Chakidu yapongeza mabunge ya Afrika Mashariki kukisambaza Kiswahili duniani


Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (Chakidu) kimeandaa kongamano lililofanyika jijini Washington DC, Marekani
na kuhuhudhuriwa na wajumbe wapatao takribani 200 kutoka maeneo mbalimbali ulimwenguni.

Kongamano hilo lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Havard chini ya uongozi wa Rais wake Prof Leonard Muaka, liliambatana na warsha ya siku moja, mawasilisho ya wajumbe, vikao vya meza mduara na mawasilisho katika ukumbi mzima.

Miongoni mwa waliotoa mada elekezi walikuwa ni Prof Maulana Karenga, Prof Alamin Mazrui na Ustadh Abdilatif Abdala huku Balozi wa Tanzania Elsi Kanza akitoa hotuba ya ufunguzi.

Siku ya Jumamosi washiriki walipata nafasi ya kuburudika katika ‘Usiku wa Mswahili’ ambapo washiriki walipata nafasi ya kula vyakula vya asili ya mwafrik na kujionea mavazi ya Waswahili pamoja na sarakasi.

Mgeni mashuhuri katika sherehe hiiyo alikuwa Balozi Ann Wanjohi, Mkurugenzi wa Utamaduni na Diplomasia nchini Kenya na ambaye pia alitoa hotuba ya kufunga kongamano.

Katika sherehe hiyo kulitolewa tuzo kwa watu na mashirika ambayo yamechangia zaidi katika kukuza na kuendeleza Kiswahili. Kati ya waliotuzwa ni Seneti na Bunge la Taifa la nchi ya Kenya.

Tuzo hizo zilikabidhiwa kwa Balozi Wanjohi kwa niaba ya Bunge.

“Nilieleza sababu kuu ya kutuza Bunge kuwa kutafsiri Kanuni za Kudumu kwa Kiswahili, ” alisema.

Pia Bunge la Tanzania lilituzwa kwa kutumia Kiswahili huku ikielezwa ni miongoni mwa chombo muhimu katika kuharakisha maendeleo ya Kiswahili.

Shirika la UNESCO lilituzwa kwa kuteua Julai Saba kuwa siku ya Kiswahili Duniani. Tuzo ambayo alikabidhiwa Zipporah Musau wa Umoja wa Mataifa.

Prof Maulana Karenga alikabidhiwa tuzo ya ‘Mcheza Kwao’ kwa juhudi zake za kukisambaza Kiswahili hasa Marekani.

Author: Gadi Solomon