UCHAMBUZI: Kiswahili kinaweza kuwa Lingua Franka ya Dunia

Amani Njoka, Swahili

Historia inaonesha kuwa biashara, dini, elimu, siasa na vyombo mbalimbli vilichangia sana kukieneza Kiswahili sehemu nyingi za Tanzania, Afrika Mashariki. Hata hivyo mambo hayo yameendelea kukieneza Kiswahili duniani na kukifanya kizidi kukubalika katika mataifa mengi kwa siku za hivi karibuni. Baada ya Kiswahili kuenea na kuendelea kuenea, hivi sasa lugha hiyo inatumiwa karibu kila sehemu duniani ingawa kwa uchache kwa baadhi ya sehemu.

Nchi kadha wa kadha kama vile Sudan Kusini na Afrika Kusini zimeonesha nia ya dhati ya kutaka kujifunza Kiswahili ikiwemo kutaka kifundishwe mashuleni. Sababu kubwa ya serikali ya Afrika Kusini kufikia maamuzi hayo ni baada ya kuona kuwa lugha zaidi ya 15 zinazofundishwa katika shule za Afrika Kusini ikiwemo Kifaransa na Kijerumani ingawa sio rasmi.

Wakati fulani Waziri wa Elimu ya Msingi wa nchi hiyo, Engie Motshegka alikiri kuwa licha ya lugha hizo kufundishwa, sio rasmi na jambo la kushangaza zaidi ni kuwa kati ya hizo lugha, hakuna lugha yenye asili Afrika.

“Kwa sasa kuna lugha zaidi ya 15 ambazo zinafundisha katika mtaala wa elimu ambazo hata hivyo sio rasmi ikiwemo Kifaransa, Kijerumani na Kimandarini, lakini kwa bahati mbaya zaidi ni kwamba hakuna lugha hata moja ya Kiafrika katika orodha hiyo.” Alisema.

Mjadala huu ulimuibua mwanasiasa wa Afrika Kusini Julius Malema na kudai kuwa kudai kuwa Kiswahili kinaweza kuiunganisha Afrika na kuwa kitu kimoja kwa kuwa kinaenea sana

“Kiswahili kina nguvu ya kuenea mpaka katika nchi ambazo haijawahi kukizungumza na kina uwezo wa kuwaleta Waafrika pamoja. Pia ni moja ya lugha rasmi za Umoja wa Afrika na tuna uhakika kuwa, kwa kuileta lugha hii Afrika Kusini kutasaidia Waafrika Kusini kutangamana kijamii na Waafrka wenzetu.” alisema.

Kwa mtazamo huu wa Afrika Kusini kutoka kwa Waziri wa Elimu na mwanasiasa maarufu Julius Malema kuna jambo limeonekana na limejificha ndani ya Kiswahili. Hakuna ubishi kwamba lugha ya Kiswahili sasa inazungumzwa na idadi kubwa ya watu ulimwenguni na klinachovutia zaidi ni kuwa lugha hii ni ya Afrika.

Dunia ya sasa ni dunia inayohitaji watu kuchangamana na kuingiliana katika nyanja zote za kimaisha. Kama watu hawa wanachangamana na wanatoka katika jamii na mataifa tofauti yanayotumia lugha tofauti, hakuna budi kuwepo kwa lugha moja ya kuwaunganisha kimawasiliano wanapokutana (Lingua Franka).

Lingua Franka ni lugha inayowawesha watu kutoka jamii mbili au zaidi zinazotumia lugha tofauti kuwasiliana. Mfano, kwa Tanzania kuna makabila mengi na pale ambapo watu wa makabila tofauti wanapokutana basi watatumia Kiswahili. Pia Kiingereza kumekuwa Lingua Franka ya dunia kwa kuwa kinawawezesha watu wa mataifa mbalimbali kuwasiliana mathali Waswahili na Waingereza, Waitaliano na Wachina na wengine. Wote hao wakikutana wanalazimika kutumia Kiingereza kwa kuwa hawawezi kuelewana kwa lugha zao.

Mpaka sasa Kiswahili kinazungumzwa Afrika Mashariki, Kati, Kusini kwa kiasi fulani na sehemu nyingine za bara Asia. Pia kuna watu wengine wapo nchi nyingine kama Marekani na Ulaya ambao wao wanaweza kuitumia kwa masomo na shughuli nyinginezo. Takwimu hizo zinafanya wazungumzaji wa Kiswahili kukadiriwa kufikia zaidi milioni 120.

Watu milioni 120 ni wengi sana, hii ina maana kwamba mtu yeyote anapotembelea Afrika Mashariki na Kati hakwepi kukutana na wazungumzaji wa Kiswahili, kila mahali na katika shughuli yoyote. Afrika Mashariki ina kila kitu kinachoweza kuwavutia wageni ikiwemo utalii, masomo, uwekezaji, biashara na shughuli nyingine za kibinadamu. Maana yake ni kwamba Kiswahili kinapaswa kuwa daraja la kuwaunganisha watu hawa. Kiswahili hakikwepeki katika maeneo yafuatayo.

Biashara, ni shughuli muhimu zaidi ya kibiasharab iliyowaunganisha watu wa jamii taofauti tangu kale. Ni biashara iliyowafanya Waraabu kuja pwani ya Afrika Mashariki. Biashara iliwafanya Wareno na Waingereza waanze kufanya safari za mbali duniani kutafuta malighafi kwa ajili ya biashara. Hakuna namna ambavyo biashara inaweza kuepukwa na binadamu.

