Lazima Nimuoe-1

Karibu msomaji wetu katika simulizi hii mpya, anza nasi mwanzo hadi mwisho ambapo kila siku tutakuletea hadithi hii katika ukurasa huu wa Swahili Hub, endelea………….

“Wakinikamata wataniua au wataninyonga tafadhali naomba unisaidie niondoke hapa kaka, nina familia inanitegemea, mimi ndio mtoto tegemeo nyumbani tafadhali nisaidie niondoke”

“Kiukweli kesi yako ni ngumu sana, sijui hata nakusaidia vipi ila ngoja tupambane tujue tunalimalizaje maana serikali ya nchi hii haina utani hata kidogo.”

…………Nini kimetokea? anza hapa…………

“NDIO hivyo bwana maisha yamekuwa magumu sana, lakini Mungu anasaidia tunapambana na mkono unaenda kinywani, hili ni jambo la kushukuru.”

“Lakini umewaona wenzetu Abdul na Mudi.. wametoka nje  na wamerudi mambo safi, mimi nawaza niongee nao wanipe mchongo, maana naona hapa ndani kila nikipambana naanguukia pua”

“Kwani jamaa wanafanya kazi gani kule..?”

“Nasikia wameenda kupika pika kwenye meli za mfuta lakini sina uhakika.”

“Aah wewe bhana hata kama anafanya deki lakini mpunga anaoupokea unaonekana mkubwa, tunachotafuta pesa tu, mimi mwanangu hata wakisema nikaoshe vyombo mimi naenda.”

“Haya bhana mwanangu acha mimi nichomoke kuna mshikaji namuwahi hapo mbele, tutachekiana basi au vipi..”
Yalikuwa ni mazungumzo baina ya marafiki wawili waliokutana barabarani na kuamua kuyajadili magumu ya maisha wanayopita kabla ya kila mmoja wao kufikia adhimio la kuagana na kuahidiana kuwasiliana kupitia vifaa vyao vya mawasiliano.

Fredis Ibrahim Nakata ni kijana mwenye umri wa miaka 19, akiwa amemaliza kidato cha nne mwaka 2019, hakufanikiwa kuendelea mbele na badala yake aliamua kujishughulisha na biashara ndogo ndogo kwa ajili ya kuliendesha gurudumu la maisha.

Nyumbani kwao anaishi na mama yake sambamba na dada yake ambaye ana mtoto mmoja lakini baba wa mtoto alikataa ujauzito.

Baba yake Fred tayari alishafariki kabla hata yeye hajamaliza elimu yake ya sekondari, hivyo muda wote huo alikuwa akiishi na mama yake ambaye alikuwa akiuza maandazi kuhakikisha analisha familia yake na watoto wanaenda shule.

“Mwanangu, leo kaja hapa mwenye nyumba anataka kodi yake kabwaaata! hadi majirani wametoka nje nimejisikia aibu sana “

“Daah! hali yenyewe ngumu, si nilimwambia anivulimilie kidogo, kuna pesa natarajia kuipata ndani ya siku chache zijazo”Fred alijibu huku akishika kiuno.

“Sasa kauli hizo inabidi umwambie yeye ukikutana naye, ukiniambia mimi utakuwa unatwanga maji kwenye kinu, mimi kama mwili wangu ungekuwa sawa ningekusaidia, lakini mwili huu ushakuwa mbovu nikitembe dakika 10 naanza kuhema kama nimekimbizwa.”

Yalikuwa ni mazungumzo ya mama Fred muda mfupi baada ya Fred kurudi nyumbani kutoka kwenye mihangaiko yake.

Mazungumzo hayo yaliendelea kwa muda kabla ya kupata chakula cha jioni na kila mmoja kushika njia ya kwenda kupumzisha mwili baada ya pilika pilika za mchana kutwa.

Usiku ulikucha, Fred alijiandaa asubuhi na mapema baada ya kupata kifungua kinywa alitoka kwenda sokoni kisha akarudi kwenye eneo lake la kufanyia kazi ambapo alikuwa amefungua genge dogo lenye nyanya, vitunguu na bidhaa nyingine.

