Kiswahili kupewa kipaumbele mkopo elimu ya juu

Na Pelagia Daniel

Serikali imetenga Sh570 bilioni zitakazowafaidisha wanafunzi 205,000 huku wanafunzi 500 watapata ruzuku ya Sh3 bilioni. Katika fedha hizo zinazojumuisha mkopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, kipaumbele kitakuwa kwa watakaochukua masomo ya lugha mathalani lugha ya Kiswahili.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda akizungumza katika hafla ya kuzindua mwongozo wa uombaji wa mkopo kwa elimu ya juu amesema lengo la kutoa kipaumbele hicho ni kupata wakalimani wengi zaidi.

“Sasa kuanzia mikopo ya mwaka huu 2022/23 wale watakaosoma Kiswahili, ukalimani watawekwa katika kundi la kwanza kwa hiyo watapewa upendeleo mkubwa zaidi wa kupata mkopo ili wasome chuo kikuu”, amesema Mkenda.

Lengo lingine ni kupata watu wanaoweza kuzungumza Kiswahili na kiingereza kwa ufasaha pamoja na lugha nyingine za kigeni ili kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili duniani.

Mkenda amewahimiza waombaji mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2022/23 kusoma ns kuzingatia mwongozo uliotolewa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ili kuwasilisha maombi sahihi.

Dirisha la kupokea maombi ya mikopo kwa njia ya mtandao linatarajiwa kufunguliwa Julai 19 hadi Septemba 30, 2022.

Author: Gadi Solomon