Licha mataifa ya nje ya Afrika kuja Afrika Mashariki kufanya biashara, raia wengi wa Afrika hutembelea Afrika Mashariki kwa ajilin ya biashra mathalani mataifa ya Afrika ya kati kama Kongo kutumia bandari za Dar es Salaam na Mombasa. Wageni hao wanapotembelea Afrika Mashariki hulazimika kutumia Kiswahili. Matumizi ya Kiswahili huwaunganisha Wafanyabiashara kutoka mataifa yasiyozungumza Kiswahili na yasiyozungumza Kiswahili na kufanikisha biashara zao.

Utalii, wageni wengi hasa nje ya Afrika huwa na utamaduni wa kutalii. Uwapo wa mbuga za wanyama kama Serengeti, hifadhi ya Ngorongoro na nyinginezo huwafanya wageni kuvutiwa zaidi kutembelea Afrika Mashariki kwa ajili ya utaliui. Kwa kuwa wageni hawa wanakuja katika mazingira mageni basi huamua kujifunza Kiswahili au kuokoteza maneno ambayo angalau yataleta maelewano miongoni mwao na wenyeji. Kwahiyo, hujikuta wakikitumia Kiswahili kama daraja la mawasiliano baina yao na wenyeji.

Shughuli za kibinadamu, hizi husiamiwa na mashirika mengi ya kimataifa na hivyo kuwaleta watu wengi Afrika Mashariki mathalani Tanzania. Mashirika kama Umoja wa Mataifa huleta wafanyakazi wengi kushughulikia matatizo ya kibinadamu kama wakimbizi, maradhi na shughuli ambazo huatangamanisha wafanyakazi na wenyeji ambao wanazungumza Kiswahili. Kwa kufanya hivyo wageni hukifahamu Kiswahili na wanaweza kukieneza kule wanakoenda na kisha kukitumia hukohuko waliko.

Elimu, zipo taasisi za nyingi za kielimu ndani na nje ya nchi na Afrika Mashariki ambazo hutahini wanafunzi kwa ajili ya mafunzo ya lugha ya Kiswahili huwaleta pamoja wanafunzi wa lugha hiyo na kuitumia wakati wa kuwasiliana na hata mazoezi yao ya darasani na hivyo kukifahamu zaidi Kiswahili na kule wanapoenda hukieneza na baadaye kupata wazungumzaji wapya ambao watawasiliana kwa kutumia Kiswahili.

Mikutano ya Kisiasa na Kidiplomasia, hili ni eneo lingine ambalo huwakutanisha wakuu wa mataifa mbalimbali kwa ajili ya masuala yahusuyo nchi zao. Katika mikutano hiyo zipo lugha ambazo huwa ni rasmi kwa ajili mawasiliano na za kuwasilishia mada mbalimbali. Kwa sasa Kiswahili ni lugha rasmi katika Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC). Hatua hii ni muhimu sana na inakuweka Kiswahili katoka uwanja wa kutumiwa na watu wengi zaidi kadri siku zinavyokwenda.

Vyombo vya Habari, ni njia muhimu sana ya kufikisha habari popote pale. Kwa kuwa vyombo vya habari hukusudia kufikisha ujumbe kwa watu, hutumia lugha inayoeleweka kwa jamii. Haja ya mashirika makubwa ya habari duniani kama BBC, Sauti ya Amerika, Redio Ufaransa, Idhaa ya Kiswahili ya DW na mengineyio kuwafikia wasikilizaji wanaotumia Kiswahili popote duniani, kulivilazimu vyuombo hivi kutumia Kiswahili. Kwa vyombo hivi kutumia Kiswahili kumesababisha Kiswahili kuenea na vilevile kuleta maelewano baina ya chombo hicho na watu ambao si wazungumzaji wa asili wa Kiswahili lakini Kiswahili kikatumika kuleta maelewano baina ya pande mbili.

Matumizi ya Kiswahili katika maeneo haya yamekifanya Kiswahili kuendeleo kuzungumzwa na kuenea kwa kasi katika sehemu nyingi duniani. Kwa sababu hiyo, Kiswahili kimekuwa mhimili wa mawasiliano kwa watu wengi na hivyo kuwa Lingua Franka miongoni mwa jamii za watu wanaozungumza lugha nyingi tofauti. Kwa kuwa maeneo yaliyotajwa yanahusisha watu wa kada zote, idadi kubwa ya watu na kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni, kuna kila sababu ya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha muhimu duniani.

Ikiwa Kiswahili kitaendelea kutumiwa na kuzidi kupewa nafasi kitakuwa lugha inayowaunganisha watu wengi zaidi ulimwenguni. Ikiwa mwaka 2020 Kiswahili kitaanza kufundishwa nchini Afrika Kusini itakuwa ni hatua nyingine kubwa kwa Kiswahili kuenea kwa nchi hiyo pia ina ushawishi mkubwa barani Afrika na Duniani na kuzishawishi nchi nyingine zenye mahusiano nazo hasa nchi jirani kujifunza Kiswahili kisha kutumika kama Lingua Franka.

amanizacharyson@gmail.com

0672395558

Author: Gadi Solomon