Serikali ichukue ombi shule chache za mfano kufundisha kwa Kiswahili

Gadi Solomon, gsolomon@tz.nationmedia.com

HIVI karibuni Serikali imesema wanafunzi katika shule 16 nchini watafanya mtihani wa taifa kidato cha nne wa Lugha ya Kichina.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Avemaria Semakafu wakati wa uzinduzi wa kituo cha mafunzo ya Kichina Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro, alisema kwamba kutokana ushirikiano wa China na Tanzania, Serikali kupitia Wizara ya Elimu imeona umuhimu wa lugha hiyo kufundishwa shuleni na vyuoni.

Hiyo ni hatua kubwa kwa nchi yetu kuweza kufungua milango kufanyia mtihani wa Taifa lugha za mataifa mengine.

Pia ni fursa kwa sababu China kwa kuwa imeendelea  kupanua wigo wa lugha hiyo inayotambulisha taifa hilo, kuingia kwenye mtalaa wetu.

Hata hivyo, hoja ya shule 16 za mfano kufanya mtihani wa lugha ya Kichina, inaendana na ombi la wanataaluma wa Kiswahili.

 Kupitia makongamano, mihadhara ya kitaaluma, semina mbalimbali  imeshaelezwa kwamba zitengwe shule za mfano ili wanafunzi wafundishwe kwa Kiswahili masomo yote na wayafanyie mtihani wa Taifa.

Mbunge wa Tabora Kaskazini, Almasi Maige amewahi kuwasilisha bungenihoja binafsi akisema ni wakati mwafaka Kiswahili kikatumika kufundishia shule za sekondari, vyuo vya kati na elimu ya juu.

Pia, Kongamano la Kiswahili lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwenye Ukumbi wa Nkurumah, liliandaliwa na Taasisi ya Taaluma za Kiswahili kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari za Kiswahili Afrika Mashariki ambacho kipo chini ya Kamisheni ya Kiswahili mwaka 2015, liliibua hoja hiyo hiyo..

Mijadala ilitawala ikigusia Kiswahili kutumika katika nyanja mbalimbali za uchumi, siasa, elimu. Taratibu maeneo mengine yameanza kutekeleza maazimio ya Kongamo hilo.

Hivi karibuni Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye alizungumzia hoja ya kuwa na mwongozo wa uwekezaji ulioandikwa kwa Kiswahili.

Hoja yangu kubwa ni kuhusu, Serikali kuamua kutoa fursa kwa wanatalaamu wa Kiswahili kufanyia kazi tafiti zao za kitaaluma zinazoeleza kwamba Kiswahili kinajitosheleza kufundishiwa ngazi zote za elimu, hivyo hatua ya kwanza ni kuanza na shule za mfano.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki), Dk Ernesta Mosha  kwenye uwasilishaji wake wa hali ya Kiswahili na maendeleo nchini kwenye mkutano wa African Academy of Languages (ACALAN) uliofanyika mwishoni mwa mwezi Juni jijiji Da rs es Salaam, pia alieleza utoshelevu wa lugha ya Kiswahili kutumika katika kufundishia.

Ombi kubwa la wanataaluma wa Kiswahili ni kuanza ngazi kwa ngazi. Ziteuliwe shule za mfano. Hatua ya kutafsiri vitabu vya vidato vingine itachochewa iwapo ombi hilo litaridhiwa.

Taarifa ya wanataaluma hao inaeleza kwamba tayari vitabu vyote kwa ajili ya kidato cha kwanza  vimeshaandaliwa.

Kwa maana nyingine nyezo za kufundishia zimeshaandaliwa, kilichobaki ni Serikali kupitia Wizara ya Elimu iruhusu kama ilivyofanya kwa lugha ya Kichina kuteua shule za sekondari ambazo zitatahini wanafunzi mitihani yote kwa lugha ya Kiswahili.

Tunazozipa nafasi lugha za kigeni kuingia kwenye mitalaa yetu, upande wao ni mafanikio makubwa. Upande wa pili sisi tunapaswa kwenda mbele zaidi kwa kuangalia namna ambayo Kiswahili kinaonekana asili yake Tanzania, kinapiga hatua hatua moja mbele.

Si ujinga kutumia Kiswahili, hatutapoteza uhusiano na mataifa ya kigeni, hatutakosa fursa kwenye jumuiya za kikanda iwapo tutaamua kutumia Kiswahili, kwani  masomo ya Kiingereza, Kifaransa Kiarabu, Kireno, Kichina kwa umuhimu wake yataendelea kufundishwa  kama kama somo.

Ninatambua kwamba tayari Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alishatoa mwongozo akisema lugha ya Kiswahili itaendelea kufundisha kama somo kwa sekondari na lugha ya kutolea maarifa itabaki kuwa Kiingereza.

Hata hivyo, bado ninaamini, Serikali haijafunga milango ya wanataaluma na watu wengine kuibua hoja ambazo zinaonyesha kwamba tunayo nafasi kuitumia Kiswahili katika nyanya zote.

Tunayo mifano mingi hapa hapa Afrika Mashariki, Nchi za Burundi na Rwanda zimetumia lugha zao kwa muda mrefu lakini haijawanyima fursa kujumuika kwenye mikutano ya kimataifa, wala haijawanyima fursa ya kuingia jumuiya za kikanda. Pia upande wa Afrika, Nchi za Komoro, Madagasca, Nigeria wametumia lugha zao katika kutoa maarifa kwa wananchi wao shuleni na vyuoni lakini haikuwazuia kujifunza wala kutofahamu lugha za kigeni.

Serikali inapaswa kutambua kumekuwa na ushindani mkubwa Afrika Mashariki katika kuchamkia fursa za Kiswahili ndani ya jumuiya na nje.

Nchini Kenya wamepiga hatu kwenye kuwaunganisha mataifa ya kigeni na Lugha ya Kiswahili. Vituo vingi vya idhaa za Kiswahili vimeweka mizizi yake Kenya zikiamini ndiko kuna Kiswahili.

Walimu wengi wa Kiswahili waliopo ughaibuni ni Wakenya.  Hiyo inatupa changamoto kuongeza juhudi zaidi katika kutangaza Kiswahili na kuzitumia fursa zinapojitokeza.

Hatua ambayo Tanzania itajivunia duniani  ni kuamua kutumia Kiswahili katika nyanja zote za elimu, mahakama na maeneo mengine muhimu.

Ninaamini kwamba tukiendelea kuipuuzia  hoja hii, jirani zetu Wakenya  ipo siku wataibeba na kuitumia kwa vitendo katika Nyanja zote za elimu. Hapo ndipo tutakapoona umuhimu  wa mawazo ya wanataaluma wa Kiswahili nchini.

Mchambuzi ni Coordinator wa Swahili Hub, Mradi wa magazeti ya Mwananchi na Taifa Leo. Anapatikana kwa simu 0712127912 na baruapepe ss.gadner@gmail.com

Author: Gadi Solomon