Lugha ya Kiswahili kuuzwa nje ya nchi

Sute Kamwelwe, Mwananchi

Dar es Salaam. Wakati lugha ya Kiswahili ikizidi kuchanja mbuga kwa kutambulika na kutumiwa na watu wengi ulimwenguni, lugha hiyo inafanywa bidhaa ili kuwanufaisha Watanzania.

Hatua hiyo inakuja ikiwa kuna watumiaji zaidi ya milioni 500 duniani kote wanaotumia lugha hiyo adhimu.

Hayo, yameelezwa Julai 7, 2024 na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro, kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kiswahili duniani (Masikidu 2024), yaliyofanyika kwenye kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) Dar es Salaaam ambayo ni ya tatu tangu kuanzishwa kwake.

Dk Ndumbaro alisema katika kutekeleza hilo lazima machapisho yote ya Kiswahili yafanyikie hapa nchini hivyo ameagiza mabaraza ya Kiswahili ya Bakita na Bakiza kutekeleza hilo sambamba na kuwawezesha watunzi wa vitabu na mashairi na wote wanaojihusisha na kazi zake.

“Pia tunapobidhaisha Kiswahili tunaangazia suala la utangazaji kwa kuwachukua watangazaji wetu kuwapeleka nje katika vituo mbalimbali vya redio na runinga za Kiswahili wakafanye kazi huko.

“Aidha, tutumie sanaa kama muziki, filamu, mavazi lazima tutambue Kiswahili itakua bidhaa kubwa duniani lazima tuchangamkie fursa hii,” alisema

“Lazima tujipange ikiwemo matumizi ya Akili Mnemba , mitandao ya kijamii, kamusi mpya katika kukuza kiswahili na ili kikue lazima tufungamanishe na taknolojia, vijana na mitandao ya kjamii kwasababu lugha inakuzwa na vijana,’ alibanisha.

Aidha alisema mabaraza ya Kiswahili ya Bakiza na Bakita yaendelee kukuza kanzidata ya wataalamu wa kiswahili: “Bakita na Bakiza shikamaneni mje na kamusi ya lugha fasaha ya Kiswahili ambayo tutaenda kuizindua nchini Uganda.”

Dk Ndumbaro alimalizia kusema kwamba tunataka Kiswahili ile kugha rasmi ya saba ya umoja wa mataifa, kwasasa kuna lugha sita na zote hamna hata moja ya kutoka afrika hivyo tunataka lugha ya kiswahili ambayo inakubalika.

Msigwa abainisha namna Kiswahili kitakavyouzwa

Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Gerson Msigwa amezifichua fursa zilizojificha katika ubidhaishwaji wa lugha ya kiswahili kupitia mradi wa Wizara uitwao “Kubidhaishwa Kiswahili”, wenye lengo la kukieneza na kukiuza nje ya Tanzania.

“Watu watajifunza Kiswahili duniani hivyo tutapeleka walimu kwenye vituo 100 na vyuo mbalimbali kukifundisha huko mpango huo ukiwa tayari kuna walimu tutawapeleka katika maeneo pia wadau wetu watakapo kuwa tayari.

“Timepanga kuandaa machapisho mbalimbali tutakaoyasambaza huko duniani kwasababu kenye kujifunza lazma yawepo machapisho ikiwemo kamusi na vitabu mbalimbali.

Msigwa ameongeza kwamba kuna nchi zlizokiswisha itikia zikiwemo Ufaransa, Kenya, Burundi, AFrika Kusini, Rwanda kwa sasa wanakamilisha taratibu kuchukua walimu kwenda kufundisha.

“Nitoe rai kwa vijana wasikibeze kiswahili wale waliopo vyuoni, shule za misingi wajue ni lugha ni utamaduni na biashara ajira yake itakua kubwa, na fursa ni nyingi hivyo wanapaswa kubobea huko kuna mahitaji makubwa,” amesema.

Amesema kuna maofisa wa balozi wamemwambia watapeleka walimu kumi mwezi ujao nchini Marekani na walimu wengne nchini Switzerland.

Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita), Consolata Mushi amesema wameweka mikakati ya kukuza kiswahili isiwe kama chombo cha mawasiliano pekee bali katika nyingine ikiwemo uchumi.

“Lengo letu ni kuwawezesha wadau wapate fursa ikiwemo kufundisha lugha hii na kufanya kazi katika vyombo mbalimbali duniani vyenye idhaa za kiswahili kama ilivyo kauli mbiu yetu ya mwaka huu.

“Tutaendeleza kiswhaili sanifu na hata sasa Serikali imenunua vifaa vya kikalimani kwa ajili ya ukufunzi wa wakalimani na hadi sasa tunao 145 na tunendelea kuwanoa wengine,” amesema Mushi.

Ameongeza kwamba maadhimisho ya leo ni sehemu ya kuitikia wito wa Kiswahili kutambuliwa na Unesco kuadhimishwa mnamo Novemba 23, 2021 ambapo kwa mara ya kwanza yaliadhimishwa Julai 7, 2022, kisha 2023 na leo 2024.

Hata hivyo, Julai Mosi mwaka huu, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeipitisha Kiswahili kuadhimishwa kila ifikapo Julai 7.

Naye, Waziri wa Habari, Vijana, Tamaduni na Michezo Zanzibar, Tabia Mwita amesema maadimisho ya leo ni kuendelea kupeperusha bendera ya Kiswahili. Amesema maadhimisho ya mwaka 2025 yatafanyika visiwani Zanzibar.

“Tunazidi kuwahamasisha Watanzania lakini hata viongozi wetu wanapokwenda nje ya nchi kuendelea kuzungumza kiswahili. Tunataka kuhakikisha Kiswahili kinakuwa bidhaa na kinatuletea kipato,” amesema Mwita.

Naye, Mwakilishi mkazi wa Unesco hapa nchini Michel Toto amesema Kiswahili ni chombo muhimu katika kufundishia, kuwasiliana na hata katika uchumi hivyo hakuna budi kuendelea kufanyakazi kwa pamoja.

Pia, Rais Samia Suluhu Hassan kupitia video iliyorekodiwa akiadhimisha siku hii ya leo amesema Kiswahili kitumike katika kujenga amani na kufundishia maadili mema, kukuza bishara na kufikisha malengo ya maendeleo ya Tanzania na Afrika kwa ujumla.

Maadhimisho hayo yenye kauli mbiu isemayo ‘Kiswahili na Fursa za Maendeleo Duniani’, yameudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kiserikali, kidini, wanafunzi wa vyuo, sekondari, wahadhiri na wawakilishi wa nchi kadhaa hapa JNICC.

Author: Gadi Solomon