Limekwisha

Asante kutuhuisha, rafiki unae nata,
Wala hujatufifisha, unatupaka mafuta,
Nema umeifikisha, kwa kuirusha kauta,
Hili sasa limekwisha,

Hili sasa limekwisha, hili lilokuwa tata,
Naambae anabisha, ni pale atanikuta,
Walio na mshawasha, kilo chao watapata,
Hili sasa limekwisha.

Hili sasa limekwisha, mkia wataufyata
Patakunwa pano washa, hivi punde watajuta,
Mzigo walo mbebesha, atende cheza karata,
Hili sasa limekwisha.

Hili sasa limekwisha, kilio kinafuata,
Rafiki kawalesha, kwa kuwanywisha mafuta,
Bora inavyo nyeesha, ukweli tuta upata
Hili sasa limekwisha.

Hili sasa limekwisha, ndoto mlizo ziota,
Mlikuwa mkiesha, ukweli kuutafuta,
Anga amelisafisha, punde tutaona nyota,
Hili sasa limekwisha.

Hili sasa limekwisha, kongole hino kamata,
Sana watufurahisha, hatukuchukii hata,
Kumbeo ulio rusha, nduguza itawapata,
Hili sasa limekwisha.

Hili sasa limekwisha, kuna koroma na mbata,
Umekuja bainisha, tujue tuka na kuta,
Haraka umewaisha, sie muda tulivuta,
Hili sasa limekwisha.

Hili sasa limekwisha, usiegame kamata,
Unachokula bakisha, usije ukala mwata,
Juu alokupandisha, shinani atakuleta,
Hili sasa limekwisha.

Kwa hapa natamatisha, inawaumiza ngata,
Mzigo mlojibebesha, si mzito katakata,
Hawaa imewachosha, thama leo mnatweta.
Hili sasa limekwisha.

Author: Gadi Solomon