Kiswahili kilianza kama lugha mama sasa ni ya kimataifa

Na Benard Semen


Neno Kiswahili linatokana ni neno la kiarabu Sawahil lenye maana ya upwa au Pwani. Hivyo, Kiswahili ni lugha ambayo ilizungumzwa na watu wa Pwani ya Afrika Mashariki. Lugha ya Kiswahili ilianza kuzungumzwa tangu mwaka 700 AD, hasa katika Kisiwa cha Lamu na ukanda wa Mto Tana. Ilienea zaidi baada ya mwaka 975 AD wakati Sultan Ali Ibn al-Hassan Shirazi alipoitawala Kilwa, ilienea hadi Kusini mwa mji wa Sofala (kwa sasa Msumbiji) na kuvuka ng’ambo ya mto Zambezi kwani ilitumia katika shughuli za kibiashara.
Lugha ya Kiswahili ilikuwa na lahaja nyingi, baadhi ya lahaja hizo ni Chimiini, Kitikiu, Kisiu, Kipate, Kiamu, kimvita, Kijomvu, Chichifundi, Kimtang’ata, Kitumbatu, Kimakunduchi, kihamidu, Kimwani pamoja na Kiunguja.
Wakati wa utawala wa ukoloni katika nchi za Afrika Mashariki ambazo ni Tanganyika, Zanzibar, Kenya na Uganda, palikuwa na haja ya kuwa na lugha moja itakayotumika katika maswala ya elimu na utawala, hivyo kukawa na haja ya kusanifisha lugha ya Kiswahili. Mwaka 1924 lahaja ya Kiunguja (lahaja ya Zanzibar) iliteuliwa kuwa lahaja ya usanifishaji dhidi ya lahaja zingine.

Januari 1, 1930 iliundwa Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki iliyoitwa Inter Territorial Swahili Language Committee, ilikuwa na jukumu la kuhakikisha nchi zote nne zinatumia lugha sanifu yenye matamshi na maana sawa na kusimamia uchapishaji wa vitabu vya Kiswahili.
Kipindi hiki Kiswahili kilikua na kuenea zaidi kutokana na matumizi yake kuongezeka. Mwitiko wa kutumia lugha ya Kiswahili ulikuwa mkubwa zaidi Tanganyika ( kwa sasa Tanzania) ambapo mwaka 1954 Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) kilianzishwa na Mwalimu Julius Nyerere; chama hicho kilitumia Kiswahili katika harakati za kupigania uhuru. Baada ya uhuru mwaka 1961 serikali ya TANU ilitangaza Kiswahili kuwa lugha ya taifa na mwaka 1962 Kiswahili kilitangazwa kuwa lugha rasmi nchini Tanzania, ambapo lugha hii ilizidi kukua na kuenea zaidi.


Hali ya Kiswahili ikoje kwa sasa?
Lugha ya Kiswahili inazidi kupiga mbiu na kuchanua mbawa zake, hadi sasa imekuwa na kutamalaki dunia nzima.


Hali ya wazungumzaji wa Kiswahili
Wazungumzaji wa Kiswahili wameongezeka zaidi, hadi sasa zaidi ya watu milioni 250 ulimwenguni wanazungumza lugha hii. Vilevile licha ya Tanzania, Kenya na Uganda kuna mataifa mengine ya Afrika na nje ya Afrika yanatumia lugha ya Kiswahili katika mawasiliano kama vile, Malawi, Zambia, Kongo, Ethiopia, Sudan, Burundi, Somalia, Madagascar, Comoros, Msumbiji na Oman.


Kiswahili katika elimu
Nchini Tanzania Kiswahili ni lugha ya kufundishia ngazi za shule za msingi na kinafundishwa kama somo ngazi za sekondari na vyuo, hali kadhalika mataifa mengine ya Afrika yanafundisha Kiswahili kama somo. Kwa mfano, Kenya, Uganda na Rwanda.

Mathalani, zaidi ya vyuo vikuu 100 duniani zinafundisha Kiswahili kama somo baadhi ya vyuo hivyo ni Chuo Kikuu cha Ohio, Chuo Kikuu cha St. Lawrence, Chuo Kikuu cha Columbia na Chuo Kikuu cha Howard zilizopo Marekani, vilevile Chuo Kikuu cha SOAS na Chuo Kikuu cha Edinburgh zilizopo Uingereza, Chuo Kikuu cha L’Orientale di Napoli kilichopo Italia, Chuo Kikuu cha Hamburg na Chuo Kikuu cha Leipzig zilizopo Ujerumani, Chuo Kikuu ya Beijing na Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Tiajing zilizopo China, Chuo Kikuu cha Tokyo kilichopo Japan, Chuo Kikuu cha York cha Korea Kusini, Chuo Kikuu cha St. Petersburg na Chuo Kikuu cha Taifa cha Moscow zilizopo Urusi, Chuo Kikuu cha Sebha na Chuo Kikuu cha Tripoli zilizopo Libya, Chuo Kikuu cha Ghana kilichopo Ghana na vyuo vingine. Kwa upande Tanzania na Kenya zaidi ya Vyuo vikuu 10 zinafundisha somo la Kiswahili.


Kiswahiki katika vyombo vya habari
Hali kadhalika, zaidi ya vyombo vya habari 100 duniani zinatumia lugha ya Kiswahili kurusha habari na matangazo. Kwa mfano, British Broadcasting (BBC) ya Uingereza, Deutsche Welle (DW) ya Ujerumani, Voice of America (VOA) ya Marekani, China Radio International ( CRI) ya China, Sauti ya Afrika ya Libya, Redio Rwanda ya Rwanda, Redio Uganda ya Uganda na redio zingine, lakini kwa Tanzania na Kenya zaidi zaidi vyombo vya habari 20 zinatumia lugha ya Kiswahili.


Kiswahili katika Jumuiya za Kimataifa
Kiswahili pia ni lugha rasmi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na Bunge la Afrika. Vilevile ni mojawapo ya lugha za utendakazi katika Umoja wa Mataifa (UN). Hali kadhalika, Kiswahili ni lugha ya nne rasmi ya mawasiliano katika shughuli za Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), maamuzi haya yalilidhiwa katika mkutano wa 39 wa viongozi wa SADC waliokutana jijini Dar es Salaam, Tanzania mnamo Agosti 2019.
Kutokana na mafanikio ya lugha hii, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kupitia mkutano mkuu wa 41 uliofanyika Novemba 23, 2021 jijini Paris, Ufaransa; Shirika liliteua Julai 7 kuwa Siku ya Kiswahili duniani kila mwaka, chini ya Azimio namba 41C/61 na kufanya Kiswahili kuwa lugha ya kwanza ya Afrika na ya saba duniani baada ya Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani, Kiarabu, Kichina na Kirusi kuwa na siku maalumu ya kuadhimishwa inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa.

Author: Gadi Solomon