Kiswahili kinaweza kuwa mpatanishi bora wa amani Afrika

Amani Njoka, Swahili Hub

Kifupi: Tayari Kiswahili ni lugha rasmi katika nchi za Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC). Hii ni hatua kubwa kwani watu wa ukanda huo watajifunza Kiswahili na hivyo kuenea.

Historia ya lugha ya Kiswahili ni ndefu na pana sana. Historia hiyo inaanzia tangu enzi za ukoloni mpaka Tanzania ilipopata uhuru 1961. Mwaka 1964 Kiswahili kilikubaliwa na bunge uwa kitumike katika shughulia rasmi. Lugha ilifuatiwa na matumizi makubwa katika shughuli za kisiasa kuanzia 1967 wakati wa azimio la Arusha.

Mpaka sasa Kiswahili kimetumika na kuwa mhimili mkubwa wa utengamano wa watu wote bila kujali kuwa wanatoka katika katika tamaduni tofauti katika makabila zaidi ya 120. Kutokana na ukweli kwamba Kiswahili kimeleta maelewano baina jamii nyingi, ni dhahiri shahiri kuwa lugha moja ya Kiswahili imekuwa nyenzo kubwa ya kuimarisha amani na utulivu nchini Tanzania.

Msingi huu ambao uliwekwa na waanzilishi wa taifa hili huku Mwalimu Nyerere akiwa mstari wa mbele ndiyo ambao mpaka leo umewaleta Watanzania pamoja na kuishi kwa umoja, amani na mshikamano bila kujali ukabila, mirengo ya kisiasa wala dini. Hivi sasa Kiswahili kimeidhinishwa kuwa lugha rasmi katika Umoja wa Nchi huru za Kiafrika pamoja na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara na Kiswahili kuwa lugha pekee yenye mizizi ya Afrika inayozungumzwa katika jumuiya hizo na mikutano yake.

Kulingana na idadi kubwa ya watu kuzungumza Kiswahili kwa sasa, lugha hii inaweza kuwafanya watu hawa kuwa kitu kimoja kwa sababu wataelewana na kushirikiana katika masuala mbalimbali. Ikiwa Kiswahili kitapewa nguvu ya kukubalika zaidi kwa jamii ya Afrika, kinaweza kulifanya bara hili kuwa kitu kimoja na kuepusha mambo mengi. Kutumika kwa Kiswahili miongoni mwa Waafrika wote kunaweza kuwa na manufaa yafuatayo:

Kuepusha vita vya kikabila, ukiondoa sababu nyingine zinazosababisha migogoro na vita barani Afrika, sababu iliyo kuu ni ukabila. Ukabila umekuwa saratani mbaya miongoni mwa mataifa haya. Nchi nyingi za Afrika kama Sudan, mauaji ya Kimbari ya Rwanda, machafuko ya Kenya, machafuko yaliyosababishwa na ubaguzi wa rangi wa Afrika Kusini, migogoro ya Afrika ya Kati ingeweza kuzuilika kama watu hawa wangetumia lugha moja. Mfano, machafuko ya hivi karibuni ya Afrika Kusini yangezulika kama Kiswahili kingekuwa ni lugha moja ya jamii tofautitofauti zingekuwa kitu kimoja na kuelewana na kuletwa pamoja na utamaduni mmoja kama vile ambavyo Watanzania wameweza kukaa pamoja kwa mshikamano na amani ilihali kuna makabila zaidi ya 120.

Kuwa na utamaduni mmoja, upo utamaduni ambao umefungamanishwa na lugha ya Kiswahili na utamaduni huu ni bora. Utamaduni wa Waswahili na Watanzania ni kuamini kuwa wao ni kitu kimoja, amani, upendo, mshikamano ni jadi. Kwa sababu ya lugha ya Kiswahili kuwa na nasaba za upendo, amani, mshikamano na ushirikiano, machafuko na migogoro haiwezi kutokea kwa sababu migogoro ambayo husababishwa na chuki haiwezi kutokea.

Kutatua migogoro kirahisi, ipo migogoro ambayo imeshindikana kumalizika au ilichelewa kumalizika kwa sababu ya kukosekana maelewano kutokana na ukabila. Hakuna upande unaotaka kuusikiliza mwingine kwa sababu ya dhana kwamba kabila moja ni bora kuliko lingine. Mfano, mgogoro wa nchini Sudan Kusini kati ya Riek Machar na mwenziye Salva Kiir umechochewa kwa kiasi kikubwa na ukabila wa viongozi hawa.

Licha mikataba mbalimbali ya amani kusainiwa tangu ule wa Januari 2014, 2015 na 2018 bado mambo hayajatengemaa. Imekuwa vita baina ya jamii ya Wadinka ya Kiir na Nuer ya Machar ambazo zote zinataka mtu wao awe rais na kuwa wengine hawafai. Hali imesababisha Wasudan kuishi katika mateso, njaa, hofu, mashaka, ukimbizi na umaskini mkubwa kwa sababu kubwa ya wao kuwa tofauti lakini kama nchi ingeunganishwa na Kiswahili na kuwa jamii moja, kusingeendelea kuwa na vita.

Kurahisisha muingiliano mkubwa wa kijamii miongoni mwa mataifa haya ungesaidiwa kuzuia migogoro. Kwa sababu ya kukaa pamoja watu wa jamii moja kwa muda mrefu, watu wa jamii hizi huhisi kutengwa, kubaguliwa na kunyanyaswa na hivyo kuamua kujaribu kupigania kile ambacho wanaamini wananyanyaswa kwacho.

Tukiirejelea Tanzania kama mfano, tunaona makabila karibu yote yamechangamana na kuamua kukitumia Kiswahili kama lugha ya mawasiliano. Mfano, jiji la Dar es Salaam ni mji ambao una kila aina ya kabila, hapa haviwezi kutokea vita vya kikabila kwa sababu ni nani na nani watakuwa wanapigana na wanapigania nini? Vivyo hivyo hata mikoa mingine. Utakuta Wachaga wapo kila mahali, Wamasai, Wamakonde, Wanyakyusa, Wahaya, Wanyaturu na makabila mengine hayapo tena kwenye mikoa yao bali yamechangamana kwenye maeneo mbalimbali ya nchi na hivyo kusababisha makabila haya kuwa jamii moja.

Kwa maana hiyo, lugha ya Kiswahili na utamaduni wake ikiwa lugha ya Afrika, watu wataingiliana kirahisi kwa sababu wanaelewana na hivyo kuishi kama jamii moja na kuepuka migogoro ya kikabila inayotokana na pande mbili kutokuelewana kwa sababu kunakuwa na mchanganyiko wa watu wa jamii nyingi.

Licha ya Kiswahili kuleta umoja, amani na mshikamano umbao unaweza kuwa suluhisho la migogoro na kuleta amani Afrika, Kiswahili pia kitaleta maendeleo kwa haraka kwa sababu watu wakiwa na amani maana yake watafanya kazi, watasoma, watazalisha na kuleta maendeleo.

Author: Gadi Solomon