Aina za maneno katika lugha ya Kiswahili-1

Amani Njoka, Swahili Hub

Neno ni miongoni mwa aina za tungo zilizopo katika lugha ya Kiswahili. Neno ni aina ya tungo iliyo ndogo kuliko sentensi lakini kubwa kuliko kishazi. Licha ya fasili nyingi zilizotolewa na wanaisimu mbalimbali, wengi wanakubaliana kuwa neno ni kipashio cha lugha kinachoundwa mofimu moja au zaidi na kutamkwa kwa pamoja kama sauti moja na kuwa ana maana fulani.

Lugha ya Kiswahili kama lugha nyingine inaundwa na maneno ambayo yakisimama peke yake yanaweza kuwa na maana au yakiungana na maneno mengine ya lugha ya Kiswahili yanaweza kuzalisha sentensi zinazoeleweka kwa wazungumzaji wa Kiswahili.

Ingawa wataalamu mbalimbali wameainisha idadi tofauti ya maneno katika lugha ya Kiswahili, katika mjadala wetu tutajadili aina saba pekee ambazo ndizo zinazoonekana kuwa kubalifu na kutumika mara nyingi katika lugha ya Kiswahli. Zifuatazo ni aina hizo.

Nomino (N), ni neno linalotaja jina la mtu, cheo, kitu, vitu, jumuiya, mahali au sehemu. Zipo aina tofauti za nomino kama vile nomino za kijamii, nomino za kipekee, dhahania na nyinginezo ambazo tutazijadili wakati mwingine.

Nomino za kipekee ni nomino zenye umahsusi, yaani zinataja majina mahsusi ya watu, mahali na vitu. Mfano wa nomino za kipekee ni kama; Mwanza, Japan, Juma, n.k. Mara nyingi nomino hizi huandikwa herufi kubwa hata kama zitaibuka katikati au mwishoni mwa sentensi.

Mfano wa matumizi ya nomino za kipekee katika sentensi; Amosi alimpiga Jonathan jana. Katika mfano wa sentensi hiyo tumeona nomino ‘Amosi’ imeanza na herufi kubwa na nomino ‘Jonathan’ ikaanza kwa herufi kubwa hata kama ilitokea katikati mwa sentensi.

Nomino za jumla, hizi ni nomino au majina yanayorejelea makundi fulani ya vitu, watu, mahali au hali. hivyo. Mfano, kunaweza kutajwa makundi kama jeshi, kwaya, timu, kikosi na mengine yanayofanana na hayo, ni majina ya jumuiya fulani. Majina haya ynaweza kuandikwa kwa herufi kubwa ikiwa tu yataanza mwanzoni mwa sentensi lakini hayataanza kwa herufi kubwa yakiwa katikati au mwishoni mwa sentensi.

 Chunguza sentensi hizi; ‘Timu yetu ipo imara’ na ‘Sisi tuna timu imara.’ Tunaona nomino ‘timu’ katika sentensi ya kwanza imeanza kuandikwa kwa herufi kubwa kwa kuwa lilitokea mwanzoni mwa sentensi lakini ikaandikwa kwa herufi ndogo ilipotokea katikati mwa sentensi.

Nomino dhahania, ni zile nomino au majina yanayotaja vitu ambavyo vipo kinadharia zaidi, havionekani kwa macho ya kawaida. Nomino hizo ni kama vile, miungu, upepo, majini, mapepo, upendo, huzuni na maneno mengine dhahania na huandikwa kwa herufi kubwa ikiwa zinatokea mwanzoni mwa sentensi au zikisimama kipwekepweke lakini zitaandikwa kwa herufi ndogo ikiwa zitatajwa katikati au mwishoni mwa sentensi.

Sehemu hii ya kwanza imeanza kwa kujadili aina ya maneno kwa kuangalia nomino na aina zake. Wakati mwingine tutaendelea na aina nyingine za nomino pamoja na aina nyingine za maneno.

Mwalimu wa somo na Lugha ya Kiswahili. Kwa ushauri na maoni: 0672395558

Author: Gadi Solomon