Lugha ya Kiswahili yateuliwa tuzo za Hamad Qatar

Gadi Solomon, Mwananchi

gsolomon@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam.

Bodi ya Waandaaji wa Tuzo za Hamad zinazofanyika Doha, nchini Qatar wameiteua lugha ya Kiswahili kwa mara ya kwanza kutumika kwenye Tuzo za Hamad mwaka huu zinazohusu tafsiri ya matini kutoka Kiswahili kwenda Kiarabu na kinyume chake.

Tuzo hizo ambazo zinawalenga watu binafsi, wachapishaji, asasi na taasisi mshindi atazawadiwa kiasi cha Dola 100,000 ambacho ni takriban Sh230 milioni za Tanzania.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu na Katibu Mtendaji, Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita), Consolata Mushi, ameeleza kwamba lugha ya Kiswahili imejumuishwa kwenye tuzo hiyo ikiwa ni siku chache kupita tangu kuiadhimisha kimataifa hapa nchini mwishoni mwa wiki iliyopita.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano wa baraza hilo, Mushi alisema hii ni faraja kwa lugha ya Kiswahili kuteuliwa kwa mara ya kwanza kwenye Tuzo za Hamad ambazo zilianzishwa mwaka 2015.

Amesema mshindi wa tuzo hizo atajishindia Dola za Marekani 100,000 ambazo ni sawa na takribani Sh230 milioni za Tanzania huku baraza hilo pia likiahidi kumzawadia mshindi yeyote atakayepatikana.

“Bakita tunaahidi kumpa zawadi mshindi yeyote ambaye atashinda tuzo hii, lakini kwa sasa hatujaweka kiwango au zawadi ya aina gani tutampa. Natoa wito Watanzania washiriki kwa wingi, na waje ili tupeane mawazo zaidi,” alisema Katibu Mtendaji huyo ambaye ni mtaalamu wa lugha ya Kiswahili.

Mushi amesema hii ni mojawapo ya fursa mpya za Kiswahili ambazo zilikuwa zinajadiliwa na kutarajiwa kufunguliwa katika uga wa kimataifa.

“Natoa wito kwa taasisi, watu binafsi kushiriki kwa sababu kategoria hii inaruhusu ushiriki wa watu binafsi hata mashirika au taasisi,” amefafanua Mushi.

Amesema lengo la tuzo hizo ni jamii za kimataifa wanaozungumza lugha ya Kiarabu waweze kujifunza na kubadilishana maarifa kuhusu utamaduni wa wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili.

Ameongeza kuwa kazi zinazotakiwa kufanyiwa tafsiri ni zile ambazo zimechapishwa katika kipindi cha miaka mitano ili kuweza kupata maudhui yanayohusu jamii katika kipindi cha hivi karibuni.

“Dhamira ya Tuzo za Hamad zimelenga kutambua pia kazi inayofanywa na wafasiri, kuhamasisha pia utamaduni wa Kiarabu pamoja na kushirikiana masuala mtambuka ya kiutamaduni kati ya lugha ya Kiarabu na lugha nyingine duniani,” amefafanua Mushi.

Amesema kwa mtu mmoja anaruhusiwa kutuma kazi moja ya tafsiri lakini kwa mashirika na taasisi wanaruhusiwa kutuma hadi kazi tatu zilizofanywa na wafasili tofauti.

Mwisho.

Author: Gadi Solomon