Kisu cha Mkunjo


Kaniita mama Enjo, huyu wakwangu jirani
Kaniomba twende chonjo, anayake mtimani
Kisu changu cha mkunjo, ataka nimuauni
Sikitoi asalani kisu changu cha mkunjo.

Kaongea kwa majonjo, shingo kalaza pembeni
Hatokitia mikunjo, ajuwa yake thamani
Roho yangu inachanjo, kukitoa sitamani
Sikitoi asilani, kisu changu cha mkunjo.

Kisu nimepata Njinjo, ya kule pande za pwani
Nakifanyia uchinjo, kwa nyama zilo laini
Kumwazima mama Enjo, nitaivunja kanuni
Sikitoi asilani, kisu changu cha mkunjo.

Bora afanye mihanjo, akasake madukani
Kuna wahunzi wa Vunjo, wanavyo tele nyumbani
Akikosa ende Sonjo, changu naficha alani
Sikitoi asilani, kisu changu cha mkunjo.

Tamati hili si punjo, beti tano shukuruni
Yabidi nikae chonjo, iliyobaki someni
Ni hivino vina vya “njo” , vinatutesa fanani
Sikitoa asilani, kisu changu cha mkunjo.
©MKANYAJI
HAMISI A.S.KISSAMVU
0715311590
kissamvujr@gmail.com
kutoka (Baitu shi’ri)
MABIBO • DAR ES SALAAM

Author: Gadi Solomon