Kongole Kikeke kueneza Kiswahili kwa miaka 20 BBC

Gadi Solomon, Swahili Hub

Jicho la Kiswahili leo limetua kwa mtangazaji mahiri wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) ambaye amejizolea umaarufu kwa namna anavyotumia sanaa kwenye utangazaji kwa kutumia lugha ya Kiswahili.

Mtangazaji huyo kinara kama anavyojiita, amejizolea sifa kutoka nchi mbalimbali ambazo zinazungumza lugha ya Kiswahili Ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zinazozungumza Kiswahili.

Lugha ni Sanaa. Jicho la Kiswahili limeona jitihada binafsi za mtangazaji huyo ambaye ni Mtanzania, ametangaza Ijumaa mwishoni mwa wiki iliyopita kuacha kazi BBC na kwenda kuangalia fursa kwingine bila kutaja anahamia wapi. Kinara huyo wa utangazaji pia amewahi kufanya kazi hapa nchini kwenye televisheni Chanel Ten na ITV.

Kikeke ambaye amezaliwa Novemba 6, 1978, akiwa BBC Swahili amekuwa na mtindo wa kipekee wa utangazaji, huku akijikita kutumia Kiswahili sanifu.

 Akiwa BBC amekuwa balozi wa Kiswahili, tangu anafanya kazi katika redio na kisha baadaye kwenye televisheni.

Akiongea kwa bashasha na kujiamini, Kikeke baada ya kumaliza kipindi chake cha Dira ya Dunia kilichomtambulisha zaidi kwa watazamaji amenukuliwa akisema “Mimi ni Salim Kikeke …kama mtangazaji kinara wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, nimekuwa BBC kwa miaka 20, miaka 10 nikiwa kama mtangazaji wa redio na Mhariri  wa tovuti yetu ya BBC Swahili na miaka 10 kama kinara wa dira ya dunia TV, mara moja moja nilikuwa nasoma matangazo ya Kiingereza katika matangazo yetu ya BBC Focus on Afrika,” aliongea kwa Kiswahili sanifu kilichojaa radha inayomfanya msikilizaji kuendelea kumsikiliza.

“Naondoka hapa kwa ridhaa yangu, wakati mwingine hata uwe na uwezo kiasi gani kukaa mahala pamoja kwa muda mrefu unaweza kuharibu kwa sababu ya wewe mwenyewe kuchoka au wengine kukuchoka. Ni muhimu kufahamu wakati sahihi wa kuteua kuondoka,” alitiririka huku akiongea kwa kujiamini na kwa sauti ya kati.

“Binadamu tumeubwa na miguu ili tutembee, nimesimama hapa kwa takribani muongo mmoja nadhani ni wakati muafa wa mimi kupiga hatua za matembezi na isingekuwa vyema kuondoka kimyakimya… niko hapa kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mwenyezi Mungu ambaye aliniwezesha kufika hapa nilipofika  lakini wako wewe ambao umekuwa ukitufuatilia muda wote katika televisheni na kwenye mitandao yetu ya kijamii,” alisema Kikeke ambaye wakati mwingine alipenda kuimba mashairi ya nyimbo katikati ya kipindi chake.

Pia alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wafanyakazi wenzake wa sasa na wa zamani kwa kufanikisha kile waliyojaaliwa kwa kadi ya uwezo wao kuweza kufanikiwa.

“Nisema tu sina shaka tutaendelea kuonana na kuwa pamoja kwa njia moja ama nyingine katika majukwaa mbalimbali niwatakie usiku mwema muendelee kuitazama BBC,” amesema Kikeke.

Ni wazi kwamba ameacha alama kwa kukitangaza Kiswahili sanifu ndani ya shirika hilojambao ambalo hata wafanyakazi wa BBC, wamekiri wanajivunia utangazaji wa Kikeke kama familia moja kwamba wataendelea kufanya kazi katika misingi imara aliyoiacha Kikeke.

Licha ya marafiki zake kumdadisi kwenye mitandao ya kijamii pamoja na wafanyakazi wenzake aliofanya nao kazi kutaka kujua anakokwenda, Kikeke amewaeleza kwamba anarudi nyumbani Tanzania.

Mtangazaji Kikeke ameacha somo kutumia nafasi yake ya mtangazaji kuwa chachu ya kueneza Kiswahili duniani.

Author: Gadi Solomon