Kongole Bunge la Kenya, sasa Kanuni za Bunge ni kwa Kiswahili

Amani Njoka, Swahili Hub

Jana Jumatano tarehe 30 Mwezi Oktoba ndio siku ambayo Bunge la Kenya liliidhinisha rasmi matumizi ya lugha ya Kiswahili katika kanuni za Bunge hilo. Baada ya kuidhinisha, tukio lililofuata ilikuwa ni kuzindua rasmi matumizi ya kanuni hizo na mtu pekee aliyepewa jukumu hilo alikuwa Spika wa Bunge la Jamhuri la Muungano wa Tanzania.

Leo Alhamisi tarehe 31 Oktoba kumefanyika tukio la kihistoria katika viunga vya Bunge la Kenya baada ya shughuli ya uzinduzi wa matumizi ya kanuni za Bunge la Kenya kwa Kiswahili tukio lililofanywa na Spika wa Bunge la Tanzania. Hili ni tukio la kipekee na kihistoria kwa nchi ya Kenya kwani hapakuwahi kufanyika jambo kama hili, ambalo linakuja katika muda ambao Kiswahili kinaenea kwa kasi kubwa.

Pongezi kubwa ziwaendee wabunge wa Kenya kwa kuamua kufanya uamuzi mzuri kwa mustakabali mzuri wa jamii kwani inakielewa na kukizungumza Kiswahili kwa kiasi kikubwa. Naibu Spika wa Bunge la Kenya, Mosses Cheboi aliwaambia wanahabari kuwa wabunge na watendaji wa bunge hilo wanakizungumza Kiswahili na hivyo wanaona ni vyema wakitumie kwa kuwa wakienda kwa wananchi kuomba kura hutumia lugha hiyo. Kwahiyo ni vyema kupitisha hilo na mwezi Februari, 2020 zitaanza kutumika katika shughuli za Bunge hilo. Hili ni jambo la kupongezwa.

Kwa upande wa lugha yenyewe ya Kiswahili, hii ni hatua muhimu katika muendelezo wa kupanuka kwa wigo wa matumizi yake. Ni ishara nzuri kwamba Kiswahili kitatumika katika mhimili muhimu katika serikali na ambao unafuatilia na watu wengi, kwahiyo hata matumizi ya Kiswahili kwa watu yatakua kwani watu watajifunza zaidi ili waweze kuelewa kinachozungumzwa.

Ipo haja sasa ya Kenya kusonga mbele katika matumizi ya Kiswahili katika maeneo mengine muhimu kama sharia na elimu ili kuzidi kupanua wigo wa uelewa wa mambo kwa manufaa ya taifa. Pia, ni somo zuri kwa nchi nyingine ambazo zinatumia zinatumia Kiswahili kama Rwanda, Burundi, Uganda, Sudan na nyinginezo kwani inawezekana kama ilivyowekana kwa Tanzania na Kenya. 

Pongezi pia kwa Spika, Job Ndugai kwa sababu licha ya kwenda kutimiza wajibu wa mwaliko wa Ofisi ya Spika pia ameshiriki katika kukieneza Kiswahili kwa kitendo chake cha kulihamasisha Bunge la Kenya kuzitumia sharia hizo ziliandikwa kwa lugha ya Kiswahili.

Mwisho ingawa si kwa umuhimu, nitoe wito kwa serikali, watafiti, wanafunzi, wasomi na wadau mbalimbali wa lugha ya Kiswahili kuendeleza mjadala na safari ya kuelekea kukitumia Kiswahili katika uga wa elimu, kuanzia shule za awali mpaka vyuo vikuu.

Hii itakuwa hatua kubwa sio tu kwa kuimarika kwa Kiswahili lakini hata maendeleo ya mataifa haya kwa sababu maarifa yatatolewa kwa lugha ambayo inaeleweka zaidi na kuchochea ubunifu, ugunduzi na ujuzi katika Nyanja mbalimbali za maisha ya binadamu na kuharakisha maendeleo. 

Author: Gadi Solomon