
Kulalamika niyani, katu sioni ajabu,
Ni lalame hadharani, ja abwakaye kalubu,
Taoneka mtu duni, kwayo sioni adabu,
Wewe miye kunisubu, kunisubu si sononi.
Huno wako uraibu, ulio nao mwendani,
Maradhi yano kusibu, yamekukaa moyoni,
Paza sauti swahibu, wasikie ikhiwani,
kunisubu si sononi. wewe miye kunisibu,
Najuwa wako undani, wala siwene ajabu,
Pendo limekusheheni, pamwe tukiwa karibu,
Sitoki mwako kinwani, tuwatanapo ni tabu,
Wewe miye kunisibu, kunisubu si sononi.
Hako ataye kutibu, zaidi ya Rahamani,
Kamwe siwezi jaribu, uipate afuweni,
Kila zama ni kitabu, chakwako ni chazamani,
kunisubu si sononi. wewe miye kunisubu,
Kunisibu kuno ni kwani, yani kuno kunisubu,
Umezingwa na sononi, hata unapata tabu,
Miye nina kosa gani, ni kwani kujiadhibu,
Wewe miye kunisibu, kunisubu si sononi.
Nina muomba Wahabu, Wahabu akuhisani,
Miyaka mingi ajabu, akuweke duniyani,
Pengine waweza tubu, ukapata afuweni,
Kunisubu si sononi. wewe miye kunisubu,
Nakomeleza matini, ninazidi jitanibu,
Usemayo sito jibu, nakuwachia mneni,
Sio kwamba siyaoni, kujibu sina sababu,
Wewe miye kunisibu, kunisubu si sononi.
MKANYAJI
Hamis Ally Kisamvu
0715311590/0784311590
kissamvujr@gmail.com
Mabibo – Dar es salaam
Tanzania
20 – 6 -2023
Maoni Mapya