Filamu za Kiswahili zinakuza Kiswahili, ziendelezwe

Amani Njoka, Swahili Hub

Leo tutaangalia namna filamu zilivyosaidia kukuza na kukieneza Kiswahili. Hivi sasa kasi ya ukuaji wa Kiswahili imeongezeka ukilinganisha na miaka ya nyuma. Ni nyakati hizi ambazo angalau Watanzania wameanza kukifurahia Kiswahili na kuondokana na dhana kuwa ukiongea lugha ya kigeni kama Kiingereza basi utaonekana mtu wa maana zaidi au msomi.

Siku za nyuma ilikuwa ni kawaida kukuta watu wakiangalia filamu za Kibongo hasa enzi za marehemu Kanumba, kulikuwa na Nsyuka, kulikuwa na Shumileta, miongoni mwa filamu nyingi zilizokonga nyoyo za mashabiki kwa wakati huo.

Hata hivyo kuna wakati soko la filamu liliyumba kidogo hasa baada ya kufariki kwa waigizaji walioaminika katika uigizaji akiwamo marehemu Steven Kanumba, hali hii ilisababisha wapenzi wa filamu za Kiswahili kuona hakuna atakayeweza kuwapa kile walichokuwa wanakipata kutoka katika filamu za Kiswahili hasa za Tanzania.

Pia utandawazi ambao ulisababisha filamu kutoka mataifa mengine kuingia nchini na kuathiri soko la filamu za Kiswahili. Filamu hizi zilipunguza soko la filamu na kusababisha wakati mwingine wahusika kuchanganyab lugha wanapoigiza ukiachilia mbali sababu nyinginezo za kufanya hivyo huku baadhi ya filamu za Kiswahili kuitwa majina ya lugha za kigeni. Kupungua kwa ununuzi wa filamu za Kiswahili ulichangia kudhoofuka kwa ueneaji wa Kiswahili pamoja na utamaduni wake hasa ukizingatia kuwa filamu ni moja ya njia kuu za ujifunzaji.

Hayo yote yaliitikisa tasnia ya filamu za Kiswahili lakini bado imesimama imara. Hivi karibuni filamu za Kiswahili zimerejea kwa kasi hasa tamthilia ambazo zinarushwa na vituo mbalimbali vya televisheni ambazo nazo zinatafsiriwa kwa Kiswahili. Mambo yafuatayo yamesaidia kuimarisha filamu za Kiswahili na hivyo kukieneza Kiswahili.

Kuimarika kwa matumizi ya Kiswahili, katika siku za hivi karibuni katika nyanja mbalimbali. Matumizi ya Kiswahili yamekuwa makubwa kuanzia Afrika Mashariki, Afrika na hata sehemu nyingine za ulimwengu na hivyo kuchochea ukuaji wa soko la filamu za Kiswahili.

Teknolojia, miongoni mwa njia nyingi za kuiimarisha tasnia ya filamu za Kiswahili, hii kuu ambayo filamu za Kiswahili kwa sasa zinaitumia kuwafikia watu wa urahisi mkubwa katika sehemu mbalimbali Afrika na Duniani. Kwa sasa ni rahisi kutazama filamu za Kiswahili kupitia simu za mkononi kupitia mitandao mbalimbali na hivyo kujipatia watazamaji wengi na kuitambulisha lugha ya Kiswahili. Pia teknolojia imesababisha filamu nyingi ambazo sio za Kiswahili kuingizwa katika mfumo wa Kiswahili kupitia tafsiri. Kuimarika kwa tasnia ya filamu za Kiswahili, kunakiimarisha Kiswahili katika mazingira yafuatayo:

Kukieneza Kiswahili, kwa kuwa filamu za Kiswahili zinaenezwa zaidi kupitia mitandao ya kijamii, ni rahisi kufika sehemu nyingi duniani. Kuenea kwa filamu hizi ambazo ni za Kiswahili, kunaathiri moja kwa moja lugha ya Kiswahili kwa kuwa nayo itasambaa zaidi na kujulikana ulimwenguni kote.

Kuongeza idadi ya wajifunzaji wa lugha ya Kiswahili, kuenea kwa Kiswahili ulimwenguni kumeenda sambamba na watu kujifunza angalau kwa kujaribu kukariri baadhi ya maneno ya Kiswahili. Mfano, filamu iliyotengenezwa na kampuni ya Disney iitwayo The Lion King ina wimbo wenye maneno ya Kiswahili ambayo hata wasio wazungumzaji wa Kiswahili hujaribu kuyaimba. Katika filamu hiyo kuna sauti inaimba ‘…uishi kwa muda mrefu mfalme…’ Hii ni faida ya kuenea kwa Kiswahili na hatimaye kinatumika katika filamu na kusababisha watu wajifunze.

Kuutambulisha utamaduni wa Mswahili, kwani kila lugha ina watumiaji wake wenye utamaduni fulani. Uwapo wa filamu za Kiswahili duniani kumesababisha utamaduni wa Mswahili kuenea kwani uhusika wanaouvaa wahusika pamoja, maudhui pamoja mazingira wanayoigizia yanaufanya utamaduni wa Mswahili kuenea mathalani salamu, nidhamu, heshima, mshikamano na ushirikiano ambao huwasilishwa kupitia lugha ya Kiswahili. Pia hata mavazi, vyakula, sherehe na matukio mengine yanayowasilishwa na filamu hizo za Kiswahili huutambulisha utamaduni.

Hata hivyo filamu za Kiswahili zinaendelea kukabiliana na uvamizi wa filamu za kigeni ambazo zimeendelea kupendwa licha ya kutafsiriwa kwa Kiswahili. Watu wengi huvutiwa zaidi na filamu za nje kutokana na ubunifu unaotumika katika uandaaji.

Waandaaji wa filamu za Kiswahili wajitahidi kuwa na ubunifu ambao utawavutia watazamaji wengi zaidi na hatimaye wazipende filamu za Kiswahili. Wakati mwingine watazamaji wanaona kama matukio ya filamu za Kiswahili hasa Tanzania hazina uhalisia ukilinganisha na zile za kigeni. Vilevile maudhui yawe rafiki kwa jamii na familia. Ni vyema kama filamu za Kiswahili hasa Afrika Mashariki zijikite zaidi katika utamaduni wetu ili kuwavutia watazamaji wa ndani nan je ya Afrika Mashariki kwani wataona utofauti.

Baraza la Sanaa na waandaaji wajitahidi kusisitiza matumizi zaidi ya lugha ya Kiswahili ili kuendelea kuikuza na kukieneza sambamba na utamaduni wake kwani ndio mhimili wa Sanaa yenyewe.

Kuwe na ufuatiliaji wa maslahi ya wahusika na waandaji kwa kuweka mikataba inayoeleweka ili wazidi kunufaika na kazi ya uigizaji. Uwapo wa maslahi mazuri utasababisha waigizaji kupata moyo wa kuigiza zaidi na kisha kuzisambaza zaidi filamu hizo.

0672395558.

Author: Amani Njoka