Lisitiri umbo lako

Kakutunuko Jalia, umewashinda wenzako,
Tambolo limetimia, kutunza wajibu wako,
Una mwendo wa Ngamia, usitiri umbo lako,
Watutia hamaniko, umbola ukiachia.

Miguu imetimia, ngozi si ya mchubuko,
Kuona inavutia, sisemi huo muwako,
Ifunike nakwambia, usitiri umbo lako,
Watutia hamaniniko, umbolo ukiachia

Maozi yametulia, ja mwezi wa mchipuko,
Ni raha unapolia, mashavu ya mbonyeko,
Tusije kuangalia, ustiri umbo lako,
Watutia hamaniko, umbolo ukiachia.

Nyoga hebu izuia, uendavyo mwedo wako,
Matatani watutia, kwa hiyo mitikisiko,
Dhambini tutaingia, usitiri umbo lako,
Watutia hamaniko, umbolo ukiachia.

Sauti kakujalia, atukuzwe Mola wako,
Ni tamu kuisikia, tamu kwa manung’uniko,
Nyamaa nakuusia, usitiri umbo lako.
Watutia hamaniko, umbolo ukiachia.

Rasini hayano tia, yatakwayo kwako yako,
Vibaya ukitumia, litakufika anguko,
Kwa mwenzawako tulia, usitri umbo lako,
Watutia hamaniko, umbolo ukiachia.

Hapa nina tamatia, kwa hili langu andiko,
Nimekuonyesha njia, waungwana waendako,
Vivazi ukivalia, usitiri umbo lako,
Watutia hamaniko, umbolo ukiachia.

           MKANYAJI
  HAMIS AS MWINYIMAD KISAMVU
       kissamvujr@gmail.com
      0715311590/ 0784311590
         BAITU SHI'RI(TZ)
           LINDI-CHELEWENI
            TANZANIA
           3-Dec-2022

Author: Gadi Solomon