Aliendelea kuuza uza licha ya kwamba biashara ilikuwa ngumu sana kwani kwa muonekano tu genge lake halikuwa na vitu vingi na watu wengi walikuwa wakimpita kwenda genge lililokuwa linapatikana hatua 20 kutoka alipokuwa yeye, genge hilo lilikuwa  maarufu, watu walikuwa tayari kukaa foleni ili kupata huduma, wakati pale kwa Fred pakiwa patupu.

“Kijana kijana kijana……” Ilisikika sauti nzito gengeni kwa Fred na kwa uvivu akanyanyua sura yake kuangalia ni nani aliyekuwa anamwita.

Baada ya kunyanyua uso ambao haukuwa na chembe ya furaha hata ya kuongopa, ghafla Fred akaonekana kuuruhusu mdomo wake kufunguka na kutasabamu kwa kutoa meno nje kutokana na kile alichokiona.

“Heeee! Mudi..! ebanaaa eee kweli pesa haziongopi naona mwanangu unazidi kunenepa tu, kweli waarabu hawana kazi ndogo, umeenda miaka mitatu tu umerudi na shavu la kutosha”Aliongea Fred kwa mshangao.

“Acha kuzingua wewe, mimi mbona nipo kawaida, wewe ndio umefura kama kifaru vile, naona chuma kimekukubali sana”Mudi naye akarudisha mapigo kwa kumpamba Fred.

“Aya bhana, wewe nicheke tu, mwili wa maandazi huu umekaa kaa tu, niambie mwanangu salama lakini? Tanzania umeingia lini?”

“Nimeingia juzi nilikuwa kwenye msiba Tanga, hapa nina siku tatu tu, itabidi nirudi tena Saudia, Nimepewa ruhusa ya muda mfupi kwa ajili ya msiba.”

“Hee! nani kafariki?” aliuliza Fred.

“Nafikiri humjui, ni baba yangu mkubwa anakaa Tanga”

Fred na Mudi ni marafiki wa muda mrefu tangu utotoni, walisoma shule moja na walikuwa wakikaa mtaa mmoja kabla ya mudi kupata mchongo wa kwenda kufanya kazi nchini Saud Arabia kwenye moja ya migahawa.

Baada ya salamu na mazungumzo ya hapa na pale Mudi alimuaga Fred na kumwambia wangeonana baadae atakapokwenda gengeni kwake kupiga stori kwani muda huo alikuwa akihitaji kupumzika kutokana na uchovu wa safari.

Pesa kweli huwa haiongopi, Mudi aliondoka mtaani akiwa amekondeana na hana hata siha wala haiba lakini muonekano wake baada ya kukutana na Fred ulikuwa tofauti kabisa, alionekana kuwa mng’avu usoni hata mavazi aliyovaa yaliakisi ukwasi wa aina yake aliokuwa nao.

Baadaye kweli walikutana gengeni kwa Fred na kupiga stori mbili tatu  wakikumbushiana baadhi ya mambo waliyowahi kufanya enzi zao za utoto.

Mwisho wa mazungumzo Fred aliitumia nafasi hiyo kumuomba Mudi ikiwa kuna nafasi huko yeye ambako anafanya, naye angetamani kwenda kufanya kwani maisha ya Tanzania yalikuwa yamemchosha na anafikiria kutoka huenda naye akabarikiwa.

“Aaah hilo mbona limeisha kaka, kwanza ni kama umeniwahi tu, kiukweli kazi zipo, mimi  nilipanga nije kukwambia tena mshahara ni mzuri tu, lakini kwanza lazima ufuatilie pasipoti alafu mambo mengine yatafuta, ila uhakika wa kazi upo. Kuna migahawa mingi inafatuta wafanyakazi.” alisema Mudi.

“Aaah mwanangu nitashukuru sana, mimi hiyo pasipoti nitapambana niipate tu, maana nishachoka kukaa bongo, kila siku hali inazidi kuwa mbaya tu.” aliongea Fred kwa sauti ya upole iliyoashiria uhitaji.

“Wewe usijali mwanangu, wewe ni rafiki yangu halafu mwanangu sana. Mimi nitakusaidia tu, kazi utapata kwa uwezo wa mungu.”

