Kuenea kwa Kiswahili: Ipo haja ya lugha kufundishwa katika kambi za wakimbizi

Amani Njoka, Swahili Hub

Mkimbizi ni mtu aliyeondoka kwake nyumbani, nchi yake na mahali anapoishi kwa sababu ya kulazimishwa, kufukuzwa au kwa hofu ya kuteswa. Baada ya watu hawa kukimbia makazi yao hatimaye hukutana kambini wakitoka mataifa mbalimbali. Wamekimbia vita na majanga kadha wa kadha yanayotokea katika nchi zao na hatimaye kujikuta kwenye mataifa ya watu na hivyo wanakuwa ugenini aua wakati mwingine ndani ya nchi yao wenyewe.

Tanzania inapokea wakimbizi kutoka nchi kama Burundi, Kongo, Rwanda na nchi nyingine nyingi zilizo nje ya jumuiya ya Afrika Mashariki. Wakimbizi hawa baada ya kufika katika kambi mbalimbali kama Nyarugusu na kwingineko wanakuwa wanaanza maisha mapya mbali na nchi zao.

Wakati wanaanza maisha mapya hukutana na changamoto mpya hasa ya kimawasiliano kwa sababu wapo katika mazingira mapya. Kwa sababu hiyo, wanahitaji mbinu mpya ya mawasiliano. Ili waweze kuwasiliana vyema wanahitaji lugha moja itakayorahisisha mawasiliano miongoni mwao pamoja na wenyeji.

Ipo haja ya wakimbizi kujifunza lugha ambayo haitaleta kutokuelewana miongoni mwao. isipokuwa kuwapa usemi mmoja, kuelewana na kutengamana miongoni mwao.

Kwa kufanya hivyo kutaleta ushirikiano na maelewano miongoni mwao. Mfano, katika kambi kama Dadab ambayo ina idadi kubwa ya wakimbizi kutoka Sudan ambao wanatoka katika makabila tofautitofauti ambayo hayalewani. Kambi ya Nyarugusu ina mkusanyiko wa wakimbizi kutoka Burundi, Rwanda na Kongo ambayo licha ya kwamba wanatoka katika nchi tofauti wanatoka makabila tofauti katika nchi zao lakini wakishafika katika kambi hiyo wakikute Kiswahili na wakitumie kama lugha arsmi.

Wote hawa wanahitaji lugha ya Kiswahili iwaunganishe waweze kuelewana. Inawezekana wanafahamu Kiswahili lakini kisiwe sanifu hali ambayo inaweza kusababisha upotoshaji wa lugha ambayo tunatamani isambae ulimwengu mzima.

Kwa maana hiyo, kuna haja ya wataalamu na walimu wa Kiswahili kuandaa kozi fupifupi ambazo zitafundishwa katika makambi hayo ambazo zitawasaidia kuwa na stadi za lugha ya Kiswahili ambazo zitawasaidia kuishi kwa kuwa na mawasiliano imara kwa kutumia lugtha moja inayoeleweka kwa walio wengi.

Inawezekana wakati mwingine maisha yanakuwa magumu zaidi miongoni mwao kwa sababu ya ugumu wa mawasiliano na kushindwa kusaidiana na hivyo kupata tabu ya kuendesha maisha yao kwa muda mrefu mapaka watakapofahamiana. Vilevile hushindwa kuwasiliana na wenyeji ipasavyo na hivyo kushindwa kuelewana na hivyo kutokusaidiwa.

Ipo haja ya taasisi mbalimbali za kiserikali na binafsi kuchukua jukumu la kuanza kufundisha lugha ya Kiswahili miongoni mwa hawa wakimbizi ambao hata hivyo wakirudi makwao wanaweza kukieneza Kiswahili na kurahisisha uenezaji wa lugha hii adhimu.

Author: Amani Njoka