Kiswahili kufundishwa Afrika Kusini

Lugha ya Kiswahili itaanza kufundishwa shuleni nchini Afrika Kusini hivi karibuni, baada ya safari ya mazungumzo iliyoanza mwaka 2018 kuleta matokeo bora kupitia makubaliano rasmi yatakayotiwa saini leo hapa nchini.

Kiswahili, lugha rasmi ya Taifa hapa nchini, imeendelea kupenya duniani, hali iliyosababisha Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi na Utamaduni (Unesco) kutangaza kila ifikapo Julai 7, kuwa siku ya lugha ya Kiswahili Duniani.

Katika maadhimisho hayo kesho, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wa Tanzania, Profesa Adolf Mkenda na Waziri wa Elimu ya Msingi nchini Afrika kusini, Angelina Motshekga watarasimisha ufundishaji wa Kiswahili nchini Afrika Kusini.

“Tuko hapa kufuatilia kile tulichokuwa tayari tumejitolea kuhusiana na ufundishaji wa Kiswahili katika nchi yetu, safari ambayo ilikatizwa na Uviko-19,” amesema Motshekga alipotembelea  shule ya msingi Uhuru mchanganyiko jijini hapa.

“Kwa kukamilika kwa makubaliano ambayo tutasaini kesho tutashirikiana katika maeneo ya mitaala, kuona jinsi ya ufundishaji wa Kiswahili, mafunzo ya ualimu, kubadilishana nyenzo na zana za tathmini” amesema.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamiseni), David Silinde alisema kwa Watanzania kuenea kwa lugha ya Kiswahili ni fursa kwao.

Author: Gadi Solomon