Mudi alikaa Tanzania kwa siku kadhaa kisha akrejea tena Uarabuni kuendelea kuzitafuta pesa.

“Basi ndio kama nilivyokwambia, hapo wewe kaa tayari na pasipoti yako, ili mimi mambo yakikaa sawa tu nakupa mchongo unapaa, hakuna kuremba tena hiyo,” Mudi alikuwa akiongea huku akinyoosha nyoosha mikono kumwambia Fred ambaye kwa wakati huo alikuwa amemsindikiza uwanja wa ndege wakati anaondoka.

“Babu wewe hilo la pasipoti niachie mimi, yaani kesho tu mimi naanza mchakato wa kufuatilia, sitaki mchezo kabisa,” aljibu Fred kwa msisitizo huku akipiga piga mikono yake.

Haikuchukua muda mrefu sana, Mudi alienda kukaguliwa na kupewa Boarding Pass  tayari kwa ajili ya kuelekea sehemu ya kusubiria ndege ambayo ilimpeleka hadi Doha, Qatar kisha akabadilisha ndege iliyomfikisha Saud Arabia.

Siku mbili mbele kweli Fred alianza mchakato wa kufuatilia pasipoti ili kujiweka tayari muda wowote mchongo utakapotokea lakini changamoto kubwa kwake ilikuwa ni pesa.

Kawaida inamhitaji mtu kuwa na kiasi kisichopungua shilingi 200,000 kwa ajili ya kukamilisha mchakato wote, kwake ilikuwa ngumu kwani hali yake ya kimaisha ilikuwa mbaya sana.

“Nimekupigia tangu asubuhi jamani hupokei na nimekuja hadi gengeni sijakuona, shida nini kaisari wangu,”

“Aaah naumwa bhana, nimeamka kichwa kinanibangua sana, nipo tu nyumbani hata sokoni sijaenda.”

“Jamani unaumwa na umeshindwa kuniambia yaani kama tumegombana..hivi ni kweli Fred..?”

“Sio hivyo Ashura bhana, jana salio liliniishia usiku, hivyo leo tangu asubuhi sijatoka nje, ndio maana unaona sijakucheki malkia wangu”

 “Aya mimi nakuja kukuona na najua tangu asubuhi haujala, nikuletee nini?”

“Wewe leta unachojisikia, mimi nitakula tu kwa sababu yako”

“Mwanaume una mbwembwe yeye, haya ngoja nije”

Huyo alikuwa ni Ashura, mpenzi wa Fred ambaye alianza kuwa kwenye uhusiano naye tangu wakiwa wanasoma elimu ya sekondari.

“Mama jamani hata mimi?” Ilikuwa ni neno la kwanza la Ashura mara baada ya kufika nyumbani kwa kina Fred na kumkuta mama yake akiosha vyombo.

“Nini tena mwanangu?”aliuliza Mama Fred huku akinawa mikono yake.

“Huyu Jambazi anaumwa tangu jana usiku, yeye hajaniambia nawewe mama hujaniambia.”Aliongea Ashura huku akisogea karibu alipokuwa Mama Fred na mkononi akiwa ameshika mfuko mweusi.

“Mwanangu hiyo habari ya kuumwa ndio unaniambia wewe muda huu, mimi najua labda kama kawaida yake kulala kama samaki pono, sijuiii kabisaaa kama anaumwa,”

“Nilikwambia mama humu mtoto huna si bora ungeenda kumbadilisha na gunia la mpunga Morogoro ukapata faida ya kula ubwabwa.”

“Hilo gunia la mpunga nalo kubwa nigewe tu maji ndoo moja namtoa mimi” Mama Fred na Aisha wamezoeana kwa muda mrefu na mbali yakuwa mtu na mka mwanawe walikuwa ni marafiki pia hivyo mara kwa mara wamekuwa wakitaniana na kubwa zaidi Mama Fred alikuwa ni Mndengeleko na Ashura ni Mmakonde, hivyo walikuwa na utani wa asili.

Baada ya mazungumzo ya muda mfupi Ashura aliingia chumbani kwa Fred.…..Itaendelea kesho

Author: Gadi Solomon