
Na Gadi Solomon na Pelagia Daniel
Dar es Salaam. Kituo cha Utamaduni cha China kilichopo Tanzania, kimepata tuzo kwa mara tatu mfululizo inayotolewa na Kituo cha CCTV Afrika. Tuzo hiyo imekuwa ikihusisha utamaduni majumui wa nchi za Afrika. Vigezo vya ushindani wa tuzo hiyo ulikuwa unawataka watu mbalimbali wanaolezea utamaduni wa jamii yoyote ya Kiafrika na video iliyokuwa imekidhi vigezo iliingia katika ushindani na kujipatia tuzo.
Video iliyopata tuzo inaelezea maisha ya msichana wa Kichina Li Huifang anayesoma shahada ya pili ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki). Video iliyowapa ushindi ililenga kueleza utamaduni wa Waswahili kama picha za Tingatinga, vinyago pia sehemu za vivutio vya watalii kama Zanzibar na sehemu za bandari ya Dar es Salaam.
Video iliyowapa ushindi ilikuwa na jina la “To Meet Tanzania”, wazo la jina hilo ilitokana na namna Li Huifang anavyo shirikiana na Waswahili katika shughuli zake za kimasomo.
“Kwa muda mwingi huwa nashinda na Waswahili, sio tu kushinda nao bali nawaelewa hivyo nikaona hiyo kazi tuipe jina hilo,” alisema Li Huifang.
Mkurugenzi wa Kituo cha Utamaduni cha China hapa nchini, Wang Si Ping akizungumza kwenye ofisi za kituo hicho jijini Dar es Salaam leo Septemba 20, 2022 amesema ushirikiano wa Tanzania na China umesaidia katika kukuza na kueneza utamaduni hasa katika kipengele cha lugha.
Amesema Watanzania wengi wamepata fursa ya kujifunza Kichina kupitia kozi mbalimbali zinazofundishwa katika Chuo Kikuu Dar es Salam na Chuo Kikuu cha Dodoma.
Pia kupitia vyuo hivyo nao Wachina wanapata nafasi ya kujifunza Kiswahili.
Kituo cha Utamaduni wa China nchini Tanzania kilianza kushiriki mashindano ya “China Afrika Youth Video Original mwaka 2019 na kwa awamu zote tatu imepata tuzo.
Si Ping amesema anafurahishwa na jinsi Watanzania walivyokuwa na mwamko wa kupenda kujifunza lugha ya Kichina.
Maoni Mapya