto wa nyumbani, viongozi wengine,wadau, wanachama, mashabiki wa Simba na wengineo.

Ama kwa hakika tumeona kwa Mkapa hakutoka mtu. Nikakumbuka maneno ya Baraka Mpenja, siku Simba walipocheza na Platimum aliposema; Kwa Mkapa ni uwanja ambao hakuna kisichowezekana, uwanja ambao Simba wanabadilisha yasiyowezekana yakawezekana, yasiyotarajiwa yakatarajiwa, yasiyotabirika yakatabirika na usiyoyaamini ukayaamini…This is another level. Kwa hakika Kwa Mkapa hatoki mtu.

Kwa kuhitimisha niseme tu, pengine hii ni fursa ya vilabu vingine kama Yanga, Azam F.C, Namuongo, Mtibwa n.k kujiimarisha zaidi ili kuendelea kuliinua soka letu la Bongo. Nadiriki kusema Simba wametuhombora, yaani wametuinua kiinchi katika medani za soka la Kimataifa. Kongoleni sana wekundu wa Msimbazi.

0713400079 sovu82@gmail.com
Mshititi Dokta Ahmad Sovu.
Mhadhiri Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kigamboni DSM.

Author: Gadi Solomon