
Gadi Solomon, Swahili Hub
Dar es Salaam. Baraza la Kiswahili la Zanzibar kwa kushirikiana na Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) wameandaa maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani ambayo mwaka huu kitaifa yatafanyika Zanzibar.
Taarifa iliyotolewa na mabaraza hayo imeeleza kwamba maadhimisho ya mwaka huu yatapambwa na mbio za Swahili Marathon ambazo zitafanyika jijini Arusha Julai Mosi mwaka huu.
Maadhimisho ya mwaka huu kwa mujibu wa taaarifa hiyo imeeleza kwamba tarehe 4 Julai imetengwa kwa ajili ya Siku ya Wanafunzi wa Sekondari na Shule za Msingi.
Vilevile wadau na wapenzi wa Kiswahili watapata nafasi ya kushiriki mdahalo wa wazi utakaofanyika Julai 5.
Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani kwa mara ya kwanza yalifanyika jijini Dar es Salaam Julai 7 mwaka 2022.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na Makamu wa Rais Dk Philip Mpango.
Akihutubia katika maadhimisho hayo, ameliagiza wizara na taasisi za Serikali kutekeleza maagizo yaliyotolewa juu ya matumizi ya Kiswahili akisisitiza mikutano, warsha na mijadala ya umma iendeshwe kwa lugha ya Kiswahili.
“Napenda kuelekeza kama ifuatavyo, jambo la kwanza wizara na taasisi za Serikali ziendelee kutekeleza maagizo yaliyotolewa kwamba nyaraka za mawasiliano za wizara na idara zake ziwe kwa Kiswahili, mikutano, warsha na dhifa ziendeshwe kwa Kiswahili,” alisema Makamu wa Rais ambaye alikuwa mgeni rasmi.
Alisema majina ya barabara, mitaa, mabango, fomu za usaili maelekezo ya matumizi ya dawa zote, bidhaa na huduma pia ziandikwe kwa Kiswahili.
Dk Mpango aliagiza taarifa za miradi na mikataba inayowahusu wananchi ziwe kwa lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha wananchi kuelewa.
“Jambo la pili, taarifa za miradi na mikataba inayohusu wananchi ni lazima ziwe kwa lugha ya Kiswahili, zisiwe kwa lugha ya kigeni pekee lengo ni kuwawezesha wananchi kuelewa kila jambo muhimu katika ustawi wa maisha yao,” amesema Dk Mpango.
Jambo la tatu sheria na kanuni ambazo bado hazijatafsiriwa, zinapaswa kufanyiwa tafsiri kwa kushirikiana na mabaraza ya Kiswahili na ofisi ya mwanasheria wa mkuu wa serikali.
Jambo la nne, aliagiza vyombo vya habari vinavyotumia Kiswahili vihakikishe vinatumia Kiswahili fasaha na sanifu na vizingatie sarufi ya lugha sanifu na ikitokea anayezungumza hatumii lugha sanifu awepo mtu wa kutoa tafsiri ya lugha kwa Kiswahili. Lengo kuwafaanya wananchi waelewe kinachozungumzwa.
Jambo la tano aliagiza kuanzisha vituo vya kujifunzia lugha ya Kiswahili, ameziomba balozi zote ziwatumie wataalamu waliosajiliwa katika kanzi data ya Bakita na Bakiza na kumuasa Waziri asimamie jambo hilo liweze kutekelezeka.
Ameagiza Bakita kwa kushirikiana na Bakiza waendelee kuwa wabunifu katika kuzalisha wa misamiati ya Kiswahili ili kuendana na kasi ya maendeleo ya kisayansi na teknolojia.
Jambo la saba, aliagiza wizara na taasisi husika kuhakikisha mfumo wa kufundisha lugha ya Kiswahili kwa wageni kwa njia ya mtandao (Swahili prime) unatumika kikamilifu.
Maoni Mapya